Ukarabati Mv Liemba kugharimu Sh32 bilioni, kuanza mwezi ujao
Muktasari:
- Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL) inatarajia kuanza ukarabati wa meli ya MV Liemba Februari, 2024 kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
Kigoma. Kampuni ya Huduma za Meli nchini (MSCL), inakusudia kuanza ukarabati rasmi wa meli kongwe ya Mv Liemba, utakaogharimu Sh32 bilioni mapema Februari mwaka huu na matengenezo hayo yatachukua mwaka mmoja na nusu.
Meli hiyo yenye uwezo wa kuchukua abiria 600 na tani 200 za mizigo, ilikuwa ikifanya safari zake kati ya Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC), na kwamba baada ya matengenezo hayo, itarejea kufanya safari zake.
Akizungumza leo Januari 23, 2024 Kaimu Meneja wa MSCL Mkoa wa Kigoma, Allen Butembero amesema wamepeleka maombi Serikali kwa ajili ya kuomba fedha za kuanza ukarabati huo na muda wowote wataingia kazini.
Butembero amesema ukarabati huo awali ulitakiwa uanze Januari, 2024 lakini mkandarasi hakukamilisha baadhi ya taratibu alizoelekezwa, ikiwemo kuwa na mtaji wa fedha za kutosha na kwamba kwa sasa amekamilisha na muda wowote kuanzia Februari, 2024 anaweza kuanza ukarabati.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wafanyabiashara na wasafiri wamesema kukamilika kwa ukarabati wa meli hiyo kutawafanya wawe na usafiri wa uhakika wa mizigo yao na abiria.
Mfanyabiashara wa saruji, Ramadhani Haruna amesema wamekuwa wakitumia boti kusafirisha bidhaa zao ambapo hutumia muda mrefu, huku usafiri huo ukiwa si wa uhakika na kwamba meli hiyo itakapokamilika itawasaidia kuwa na usafiri wa kudumu.
Naye Mwamvua Abdul amesema kukamilika kwa ukarabati wa meli hiyo, hata mzunguko wa fedha utaongezea kwa mkoa huo kutokana na bidhaa kuingia na kutoka mara kwa mara na wafanyabiashara kutumia huduma mbalimbali za kijamii mkoa humo.
“Hii meli imesimama kwa muda mrefu, hivyo itakapokamilika, itatufaa sana sisi wafanyabiashara kubeba mizigo yetu, kwani ni usafiri imara na wa uhakika kuliko boti ambazo zinaweza kupata madhara muda wowote ikiwa njiani,” amesema Mariam Mohammed, mfanyabiashara wa vitengo.