Wanafunzi walioathirika Hanang wasaidiwa sare, vifaa ya shule

Sehemu ya nyumba za makazi ya Wananchi wa eneo la Jorodom, Katesh Wilayani Hanang likiwa tupu mara baada ya kupitiwa na mafuriko pamoja na maporomoko ya matope na mawe hali iliyopelekea uharibifu unaonekana pichani.
Muktasari:
- Chama cha Makatibu wa Afya Mkoa wa Manyara, (Cahsata) kimewasaidia sare na vifaa vya masomo wanafunzi walioathirika na maporomoko ya tope na mawe na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na makazi.
Hanang. Wanafunzi wa shule za msingi walioathirika na maporomoko ya tope na mawe wilayani Hanang mkoani Manyara wamepatiwa msaada wa sare na vifaa vya shule.
Msaada huo wenye thamani ya Sh2.5 milioni umetolewa na Chama cha Makatibu wa Afya Tanzania (Cahsata), umetolewa leo Jumapili Januari 8, 2024, siku moja kabla ya shule za msingi na sekondari kufunguliwa hapo kesho Jumatatu.
Maporomoko hayo yalitokea alfajiri ya Desemba 3, 2023 na kusababisha vifo vya watu 89, majeruhi zaidi ya 130 na kuharibu miundombinu ya barabara na makazi ya wananchi.
Akikabidhi msaada huo, leo Jumapili, Januari 7, 2024, Mwakilishi wa Katibu wa Afya Mkoa wa Manyara, Thomas Malle amesema msaada huo umegharimu Sh2.5 milioni.
Malle ametaja vifaa vilivyotolewa kuwa ni mashati 100, kaptula 100, sketi 100 na madaftari 1,000.
"Wanachama wa Cahsata baada ya kusikia maafa yaliyotokea Hanang walijichanga na kutoa walichonacho ili kuwasaidia wanafunzi waliopatwa na maafa hayo," amesema Malle.
Amewataka wadau wa elimu kujitoa na kuwasaidia wanafunzi walioathirika kwenye maafa hayo ili waweze kuendelea na masomo yao kwa mwaka 2024.
"Wapo wanafunzi wa shule za msingi watakaofanya mtihani wa kitaifa kwa mwaka huu wa 2024 ikiwemo wa darasa la saba na la nne, hivyo wanapaswa kusaidiwa," amesema Matle.
Akipokea msaada huo Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja amewashukuru Cahsata kwa kuwasaidia waathirika wa maafa hayo na akuwa msaada huo umefika muda muafaka wa shule kufunguliwa.
Mkazi wa Kijiji cha Gendabi, Yasinta Matle amesema “miongoni mwa wanafunzi ambao watanufaika na msaada huo ni wa shule za msingi Gendabi na Jorodom ambazo zilikumbwa na maafa hayo," amesema Matle.