Ulega aagiza barabara ya Bigwa – Kisaki ipitike wakati wote wa ujenzi
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akizungumza leo Julai 14, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo mkoani Morogoro.
Muktasari:
- Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akisisitiza kuwa ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha maeneo yanayotumiwa na wananchi yanakuwa katika hali nzuri ili kurahisisha usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji.
Morogoro. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na mkandarasi anayejenga barabara ya Bigwa – Kisaki yenye urefu wa kilomita nane, kuhakikisha inapitika wakati wote wa ujenzi.
Ulega ametoa agizo hilo leo Julai 14, 2026 wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo mkoani Morogoro, akisisitiza kuwa ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha maeneo yanayotumiwa na wananchi yanakuwa katika hali nzuri ili kurahisisha usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji.
Amesema haikubaliki kwa wananchi kuendelea kutumia barabara yenye mashimo makubwa wakati mkandarasi yupo eneo la mradi, akieleza kuwa matengenezo ya mara kwa mara ni sehemu ya wajibu wake.
“Ni lazima barabara ipitike vizuri katika eneo lote ambalo ujenzi unaendelea. Hili si jambo la hiari, bali ni wajibu wa mkandarasi kuhakikisha wananchi hawapati usumbufu,” amesema Waziri Ulega.
Ameongeza kuwa hakuna sababu ya kuiacha barabara ikiwa imeharibika kiasi cha kushindwa kupitika, akisisitiza kuwa matengenezo ya kawaida yanapaswa kufanyika wakati wote ili wananchi waendelee kupata huduma bora za usafiri.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo amemuelekeza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro kuhakikisha anamrejesha mkandarasi katika barabara ya Kinole – Madamu, yenye urefu wa kilomita 10, kwa ajili ya kufanya matengenezo ya dharura ili kurahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ amesema wananchi wa eneo hilo wana imani na Serikali kuwa itakamilisha ujenzi wa barabara hiyo kwa wakati, hatua itakayoboresha huduma za usafiri na kuchochea maendeleo.
Awali, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Patrick Rambika amesema ujenzi wa barabara ya Bigwa – Kisaki ulianza Septemba 2025 na unatarajiwa kukamilika Desemba 2027.
Amesema mradi huo unatekelezwa na mkandarasi, kampuni ya China Railway 15 Bureau Group Corporation.