Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ukweli kuhusu Gen Z kuwa kizazi chenye afya bora

Muktasari:

  • Wataalamu wa afya nchini wanasema kizazi hicho kinaonyesha mafanikio makubwa katika baadhi ya maeneo ya afya, huku kikikabiliwa na hatari mpya ambazo hazikuwepo kwa kiwango kikubwa kwa vizazi vya nyuma

Dar es Salaam. Wakati kizazi cha Gen Z kikionekana kuwa na mwamko mkubwa kuhusu masuala ya afya kuliko vizazi vilivyotangulia, vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na mazoezi ya mwili, kufuatilia taarifa za afya kupitia mitandao ya kijamii na kuzungumzia afya ya akili kwa uwazi zaidi.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanasema pamoja na mafanikio hayo, kizazi hicho kinakabiliwa na changamoto mpya zinazotokana na matumizi makubwa ya teknolojia, mabadiliko ya mtindo wa maisha na ongezeko la utegemezi wa mifumo ya kidijitali, hali inayoweza kuathiri afya ya mwili na akili kwa namna mbalimbali.

Gen Z, inayojumuisha vijana waliozaliwa kati ya mwaka 1997 na 2012, wamekuwa wakitajwa kuwa kizazi chenye afya bora zaidi kutokana na upatikanaji wa taarifa na ongezeko la uelewa kuhusu masuala ya afya.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaonya kuwa mafanikio hayo hayawezi kupimwa kwa kuangalia upande mmoja pekee, kwani bado kuna changamoto zinazohitaji kushughulikiwa.

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Asha Mwinyi, amesema Gen Z wameonyesha mabadiliko makubwa katika namna wanavyotazama afya zao ikilinganishwa na vizazi vilivyopita.

“Vijana wa sasa wanajua zaidi kuhusu afya kuliko vizazi vilivyopita. Wanazungumzia afya ya akili, wanajihusisha na mazoezi na wanafuatilia taarifa kupitia mitandao. Lakini bado kuna changamoto kubwa za kitabia na kimazingira,” amesema Dk Asha.

Amesema pamoja na ongezeko la maarifa kuhusu afya, bado vijana wengi wanashindwa kuyageuza maarifa hayo kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.

“Maarifa waliyonayo yanahitaji kugeuzwa kuwa vitendo vya kila siku. Ndipo tutakapoweza kusema kama kweli ni kizazi chenye afya bora au la,” amesema Dk Asha.

Takwimu zisizo rasmi kutoka kwa wataalamu wa afya ya jamii zinaonyesha kuwa vijana wengi mijini wameongeza ushiriki wao katika mazoezi ya viungo, ikiwamo gym, kukimbia na michezo mbalimbali.

Hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na maudhui ya afya na mwonekano wa mwili yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kuwa matumizi makubwa ya simu za mkononi na kompyuta yameibua changamoto mpya ya maisha ya kukaa muda mrefu bila kufanya shughuli za kutosha za mwili.

Mtaalamu wa lishe na mazoezi, Neema Lema, amesema hali hiyo inaweza kupunguza manufaa yanayotokana na mazoezi.

“Ni kweli vijana wengi wanafanya mazoezi, lakini muda mwingi zaidi wanakaa kwenye simu au kompyuta. Hii inasababisha mwili kukosa shughuli za kutosha, na hatimaye kuongeza hatari ya unene, kisukari na magonjwa ya moyo,” amesema Neema.

Kuhusu  matumizi ya tumbaku, imeelezwa kuwa  kumekuwa na mabadiliko chanya kutokana na kupungua kwa matumizi ya sigara za kawaida miongoni mwa vijana wa sasa ikilinganishwa na vizazi vilivyopita.

Hata hivyo, kuongezeka kwa matumizi ya sigara za kielektroniki na shisha kumeibua wasiwasi mpya kwa wataalamu wa afya.

Daktari wa magonjwa ya mapafu, Dk Baraka Mushi, amesema vijana wengi wanaamini kuwa kuvuta shisha ni salama kuliko sigara za kawaida, jambo ambalo si sahihi.

“Hii ni dhana potofu. Shisha ina kemikali zinazoweza kuathiri mapafu na mfumo wa upumuaji. Vijana wengi hawajui madhara ya muda mrefu,” amesema Dk Mushi.

Mbali na lishe, wataalamu wamebainisha kuwa ukosefu wa usingizi wa kutosha ni changamoto nyingine inayoongezeka miongoni mwa vijana wa kizazi hicho.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, matumizi ya simu hadi usiku wa manane yameathiri ratiba za usingizi kwa vijana wengi, jambo linaloweza kuathiri afya zao kwa ujumla.

“Vijana wengi wanalala saa nne au tano tu kwa usiku, wakati wanatakiwa kulala angalau saa saba hadi nane. Hii inaathiri afya ya ubongo, umakini na hata kinga ya mwili,” amesema Dk Mushi.

Katika eneo la afya ya akili, Gen Z wanaonekana kufanya vizuri zaidi kuliko vizazi vilivyopita kwa kuwa tayari kuzungumzia changamoto zao za kihisia na kutafuta msaada wanapouhitaji.

Mtaalamu wa saikolojia, Rehema Kimaro, amesema hatua hiyo ni mabadiliko makubwa katika jamii ambayo kwa muda mrefu iliona masuala ya afya ya akili kama jambo la kufichwa.

“Hii ni hatua kubwa ya maendeleo. Vijana sasa wanaelewa umuhimu wa kuzungumza kuhusu afya ya akili. Hata hivyo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa huduma na unyanyapaa katika baadhi ya jamii,” amesema Rehema.

Amesema pia shinikizo la kufanikiwa haraka, ukosefu wa ajira na ushindani unaojengwa kupitia mitandao ya kijamii vimechangia kuongezeka kwa msongo wa mawazo miongoni mwa vijana.

"Gen Z wana fursa kubwa zaidi ya kujenga kizazi chenye afya bora kutokana na upatikanaji wa taarifa na teknolojia. Hata hivyo mafanikio hayo yatategemea uwezo wao wa kubadili maarifa waliyonayo kuwa tabia na maamuzi sahihi ya kila siku yanayolinda afya zao za sasa na za baadaye".