Umri wa kuishi Mtanzania waongezeka, wanawake wanaongoza

Mukurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa.

Muktasari:

  • Wastani wa umri wa kuishi kwa Watanzania umeongezeka kutoka miaka 44 mwaka 1978 hadi kufiki miaka 65 mwaka 2022, wanawake wakiongoza kuishi miaka mingi zaidi.

Dar es Salaam. Umri wa kuishi sasa umeongezeka, ambapo mwaka 1978 Tanzania ikiwa na watu 17.5 milioni, umri wa kuishi ulikuwa wastani wa miaka 44; hata hivyo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), imeonyesha kuwa, takwimu za 2022 zinaonyesha umri huo kuongeka hadi kufikia miaka 65; huku idadi ya watu ikifikia 61.7 milioni.

Hayo yameelezwa leo na Mukurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa wakati wa uzinduzi utafiti wa afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Malaria.

Dk Albina amesema takwimu zinaonesha kuwa umri wa kuishi kwa Mtanzania umeongezeka huku wanawake wakiishi kwa miaka mingi zaidi ambayo ni 69 dhidi ya miaka 62 ambapo wanaume huishi.

“Hii inajulikana Mungu ametupa upendeleo kidogo wanawake kwa kuwa sisi tunabeba watoto halafu hata kazi tunazofanya ni tofauti na wanaume. Pamoja na hilo hatua hii inatokana na maboresho makubwa yanayofanyika katika sekta ya afya huduma zinatolewa,” amesema Dk Albina.

Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa utafiti huo ni wa saba na ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1971 ukihusisha NBS, Wizara ya Afya na ufadhili wa Marekani.

Amesema lengo la utafiti huo ni kupata viashiria vya afya vya nchi ya Tanzania vitakavyoenda kujibu kwenye lengo la tatu la maendeleo endelevu.

Lengo lingine kuiwezesha nchi ni kujua ni makundi gani hasa ambayo hayajafikiwa na huduma za afya ya uzazi ya mama na mtoto, bila kuwa na utafiti huwezi kujua.

“Utafiti huu umefanywa na watalaam wa ndani, hapo awali damu zilikuwa zinaenda kupimwa Marekani sasa hivi kazi imefanyika katika maabara ya taifa.

“Kati ya nchi 110 duniani Tanzania inafanya utafiti huu, hii inadhihirisha ni kwa namna gani nchi hii inahangaika kutafuta viashiria ambavyo vitaisaidia Serikali na wananchi wake kupanga mipango ya maendeleo,” amesema Dk Albina.