Ulimbukeni watajwa vijana vyuoni kuvuta shisha

Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Ziwa, Dezidel Tumbu (aliyesimama/mwenye miwani) akitoa semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) na Chuo cha City College Mwanza kuhusiana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Mafunzo hao yaliyofadhiriwa na Taasisi ya Uelimishaji kwa Umma ya Taifa Digital Forum. Picha na Mgongo Kaitira.

Muktasari:

  • Imeelezwa kutokana na ulimbukeni na teknolojia, vijana wengi wanaanzia kuvuta shisha baadaye wanatumia dawa za kulevya.

Mwanza. Wanafunzi wa elimu ya juu jijini hapa,  wameonywa kuhusu matumizi ya shisha, ikielezwa kuwa huwasababisha kutumia dawa za kulevya.

Kauli hiyo imetolewa na Ofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Ziwa, Dezidel Tumbu.

Tumbu ametoa  tahadhari hiyo jana Februari 24, 2024 wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) na Chuo cha City College Mwanza, akisema baadhi hufuata mkumbo kutokana na ulimbukeni.

Mafunzo hayo yalifadhiliwa na taasisi ya uelimishaji kwa umma ya Taifa Digital Forum.

Tumbu ametahadharisha kwamba, mvuto mmoja wa bidhaa ya shisha ambayo inatengenezwa kwa kutumia tumbaku, moshi wake ni sawa na kuvuta sigara 200 zilizotengenezwa kwa tumbaku kwa wakati mmoja.

Amewataka wanaovuta shisha kuacha kufanya hivyo ili kulinda afya zao.

Amesema DCEA inaendelea na uchunguzi kuwabaini wauzaji na watumiaji wa shisha katika maeneo ya starehe wanaochanganya bidhaa hiyo na dawa za kulevya, zikiwamo bangi, heroin na cocaine.

Kufanya hivyo amesema ni kinyume cha Sheria namba 5 ya mwaka 2015 ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.

“Kutokana na ulimbukeni na teknolojia, vijana wengi wanaanzia kuvuta shisha baadaye wanajikuta wamekuwa waraibu wa dawa za kulevya kwa kuchanganya shisha na bangi, cocaine au heroin. Ndiyo maana tunatoa elimu kwa wasomi hawa tunaamini watatusaidia kuielimisha jamii,” amesema Tumbu.

Amesema katika kipindi cha Januari 2023 hadi Februari 2024, DCEA pekee imewakamata watu zaidi ya 40 kwa tuhuma za kujihusisha na kutengeneza, kutumia, kusafirisha na kuuza dawa za kulevya katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

“Tayari tumeshautambua mtandao mzima wa dawa za kulevya Kanda ya Ziwa. Kilichobakia ni kuanza kuwakamata vinara na tunachowataka ni kuacha mara moja kabla ya kufikiwa,” amesema.

Tumbu amesema kupitia doria na misako iliyofanyika mkoani Mara, kunakosadikiwa kuwa kinara wa ulimaji wa bangi, wamebaini mbinu mpya ya kilimo hicho haramu.

Amesema wakulima hulima mahindi kuzunguka shamba na katikati hupanda bangi.

“Tulichobaini ni kwamba wakulima wengi wa bangi mkoani Mara wanarithishana kulima zao hilo, wanaamini ndilo linaweza kuwafanya wafanikiwe. Tumeanza kufanya misako na kutoa elimu kwa kushirikiana na idara nyingine ikiwemo kuwapelekea zao mbadala la kiuchumi,” amesema.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa Digital Forum, Charles Adson amesema semina hiyo inalenga kuwajengea uwezo wanafunzi zaidi ya 100,000 vyuoni nchi nzima ili watambue madhara ya kutumia dawa za kulevya na shisha.

“Katika taasisi za elimu ya juu vijana hawawezi kujizuia kutokana na kuwa na uhuru kupindukia matokeo yake wanajiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, wakati mwingine kwa mkumbo. Kupitia elimu hii tunaamini tutawanusuru dhidi ya madhara ya dawa za kulevya na shisha,” amesema Adson.

Mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Saut, Nastra Hussein ameshukuru kwa kupatiwa mafunzo hayo akiahidi kufikisha elimu kwa wanafunzi na jamii inayomzunguka kwa kuanzisha klabu maalumu za kupinga matumizi ya dawa za kulevya na shisha.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Benki Kuu jijini Mwanza, yalihusisha maofisa kutoka DCEA, Taifa Digital Forum, na wanafunzi zaidi ya 200 kutoka Saut na City College Mwanza.