Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ulega awageukia mameneja wa Tanroads

Muktasari:

  • Ulega amewataka mameneja kuhakikisha kipindi cha mvua kinachotarajiwa, barabara hazisababishi athari kwa wananchi na kuwazuia kufanya shughuli zao.

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewaagiza mameneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) nchi nzima kuhakikisha hakuna foleni zisizo na sababu, zinazoweza kukwamisha au kupunguza kasi ya shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi.

Ulega ametoa agizo hilo leo Jumapili Novemba 30, 2025  jijini Dar es Salaam alipokagua maendeleo ya upanuzi wa Barabara ya Mbagala Rangi Tatu–Kongowe (kilomita 3.8).

Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameidhinisha Sh54 bilioni kwa ajili ya kutatua kero ya foleni kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

"Wakurugenzi kutoka Tanroads, ninaagiza kwa mameneja wote nchi nzima, nikisikia habari za foleni zinalalamikiwa na wananchi na hakuna suluhu ya muda mfupi na ya muda mrefu, hufai kuwa meneja," amesema Waziri Ulega.

Pia,  amewataka mameneja hao kuhakikisha kipindi cha mvua kinachotarajiwa, barabara hazisababishi athari kwa wananchi na kuwazuia kufanya shughuli zao, akisisitiza hatua za haraka zichukuliwe kutatua changamoto zinazoepukika.

"Mameneja fanyeni kazi, msikae kimazoea na kuona jambo hilo ni la kawaida, kukatika kwa barabara tafsiri yake meneja hukagui barabara yako na kuona hapa kuna udhaifu ambao lolote likitokea pataharibika," amesisitiza Ulega.

Vilevile, Ulega amemuagiza Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani kuhakikisha kuwa, barabara ya zamani ya Morogoro inakarabatiwa haraka iwezekanavyo, ili iwe njia mbadala ya kupunguza changamoto za magari kukwama katika barabara kuu ya Dar es Salaam hadi Chalinze.

Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Lazeck Alinanuswe amesema upanuzi wa barabara hiyo, unatekelezwa na Mkandarasi Stecol Corporation kutoka China na unasimamiwa na Kitengo cha Tecu cha Tanroads kwa miezi 15.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika Novemba 2026,  unahusisha upanuzi wa barabara kutoka njia mbili hadi sita, ujenzi wa daraja la juu (interchange) eneo la Kongowe, ujenzi wa mfumo wa maji ya mvua, njia za watembea kwa miguu kila upande, njia za pembeni kila upande na miundombinu ya usalama barabarani.