Umewahi kupitia haya kwenye mkusanyiko?

Muktasari:

  • Kwa kufanya udhalilishaji unaweza kuwekwa kizuizini na kulipishwa faini.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wamelalamikia vitendo vya udhalilishaji wanavyokumbana navyo kwenye maeneo yenye msongamano wa watu kama vile sokoni.

 Wanaeleza udhalilishaji huo unawanyima uhuru wa kufanya manunuzi, kwani baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiwagusa mwilini ikiwamo kwenye makalio na matiti bila ridhaa yao.

Si hayo tu, wapo wanaowaita majina yenye kudhalilisha au kupiga miluzi na kelele za aina nyingine.

Wakati malalamiko hayo yakitolewa, wapo wenye mitazamo tofauti, wakisema hayo husababishwa na namna mtu alivyojiweka katika mwenendo na mavazi yake.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika Soko la Kariakoo, Magdalena Mzingo amesema mara kadhaa amekuwa akikwazwa hususani anapopita katika mtaa wa Kongo.

“Wengine wanachukulia ule msongamano kama fursa, ukiwa unahangaika kupisha mwenzako anakushika matiti jambo ambalo silifurahii kabisa,” amesema Magdalena.

Amesema hali hiyo imemfanya kuwa mtu wa kuangalia mara mbili kile anachokivaa kabla ya kuingia sokoni Kariakoo.

“Nafikiri ni hulka, unaweza kuvaa vizuri bado mtu akawa analazimisha kukushika hata sehemu haina msongamano au mwingine anajifanya anataka kukushika mkono akuonyeshe bidhaa, basi anauburuza kwenye titi,” amesema.

Si hayo tu, wenye makalio makubwa wamekuwa wakidhalilishwa kwa kuitwa majina yasiyofaa kama vile kontena, chura, zigo na hata kupigiwa kelele za ‘anasepa na kijiji’ jambo linalowanyima uhuru wa kufanya shughuli katika maeneo hayo.

“Unaweza kuwa umekaa unasikia kelele za wamachinga, ukiwa unahangaika ujue ni nini kimetokea unaambiwa ni mtu anapita ndiyo anashangiliwa, sidhani kama ndugu wa wahusika wangekuwa wanaona vitendo hivi wangevifurahia,” amesema.

Hali hiyo imekuwa ikiwanyima uchangamfu baadhi ya kinamama wanaotaka kwenda kufanya manunuzi sokoni hapo, huku wengine wakijiandaa kisaikolojia juu ya kile wanachoweza kukutana nacho.

“Achana na kusongwa na watu, unatembea unajilinda kimya kimya mtu akikugusa uwe na wepesi wa kumtoa mkono au kumkaripia," amesema mama aliyejitambulisha kwa jina moja la Shamira.

Katika soko la Karume na la Kariakoo, baadhi ya wafanyabiashara wamelalamikia vitendo vya baadhi ya wanawake kuvaa nguo zinazowashawishi watu kuwafanyia udhalilishaji.

“Watu hawajali hata ni saa ngapi, anataka kwenda wapi avae nini kulingana na mazingira anayokwenda, akifanyiwa hivi alalamike kweli?” amehoji Mudrick Kajuna, mchuuzi wa viatu katika Mtaa wa Msimbazi.

“Unakuja sokoni ukijua tuko watu wa imani tofauti na wengine wamefunga, ukipita na nguo isiyoeleweka wengine wanaweza kutumia maneno ya kukera kuelezea kile ulichokifanya ukakwazika,” amesema Kajuna akizungumzia uvaaji wa mavazi yasiyo ya staha wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mwanasaikolojia Charles Nduku amesema wakati mwingine kelele zinazopigwa na watu sokoni dhidi ya mwili wa mtu huweza kumfanya ajichukie vile alivyo na akaondokewa ile hali ya kujiamini.

“Maoni yakiwa ya kawaida hayana shida, lakini inapofikia hatua ya kuwa kwa kiasi kikubwa, miluzi kupigwa inamfanya mtu aanze kujikataa, kupoteza kujiamini, kuhisi mwili wake unashida kama watu wanavyomtazama kwa kudhani amekuwa zaidi ya kawaida,” amesema Nduku.

Akizungumzia suala hili, Wakili Dk Khamis Masoud amesema ikiwa watu wanapitia changamoto hizo wana haki ya kushtaki na kulipwa fidia kwa kadri itakavyoonekana.

“Kumekuwa na hii tabia na inawakuta sana wanawake, wakiwamo wenye maumbile makubwa, wanapitia changamoto akipita watu wanakohoa, anavutwa, kushikwa maumbile pasipo ridhaa yake. Hili hufanyika katika vijiwe na sokoni, inafanya mtu akose uhuru wa kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” amesema Wakili Masoud ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa taasisi ya Everlasting Legal Aid Foundation.

Amesema mtu atakayebainika kutenda kosa anaweza kushtakiwa kwa kufanya udhalilishaji, kuwekwa kizuizini na kulipishwa faini kwa namna atakavyooneka ametenda kosa hilo kisheria.

“Shida kubwa ni watu hawajui sheria japokuwa si kizuizi cha sheria kufuata mkondo wake, ila inawezekana,” amesema Dk Masoud.

Kutokana na yanayotokea, imeelezwa kuna haja ya kutoa elimu kwenye maeneo yenye mkusanyiko.