Ukatili wa kijinsia bado janga, wizara yaweka mkakati imara

Muktasari:

Bado matukio ya ukatili yanaendelea nchini licha ya jitihada za Serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya jinsia katika kukomesha matukio hayo.

Bado matukio ya ukatili yanaendelea nchini licha ya jitihada za Serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya jinsia katika kukomesha matukio hayo.

Hali hii inajidhihirisha katika takwimu mbalimbali zinazotolewa na Jeshi la Polisi nchini, ambapo takwimu hizo ni kwa yale matukio ambayo yanaripotiwa katika jeshi hilo huku mengine yakiwa yanaishia kwenye jamii.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura watu 15,131 walifanyiwa ukatili wa kijinsia kati ya Januari hadi Juni 2021, idadi ambayo ni wastani wa matukio 2,522 kwa mwezi na wastani wa matukio 14 kwa siku.

Hata hivyo idadi hiyo ni pungufu ya matukio 4,209 ambayo ni asilimia 21.8 katika kipindi kama hicho mwaka juzi.

Wambura alitaja kuwa maeneo yaliyoongoza katika kipindi hicho kuwa ni Arusha (1,697), Ilala (1,486), Tanga (1,347), Kinondoni (924) na Lindi wenye matukio 780.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kusababisha ukatili wa kijinsia ni imani za kishirikiana, mmomonyoko wa maadili, wivu wa mapenzi, tamaa mbaya za mwili na ulevi uliokithiri.

Hata hivyo, Serikali imechukua jitihada mbalimbali za kupambana na ukatili wa kijinsia miongoni mwake ni mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (MTAKUWWA), kuanzisha madawati ya kijinsia katika vituo vya polisi na namba za simu za bure kwa ajili ya kuripoti matukio hayo.

Mchambuzi wa masuala ya jinsia kutoka shirika la Engender Health, Dk Katanta Msole, anasema kwa sababu masuala ya ukatili wa kijinsia yanafanywa na watu, hivyo ni muhimu wakati programu zinapoanzishwa zilenge kuwafikia watu binafsi ili kuwawezesha kujua dhana ya ukatili wa kijinsia.

“Changamoto kubwa tunayoiona hivi sasa ni watu wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia kutotoa ushirikiano na wana sababu nzuri kwa sababu mtu anayefanya ukatili wa kijinsia anakuwa ana nguvu (mamlaka) au mume au bosi au kiongozi,” anasema.

Anasema jambo hilo limeleta shida kubwa kutoa taarifa na utekelezaji wa programu ambazo zinawawajibisha wafanyaji wa ukatili.

Dk Katanta anasema changamoto nyingine ni ya uelewa watu kufahamu njia na mahali pa kutoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia, lakini pia njia haziko rafiki sana kuweza kumhakikishia anayetoa taarifa kuwa atakuwa salama.

“Serikali na wadau mbalimbali wanafanya kazi na niweze kusema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tunaweza kuona mafanikio,”anasema.

Dk Katanta anasema pia wameweza kuona jukumu la vyombo vya habari hasa mitandao ya jamii katika kuibua masuala ya ukatili wa kijinsia unaofanyika nchini.

Anasema katika miaka mitano iliyopita Watanzania wameshuhudia Serikali ikianzisha MTAKUWAA, sambamba na afua maalum za kuzuia ukatili wa jamii.

“Utashi huo wa kisiasa unaoendelea hivi sasa ni mafanikio hatuna budi ya kusema kwamba tunaishukuru Serikali imeonyesha mazingira mazuri. Na zaidi ya yote Serikali imejenga mazingira mazuri kwa asasi za kiraia kufanya kazi ya kupinga ukatili wa kijinsia na kushirikiana nazo,” anasema.

Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Fatma Toufiq anasema matukio ya ukatili wa jinsia hivi sasa yameshamiri sana, kwani haipiti siku bila kusikia tukio la mtu kufanyiwa ukatili wa kijinsia.

Anasema mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanapaswa kuanzia katika ngazi ya familia na baadaye katika jamii.

“Inaelekea kuna mambo mengine watu wanayaona katika familia zao lakini hawaripoti. Maeneo mengi mama anapigwa, pengine mjomba anambaka mtoto…Na ule mtindo kuwa mtoto unamlaza na mjomba ama mgeni hapana tuache,”anasema Fatma.

Anashauri watoto wafundishwe kukataa na kutoa taarifa endapo kuna mtu yoyote anayetaka kuwashika katika sehemu za siri ama kwenye mwili wake.

Pia anawataka walezi au wazazi kutowapuuza watoto wanaotoa taarifa hizo za viashiria vya ukatili wa jinsia na badala yake kuwa nao karibu, kuwasikiliza na kuchukua hatua.

Fatma anataka msukumo kuwekwa kwa viongozi wa dini, wa mila na wengine wenye nafasi katika kupambana na ukatili wa kijinsia ambao hivi sasa unaonyesha kuongezeka.

Anasema pamoja na juhudi za Serikali katika kupambana na ukatili wa kijinsia, bado nguvu ya Serikali inatakiwa kuhakikisha kuwa elimu inatolewa kwenye shule na jamii.

Pia anasema maeneo ya kutolea taarifa za ukatili wa kijinsia yawe rafiki kwa Watanzania hasa watoto na kutoa mfano madawati yaliyopo katika vituo vya polisi, ambayo watoto hawawezi kwenda kutoa taarifa.

Anashauri kuwepo kwa madawati ya kutoa taarifa shuleni ambayo ni rafiki kwa wanafunzi na vituo vya kijamii vilivyokuwepo miaka ya nyuma, virudishwe ili kutoa mwanya kwa watu wengi kuweza kufika na kutoa taarifa.

“Lakini kwa kweli hali ni tete pamoja na mipango mizuri ya Serikali kuna kamati za Mtakuwa lakini bado ripoti za ukatili zinazidi siku hadi siku,”anasema.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu anasema ni vyema jamii hasa wazazi warudi kwenye majukumu yao ya malezi kwa kuwalea watoto ipasavyo.

“Kamati za MTAKUWWA zinatakiwa kuwa mbadala lakini nguvu kubwa ielekezwe kwenye jamii ili kuzuia ukatili wa kijinsia kuliko kutibu. Kama ukatili anafanyiwa mtoto hawezi kuitafuta kamati hiyo na kuripoti kufanyiwa ukatili wa kijinsia,”anasema.


Mianya katika adhabu

Mbunge wa Viti Maalum Esther Matiko anasema kutokana na kuibuka kwa matukio mengi ya ukatili wa watoto, anafikiria kuwa wanaobainika kufanya hivyo wahasiwe ili kuifanya jamii ya Kitanzania kuwa salama.

“Yanasikitisha sana, (matukio) mengine yanakuwa reported (yanatolewa taarifa) mengine hayawi reported inasikitisha sana hata akipona ataathirika kisaikolojia sasa wapo wangapi katika Taifa letu?,”anahoji.

Anasema wakati fulani anaona kama hizi sheria zina mianya na hivyo kutaka wanaothibitika kufanya vitendo hivyo wahasiwe ili jamii iweze kukaa vizuri.

Anashauri kutafutwa kwa njia nzuri ya kukabiliana na hayo matukio ya ukatili kwa kutenga fedha kwenye wizara zinazohusika kutekeleza kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Anazitaja wizara hizo ni Ofisi ya Rais Tawala za Mitaa (Tamisemi) Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Mambo Ndani, Wizara ya Afya na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, Watoto na wenye Ulemavu.


Mikakati ya Serikali

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima anasema Serikali katika kutekeleza mpango wa MTAKUWAA imechukua jitihada mbalimbali za kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kukuza uelewa wa jamii kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia kwa kutumia njia mbalimbali.

“Jitihada hizi zimewezesha kuongeza idadi ya wanaotoa taarifa za matukio ya ukatili wa kijinsia kwa vyombo husika kwa kipindi cha mwaka 2020/2021 jumla ya matukio 20025 yaliripotiwa ikilinganishwa na matukio 18,270 yaliyoripotiwa mwaka 2019/2020,”anasema wakati akizindua dawati la jinsia katika taasisi za elimu ya juu na ya kati.

Dk Gwajima anasema madawati ya jinsia yanayoshughulikia mashauri ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto 420 yameanzishwa katika vituo vya polisi na katika Jeshi la Magereza yaliyowezesha wananchi kutoa taarifa.

Anasema wameunda na kuimarisha kamati za ulinzi wa wanawake na watoto katika ngazi ya Taifa, mkoa, wilaya, kata na kwenye baadhi ya mitaa, vijiji na vitongoji ambapo hadi sasa kamati 18,186 zimeanzishwa nchini.