Ujenzi SGR Tabora-Kigoma kukamilisha reli ya Kati

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema utiaji saini wa ujenzi awamu ya pili wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kutoka Tabora kwenda mkoani Kigoma utakapokamilika utatimiza ujenzi wa reli ya Kati na kitakachofuata ni ujenzi wa matawi.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema utiaji saini wa ujenzi awamu ya pili wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha kkutoka Tabora kwenda mkoani Kigoma utakapokamilika utatimiza ujenzi wa reli ya Kati na kitakachofuata ni ujenzi wa matawi.

Kadogosa ameyasema hayo leo Jumanne Desemba 20, 2022 wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa awamu ya pili, kipande cha kwanza (SGR LOT 6 Tabora - Kigoma) iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Amesema ujenzi mwingine utakaofuata ni kujenga matawi ikiwemo Kakiuwa kwenda Mpanda, Uvinza-Msongati na Kisaka kwenda Kigali.

 “Utiaji saini huu unakamilisha manunuzi ya Kilomita 2,102 njia kuu ikiwa ni kilomita, 1,633 na njia za kupishania kilomita 469, kilomita hizi zinafanya Tanzania kuwa nchi yenye ujenzi wa njia ndefu ya SGR barani afrika,” amesema Kadogosa.

Amesema ununuzi wa tawi la Uvinza hadi Kitega Burundi unaendelea ambapo utakapokamilika utaunganisha na watu wa machimbo ya nikeli.

 “Reli hii itakapokamilika itatuunganisha bandari ya Dar es Salaam Kongo kupitia bandari ya Kigoma na kuweza kufikia Uvila, Bukavu, Goma Kalimie na Kugumbashi na kwa ujenzi huu tutakuwa tumefikia miji mikubwa mitatu ndani ya Kongo.

“Hii itakuwa fursa kubwa kwa wafnyabiashara ambapo kipande hicho kina kilomita 516, mkia kuu ikiwa ni kolomita 416 na njia za kupishania kilomita 15,” amesema.

Ujenzi huo unaotarajiwa kuchukua miaka minne hadi kukamilika utagharimu Sh6.34 trilioni huku Tanzania ikiwa imewekeza Sh 23.3 trilioni ikijumuisha kipande cha Dar es Salaam Mwanza na kipande cha Tabora Kigoma.