Ukuzaji wa mfumo endelevu wa kibiashara wa mbegu bora za muhogo nchini

Friday June 04 2021
ittapic1

Wakulima wakiwa wameshika mavuno ya muhogo toka kwenye mbegu bora za mihogo iliyovunwa shambani (IITA).

By Mwandishi Wetu

Huko nyuma, Grace Mvula, mkazi wa kijiji cha Kasera, wilayani Mkinga mkoani Tanga, alipata changamoto nyingi katika kilimo cha zao la muhogo kwa kutumia mbegu za asili.

Hii ilikuwa ni pamoja na muhogo kushambuliwa na magonjwa mawili yanayoathiri muhogo nchini Tanzania na nchi jirani  yaani ugonjwa wa batobato (CMD) na ugonjwa wa michirizi ya kahawia (CBSD), na pia kutofuata kanuni bora za kilimo.

Kutokana na changamoto hizo, mapato yake kwenye zao la muhogo yalikuwa ya chini ukilinganisha na juhudi zake. Magonjwa haya mawili ya virusi husambazwa na inzi wadogo weupe waitwao  Bemisia tabaci na pia kupitia wakulima, bila kujua wanapopeana vipando vilivyoathirika au kurudia kupanda tena vipando vilivyotumiwa misimu iliyopita. Kuwapatia wakulima kama Grace aina mpya za mbegu bora zinazohimili magonjwa na mafunzo ya kanuni bora za kilimo, ndio njia bora zaidi kiuchumi na kiikolojia katika kudhibiti magonjwa na kuongeza uzalishaji wa muhogo ili kuongeza usalama wa chakula na kipato. Hivi sasa, muhogo umekuwa zao la biashara lenye uwezo mkubwa wa kubadilisha sekta ya kilimo na maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima wadogo.

Mradi wa kujenga mfumo endelevu wa uzalishaji na usambazaji mbegu bora za muhogo (BEST Cassava)

Mradi huu umekuwa ukijenga mfumo rasmi na endelevu wa kibiashara wa upatikanaji wa mbegu bora za muhogo ili kufikia azma yake ya kuhakikisha upatikanaji endelevu wa mbegu bora za muhogo kwa wakulima kwa bei nafuu.

Mradi huu wa miaka mitano unaongozwa na shirika la maendeleo MEDA na unatekelezwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo kupitia taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), TOSCI na Taasisi ya Kimataifa ya Kilimo cha Kitropiki (IITA).

Advertisement

Akiwa mmoja ya wanufaika wa mradi huu wa BEST cassava, baada ya kufundishwa kanuni bora za kilimo cha mbegu na muhogo ikiwemo matumizi ya mbegu bora na udhibiti wa magonjwa, Grace alishuhudia ongezeko la mavuno na kipato kutokana na mauzo ya mbegu na mavuno yake ya muhogo ya ziada katika soko la ndani ya mkoa wa Tanga, kilichochomuwezesha kuboresha maisha yake.

“Kutokana na kufuata njia bora za kilimo cha zao la muhogo, nimeshuhudia tofauti ya mavuno na ongezeko la kipato kilicchoniwezesha kuboresha maisha yangu,” anasema Grace.

Kutokana na kuongezeka kwa kipato, Grace amefanikiwa kuongeza ukubwa wa shamba la uzalishaji mbegu bora za muhogo kutoka ekari tatu mwaka 2017 hadi ekari tano mwaka 2020. \

Grace ana ndoto ya kuendelea na biashara ya uzalishaji wa mbegu za muhogo na kuhakikisha anakuwa ‘kinara’ wa kuhamasisha kilimo cha muhogo katika jamii yake, kwa kuwafundisha wanakijiji wenzake juu ya umuhimu wa matumizi ya mbegu bora za muhogo zilizothibitishwa, na kufuata kanuni bora za kilimo cha muhogo ili nao waweze kunufaika na kilimo hicho, kwani mkoa wa Tanga una soko kubwa la muhogo ambalo mahitaji yake bado hayajatimizwa.

Hivi sasa, mradi wa BEST Cassava una zaidi ya wajasiriamali 600 wanaozalisha mbegu bora za muhogo kama Grace waliopo katika ngazi mbalimbali za uzalishaji mbegu, katika maeneo yote yanayozalisha muhogo kwa wingi hapa nchini Tanzania ambako mradi huo unatekelezwa. Wajasiriamali hawa wamefundishwa na kusajiliwa rasmi na wanatambulika na wizara ya kilimo kuwa wafanyabiashara wa mbegu.

Kwa msimu huu wa 2021/2022, kuna jumla ya ekari 2,000 zilizokwishakupandwa mbegu bora za muhogo ambazo zipo tayari kwa ajili ya wakulima wenye mahitaji ya mbegu bora.

Mradi wa BEST Cassava unaendeleza juhudi za miradi kadhaa ya hapo awali:

Hii ni pamoja na kupatikana kwa aina mpya za mbegu za muhogo na zilizo safi kwa ajili ya kupambana na magonjwa ya michirizi kahawia (CBSD) na batobato (CMD), uliojulikana kwa kifupi kama 5CP (New Cassava Varieties and Clean Seed to Combat CBSD and CMD) ulioongozwa na IITA, ambao ulijaribu mfumo wa kuzalisha mbegu bora za muhogo zisizo na virusi na zinazostahimili magonjwa; Muhogo Mbegu Bingwa (MMB), uliotekelezwa na MEDA ambao ulijaribu mfumo rasmi endelevu wa usambazaji wa mbegu safi; na mradi wa ushirikishwaji wa jamii katika kudhibiti magonjwa ya muhogo (Community Phytosanitation) ulioongozwa na kituo cha utafiti cha TARI Kibaha ambao ulishirikisha jamii mbili za mikoa ya Pwani (Mkuranga) na Kaskazini Magharibi (Chato) Tanzania, kwa pamoja, kung’oa mbegu za asili zenye magonjwa na kubadilisha kwa kupanda mbegu bora safi za muhogo zinazostahimili magonjwa.

Ittapic2

Wakaguzi wakiwa shambani kukagua ubora wa mbegu za zao la muhogo (IITA).

Mafanikio ya mradi huu katika kuanzisha mfumo endelevu wa kibiashara wa mbegu safi za muhogo ni pamoja na:

Ugunduzi wa aina mpya za mbegu za muhogo

Mfumo ya mbegu huanza na upatikanaji wa aina mpya za mbegu bora za muhogo zinazotoa mavuno mengi na kustahimili magonjwa. Mradi umebaini aina za mbegu mpya zinazohimili magonjwa ya CBSD na CMD kupitia utafiti uliofanywa na TARI na IITA.

Mradi umeanzisha majaribio ya pamoja na wakulima katika mikoa inayolima muhogo nchini ili kuchagua aina za mbegu za muhogo zinazokidhi matakwa yao na pia kuzizalisha kwa wingi aina zilizochaguliwa. Mradi huu umesaidia kuthibitishwa rasmi kwa aina tisa za mbegu bora mpya nchini.

Kuimarisha mfumo wa uthibiti wa mbegu bora

Uthibiti wa ubora wa mbegu za muhogo ni muhimu ili kuhakikisha wakulima wanapata mbegu za muhogo zisizo na magonjwa. Mradi wa BEST Cassava umekuwa ukiimarisha uwezo wa Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) juu ya uhakiki wa ubora wa mbegu za muhogo.

Hii ni pamoja na kuboresha mwongozo wa ukaguzi wa mbegu za daraja la kuazimia Ubora (QDS) kwa mazao ya vipando kama vile muhogo na viazi vitamu; kutoa mafunzo kwa wataalam wa TOSCI juu ya taratibu za njia ya kisasa ya utambuzi wa virusi na ununuzi wa vifaa vya maabara ili kuongeza ufanisi katika kuhakiki ubora.

Mradi umetoa mafunzo kwa wakaguzi zaidi ya 80 wa mbegu za muhogo wanaoisaidia TOSCI katika uthibiti wa ubora wa mbegu ili kuweza kurahisisha ukaguzi wa mbegu za muhogo katika ngazi za kata ili kuweza kuwafikia wazalishaji wa mbegu za muhogo kwa urahisi zaidi.

Mradi pia umeanzisha mfumo wa kidijitali wa ‘Seed tracker’ kwa ajili ya kufuatilia uzalishaji mbegu za muhogo, usajili wa mashamba ya mbegu, na shughuli za masoko.

Kuhakikisha faida kwa wajasiriamali wazalishaji wa mbegu bora za muhogo

Mradi umeanzisha mfumo wa kibiashara ambao umeweza kuwaunganisha watafiti wanaozalisha aina mpya za mbegu bora pamoja na wakulima wenye uhitaji wa hizo mbegu za mohogo.

Mfumo huu umeonekana kuwa na faida kwa Wajasiriamali wa Mbegu za Muhogo katika ngazi zote, ambapo faida ni motisha ya uzalishaji endelevu wa mbegu za muhogo.

Kwa sasa, kuna wajasiriamali wa mbegu za muhogo zaidi ya 600 waliopata mafunzo na kuthibitishwa waliopo katika maeneo makuu yanayolima zao la muhogo nchini Tanzania ambako mradi wa BEST Cassava unatekelezwa na idadi hii inaendelea kuongezeka.

Uanzishwaji wa teknolojia mpya za kuzalisha mbegu za muhogo kwa haraka

Ili kusaidia uendelevu wa upatikanaji wa mbegu za muhogo kibiashara, mradi huu umeweza kuja na teknolojia mpya ya kuzalisha kwa haraka mbegu za muhogo, inayojulikana kama ‘Semi Autotrophic Hydroponics’ (SAH) kwa kingereza, nchini Tanzania.

Teknolojia hiyo ilitengenezwa na SAHtechno LLC kwa ajili ya viazi na IITA kupitia mradi imeitumia kwa mbegu za muhogo.

Watafiti wa TARI na washirika wengine wamefundishwa juu ya teknolojia na leseni imepatikana kutoka SAHtechno kwa matumizi ya teknolojia ya SAH nchini. Mradi pia umeimarisha uwezo wa wajasiriamali wa mbegu za muhogo wa kawaida sita kuweza kuzalisha mbegu kwa njia ya haraka ya teknolojia ijulikanayo kama “twonode multiplication” kwa kutumia vitalu nyumba.

ittapic3

Mtafiti wa IITA akikagua mbegu za muhogo zilizozalishwa kwa haraka kwa kutumia teknolojia ya SAH (IITA).

Zana za kidijitali

Mradi umeanzisha na unahamasisha matumizi ya zana anuwai za kidijitali kusaidia maendeleo ya mfumo wa mbegu za muhogo. Hii ni pamoja na matumizi ya AKILIMO zana ya kidijitali ambayo inaongoza wakulima kufanya maamuzi ya kilimo.

Inajumuisha mapendekezo maalum ya matumizi ya mbolea, njia bora za upandaji mazao, upandaji mseto na ratiba ya kupanda ili kuhakikisha uvunaji wa mihogo mwaka mzima hii ni muhimu katika biashara ya muhogo.

Zana nyingine ni NURU, ambayo hutambua kwa usahihi majani yaliyoharibiwa na ugonjwa wa batobato (CMD) na ugonjwa wa michirizi ya kahawia (CBSD) na wadudu waharibifu kama utitiri wa kijani na mwekundu.

Ilianzishwa na IITA na Chuo Kikuu cha Jimbo la Pennsylvania, Marekani, na kwa sasa inatumiwa na TOSCI na wajasiriamali wa mbegu za muhogo katika ufuatiliaji wa magonjwa ya muhogo.

Uchechemuzi na uelekezaji

Kupitia kitengo hiki kinaongozwa na IITA, mradi umefanikiwa kuongeza mwamko katika Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) juu ya umuhimu wa matumizi ya mbegu bora na safi kwa wakulima katika kupunguza kuenea kwa magonjwa ya muhogo.

Hii imepelekea baadhi ya Halmashauri kutunga sheria ndogo za kuongoza uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora za muhogo katika maeneo yao. Mamlaka za Serikali za Mitaa mingine pia zimeanza kutekeleza maazimio yao ya kuendeleza mfumo wa mbegu bora za muhogo kama walivyoainisha na kutenga bajeti ya kusaidia mfumo huu.

Hivi sasa, pameanza kuwa na mwamko kwa wakulima kuacha kupeana vipando na kutumia mbegu za zamani na kuanza kununua mbegu safi kutoka kwenye vyanzo vilivyothibitishwa.

Tangu 2017, mradi umeweza kunufaisha moja kwa moja walengwa 46,603 na watu wengine wapatao zaidi ya 213,374 wamefanikiwa kwa njia moja au nyingine mpaka sasa.

Ingawa mradi umeonesha maendeleo makubwa, zipo changa-moto kadhaa zinazoukabili mfumo wa mbegu bora za muhogo kote nchini. Jitihada za kuzitatua zitaendelea chini ya awamu ya pili ya mradi wa BASICS II.

Mafunzo yaliyotokana na juhudi za mradi huu ni pamoja na:

Utangamano na uratibuIli kuunda mfumo endelevu wa kibiashara wa mbegu bora za muhogo wahusika wote wanahitaji kuwa na makubaliano ya pamoja juu ya jinsi ya kufanya biashara ya mfumo wa mbegu na kufanya kazi pamoja kufikia lengo moja.

Ushirikiano

Ushirikiano huleta kukubalika, kukuza biashara, kuhamasisha mabadiliko ya sera, na kuharakisha mchakato kwa wadau wote.

Uchechemuzi

Utashi wa kisiasa ni muhimu sana katika kufanikisha mfumo wa mbegu kibiashara. Uchechemuzi ni muhimu ili kupata msaada wa kisiasa kutoka kwenye mifumo ya serikali.

Faida

Faida ni motisha nzuri kwa wadau kwa ajili ya mfumo endelevu wa mbegu. Wazalishaji wa mbegu wanapoona faida, wataendelea kuzalisha mbegu bora za muhogo.

Kupatikana kwa mbegu za awali kutoka utafiti

Watafiti wanaohusika na mbegu za kizazi cha awali wanahitaji kuwa na mwelekeo wa kibiashara na, ikiwezekana, sekta binafsi iruhusiwe kuzalisha EGS ili kusaidia mnyonyoro wa kibiashara wa mbegu.

Ushahidi wa ukuaji wa mahitaji

Wakulima watanunua mbegu iwapo wataona faida dhahiri.

Mipango

Anza na wajasiriamali sahihi. Mtindo sahihi wa biashara katika kiwango tofauti cha mfumo wa mbegu ni muhimu sana.

Kujenga uwezo na uendelevu

Kujenga uwezo katika shughuli zote ni muhimu kwa uendelevu.

Soko la mazao

Uunganishaji wa soko la mazao (muhogo) ni muhimu sana kwa mfumo endelevu wa kibiashara wa mbegu za muhogo.


itaapic4

Wakulima wakifunga vipando vya mbegu bora za muhogo(MEDA).


Advertisement