Ukatili wa kijinsia washika kasi nchini

Ukatili wa kijinsia washika kasi nchini

Muktasari:

  • Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya jinai (DCI), Camilius Wambura ametaja mambo manne kuwa chanzo cha matukio ya ukatili wa kijinsia.

Dodoma. Licha ya Serikali, asasi za kiraia na wanaharakati kupaza sauti katika kukabiliana na matukio ya ukatili, bado limeonekana ni tatizo.

Hiyo inatokana na taarifa kwamba, jumla ya watu 15,131 wamefanyiwa ukatili wa kijinsia katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni, 2021.

Idadi hiyo ni wastani wa matukio 2,522 kwa mwezi huku kwa siku ikiwa ni wastani wa matukio 14.

Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema kuwa matukio hayo ni pungufu ya matukio 4,209 ambayo ni asilimia 21.8 katika kipindi kama hiki kwa mwaka jana ambako kulikuwa na matukio 19,340.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Camilius Wambura amesema leo Jumatatu Julai 12, 2021 kuwa mikoa inayoongoza kwa matukio hayo ya ukatili ni Arusha (1,697), Ilala (1,486), Tanga (1,347), Kinondoni (924) na Lindi wenye matukio 780.

Amesema katika kipindi hicho matukio 6,009 ya ukatili wa kijinsia kwa yameripotiwa wakati kipindi kama hicho kwa mwaka jana yalikuwa matukio 7,333 hivyo, kuna upungufu wa matukio 1,324.

“Hata hivyo, hali bado si nzuri kwani katika siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mengi licha ya kuwakamata wahusika,” amesema Wambura.

Wambura amezitaja sababu za kuendelea kwa matukio hayo kuwa ni imani za kishirikiana mmomonyoko wa maadili, wivu wa mapenzi na tamaa mbaya za mwili ambapo, amesema jamii inapaswa kubadilika na kuomba viongozi wa dini kusaidia kukemea vitendo hivyo.