Ummy ataka ukaguzi maduka ya dawa

Waziri wa Afya ,Ummy Mwalimu akifunga kongamano

Muktasari:

  • Kumekuwepo na ongezeko la matumizi holela ya dawa za vijiua sumu mwilini (Antibiotics) hali ambayo inachangia usugu wa vimelea vya magonjwa kwa binaadamu na mifugo.

Arusha. Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wakuu wa mikoa na wilaya, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maduka ya dawa ili kudhibiti uuzwaji holela wa dawa ambazo zinahitaji vyeti vya madaktari.

Kumekuwepo na ongezeko la matumizi holela ya dawa za vijiua sumu mwilini (Antibiotics) hali ambayo inachangia usugu wa vimelea vya magonjwa kwa binaadamu na mifugo.

Akizungumza wakati wa kufunga kongamano la tatu la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa za binadamu na mifugo jijini Arusha leo Novemba 17, 2023, Waziri Ummy amesema ni muhimu kudhibiti matumizi holela ya dawa.

Amesema madaktari wa mikoa na wilaya kwa kushirikiana na madaktari wa mifugo ni lazima wasaidie kudhibiti maduka ya dawa ambayo yanakiuka sheria kwa kuuza dawa bila kuzingatia sheria.

"Afya bora ndio msingi thabiti wa maendeleo ya taifa hivyo ni vema elimu kwa jamii isambazwe kufahamu madhara ya kutumia dawa za antibiotics bila kupewa cheti cha daktari"amesema

Amesema wataalamu wa afya ni lazima wazingatie muongozo wa Taifa wa matibabu kwa kutoa Elimu juu ya madhara ya matumizi yasiyo sahihi ya dawa kwa wagonjwa.

Awali akimkaribisha waziri Ummy, Mganga mkuu wa Serikali Profesa Tumaini Nagu amesema kuwa usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa ni janga la kimataifa lakini ni janga kubwa zaidi katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwemo Tanzania na kusababisha vifo kwa watu.

Amesema kwa sasa usugu wa vimelea vya magonjwa unasababisha vifo vingi mara tatu ya watu wanaofariki kwa ugonjwa wa Malaria.

Profesa Magu amesema katika kongamano hilo wameweka mpango mkakati wa kushirikiana katika tafiti za kupambana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwani imeonekana kuwa ndiyo njia bora zaidi ya kupunguza athari za usugu wa vimelea sugu dhidi ya dawa.

Akiwasilisha mada   juu ya kupambana na usugu wa vimelea Professa Robinson Mdegela amesema wameweka mikakati ya kuongeza uelewa kwa jamii na mabadiliko ya tabia kuhusu matumizi sahihi ya dawa, kuzuia na kupambana na maambukizi na kutumia dawa iliyo sahihi.

Amesema muunganiko kati ya binadamu na wanyama katika chakula na dawa ni mkubwa hivyo jamii inapaswa kuwa makini katika kudhibiti matumizi yasiyo sahihi ya dawa ili kupunguza usugu wa vimelea dhidi ya dawa.

Naye Mkurugenzi wa huduma za mifugo,Profesa Hezron Nonga amesema hivi sasa pia kuna ongezeko pia la matumizi ya dawa za antibiotics kwa mifugo hasa kuku na Ng'ombe na kutaka madaktari kushirikiana kudhibiti.