Ukosefu wa madaktari bingwa shubiri kwa wananchi Wilaya ya Tanganyika

New Content Item (1)

Hospitali ya halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika inayodaiwa kutokuwa na huduma za upasuaji. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji wa ngiri ya korodani, ngiri ya utumbo, uvimbe, saratani ya matiti, bawasili, ini analazimika kusafiri kwenda hospitali ya rufaa Mbeya, Mwanza, Dodoma, KCMC au Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Katavi. Asilimia 15 ya wagonjwa wa upasuaji wanaopatiwa rufaa Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika kwenda kutibiwa nje ya mkoa, wanadai kushindwa kumudu gharama hali inayosababisha baadhi yao kupoteza uhai wao.

Rufaa hizo zinatolewa kutokana na kukosekana kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya upasuaji hospitalini hapo na mkoa kwa ujumla.

Inaelezwa, mathalani mgonjwa anayehitaji kufanyiwa upasuaji wa ngiri ya korodani, ngiri ya utumbo, uvimbe, saratani ya matiti, bawasili, ini na mengineyo, inamlazimu kufuata huduma hiyo katika hospitali za rufaa za mikoa ya  Mbeya, Mwanza, Dodoma, KCMC au Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Maida Msuna mkazi wa Majalila akionyesha uvimbe shingoni na ameshindwa kwenda Mhimbili kufanyiwa upasuaji kwa sababu ya kukosa fedha. Picha na Mary Clemence

Hali ilivyo ni kuwa  wakazi wengi wa Wilaya ya Tanganyika ni jamii ya wafugaji na wakulima wanaodai kipato chao ni kidogo, hivyo hawawezi kumudu gharama za usafiri, matibabu na mahitaji mengine.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Februari 22, 2024, Maida Msuna mkazi wa kijiji cha Majalila amesema anasumbuliwa na uvimbe shingoni na ameenda hospitali akapewa rufaa ya kwenda kutibiwa nje ya mkoa.

“Angalia kwenye shingo nina uvimbe kichwa kinanisumbua niliambiwa niende Muhimbili kufanyiwa upasuaji nimekosa hela. Kipato changu nategemea nilime vibarua ndiyo nipate hela ya kula na kuwalea wanangu watatu, sina mume wa kunisaidia,” amesema Msuna.

Hata hivyo, amesema amesikia Aprili mwaka huu, kuna madaktari watafika hospitalini hapo kutoa huduma, hivyo anawasubiri.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Alex Mrema amekiri kuwa asilimia 15 ya magonjwa 10 ambayo wagonjwa wamebainika kuugua baada ya vipimo, yanahitaji upasuaji huduma ambayo hawawezi kuipata katika hospitali ya wilaya kutokana na kukosekana kwa madaktari bingwa.

Ili kuwanusuru wagonjwa, Dk Mrema anasema hospitali inalazimika kuwapatia rufaa wakatiwe kwenye hospitali za rufaa mikoa mingine.

“Tumeandaa maandiko, tulichukua miaka mitatu nyuma tukaangalia idadi ya wagonjwa tuliowapa rufaa, tulifanya ufuatiliaji na kubaini wengi hawaendi kutibiwa na baadaye hurudi wakiwa mahututi hadi kupoteza maisha, tukiwauliza ndugu wanasema uwezo wa kuzifuata huduma hawana,” amesema mganga huyo.

Hata hivyo, anasema kama hospitali ya Tanganyika ingekuwa na madaktari hao bingwa, ingesaidia kupunguza madhira wanayokumbana nayo wananchi.

Hata hivyo, anasema tayari wameanza utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma za upasuaji wilayani humo kwa kushirikiana na Shirika la Norbert and Mission (NFM-Bright) ili kunusuru afya za wagonjwa.

“Zaidi ya madaktari bingwa 20 watafika hospitalini kwetu kufanya upasuaji wa magonjwa tofauti, lengo ni kuwapunguzia adha ya gharama za usafiri na mengineyo wananchi,”amesema Mrema.

Naye Mkurugenzi wa shirika hilo, Joel Yalanda amesema huduma hizo zitaanza kutolewa kwa awamu ya kwanza Aprili 6 mpaka 13, 2024, ikifuatiwa na timu ya pili itakayoanza kutoa huduma Mei 3 mpaka 11, 2024.

“Tumelenga kuboresha sekta ya afya, huduma za upimaji zitatolewa bure isipokuwa wananchi watachangia matibabu, mradi huu ni endelevu,”amesema Yalanda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Shabani Juma ametoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi na mikoa jirani kujitokeza kupata huduma hizo.