Umuhimu wa baba kwa malezi ya mtoto wa kike
Hivyo kutokana na mitazamo hiyo, imesababisha kuwepo kwa mipaka baina ya baba na watoto wa wakike kwa kile kinachoaminika kwamba baba hatakiwi kujihusisha na jambo lolote la mtoto wa kike.
Kuna baadhi ya wanaume huamini katika mila na tamaduni kuhusiana na mtoto wa kike na hata uamuzi wa maisha yao, inawezekana baba asiweke usawa katika kuwalea watoto wa kike na kiume.
Miaka ya zamani ikitokea mama amefariki dunia na baba akabaki na watoto likitokea jambo lolote litakalohusu masuala ya kike atatafutwa shangazi, bibi au jirani ili kumsaidia binti, hususan katika ukuaji wake.
Lakini kwa sasa imekuwa tofauti kwa baadhi ya watoto, hususan wa mjini, anaweza kuongea na baba yake kila changamoto anayokutana nayo kutokana na urafiki waliojenga.
Kumekuwa na visa vingi ambavyo watoto wanakutana navyo pindi wanapoelekea kwenye ukuaji wao, lakini wanakosa mtu maalumu wa kumueleza.
Kulingana na tafiti mbalimbali za kisaikolojia, zinaonyesha baba ni rafiki wa kwanza wa kiume kwa mtoto wa kike na vivyo hivyo, mama ni rafiki wa kwanza wa kike kwa mtoto wa kiume.
Kutokana na ukweli huo, ni muhimu kwa wazazi kutenga muda wa kutosha kuzungumza na watoto wao sambamba na kushiriki katika mambo yao muhimu na kuwaelimisha masuala mbalimbali ya kijinsia.
Akifafanua hilo, Mwanasaikolojia, Ramadhani Massenga anasema kitu cha kwanza cha kuelewa ni kuwa mtoto wa kike mtu wake wa kwanza kumpenda aliye tofauti na yeye kijinsia ni baba yake.
Anasema zaidi ya hilo, mtoto wa kike anapowekwa karibu na baba yake na akaweza kuzungumza masuala yake binafsi, inamjengea pia tabia na uwezo wa kujadili masuala yake hata na mumewe pindi akiolewa.
“Umri wa kuanzia miaka miwili hadi minne, mtoto wa kike huvutiwa zaidi kushikwa na baba yake pengine hata kuliko mama yake. Kitaalamu tunasema mtoto wa kike katika umri huu huwa anapata hisia fulani za wivu kwa mama yake dhidi ya baba yake," anasema Massenga.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Maadili Centre na mtaalamu wa malezi, Florentine Senya anasema mtoto wa kike kuwa karibu na baba anajengewa uwezo wa kujiamini.
Lakini hali hiyo pia inamfanya awe na upendo na jinsia nyingine ambayo inamtengenezea mazingira ya kuwa mama mwenye upendo kwa familia yake ya baadaye.
“Hii itamfanya kuwa mama bora mwenye kumjali mumewe na familia yake kwa sababu alishaonyeshwa upendo tangu akiwa mdogo kutoka kwa baba na hivyo kuweza kutenda mema kwa kuwa alijengewa upendo mapema,” anasema.
Anasema katika jamii za Kiafrika hususan Tanzania, elimu ya hivyo hakuna na
kutokana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili, baba akionekana kuwa karibu na mtoto wake, hasa katika kipindi anachoelekea balehe, jamii inaweza kumuangalia kwa jicho lingine kwa sababu ni kitu ambacho hakijazoeleka, lakini kuna faida kubwa kwa mzazi wa kiume kuwa karibu na watoto wao wa kike.
“Kwa sasa watoto wengi wanalelewa na mama hivyo madhara mengi yanaonekana kwa jamii kwa kukosekana upendo kutokana na mtoto kulelewa na mama peke yake na hakupata mapenzi ya baba, hivyo anaishi na majeraha ya kukosa upendo wa baba.
“Mzazi anayeishi na binti anatakiwa kumpa nafasi mtoto ya kuonana na baba yake na ikiwezekana kukaa naye kwa kipindi atakachokuwa anamhitaji ili kumjenga kisaikolojia na kumfanya awe mtu wa tofauti,” anasema.
Kwa waliopo ndani ya familia ni fursa kwa wazazi kumfundisha mtoto wa kike kuepuka maovu ambayo hayatomjengea hisia na baba yake na hivyo kuweza kumuepusha na baadhi ya matendo ya kikatili.
Ni muhimu hata kiafya
Mtaalamu wa elimu ya afya ya uzazi wa Hospitali ya Marie Stopes, Dk Mashingo Lerise anasema kuna haja ya wanaume kupata elimu ya afya ya uzazi itakayowasaidia kuzungumza na watoto wao kipindi cha balehe ili wasione kama ni kitu kipya kinachozungumzwa hata kama anaishi na mzazi mmoja.
Anasema kama ilivyo kwa mzazi wa kike, baba analo jukumu la kumnunulia mtoto wake taulo za kike. Hivyo baba anatakiwa kuishi na mtoto wake wa kike katika mfumo utakaowafanya wawe karibu.
"Elimu hii itamsaidia mtoto kujitambua kwa sababu haiwezekani mtoto anapata hedhi yake ya kwanza halafu anakwambia unaanza kupiga kelele au kumshika mkono na kumpeleka kwa watu wengi wakati kulikuwa na uwezekano wa kumsaidia.
"Wasichana wengi wanaoanza hedhi ya kwanza huwa wanaogopa na kuhisi kifo, hivyo kama hajapewa maelekezo atakuwa anachanganyikiwa, hivyo ni muhimu kwa baba akafahamu ili kumlinda mtoto huyo wa kike pindi anapopatwa na hali hiyo," anasema daktari Mashingo.
Wasemavyo wanaume
“Sisi na baba yetu hatukuwa na mahusiano mazuri si kwamba alikuwa anatuadhibu, bali kutokana na muonekano wake, ulitufanya tumuogope kwa sababu hakutaka sisi tuwe karibu naye,” anasimulia Dickson John.
Anasema baada ya kuanza kujitegemea alijikuta anakuwa na tabia kama za baba yake na ndipo alipokuja kubadilisha mtazamo wake kwa kuhisi anawakatili watoto wake kwa kukosa upendo wa baba kama ilivyokuwa yeye na ndugu zake .
John anasema aliamua kubadilika na kuwasogeza karibu mabinti zake kwa kuwataka kuacha kumuita baba na kumuita jina lake la Dickson, japokuwa awali ilikuwa ngumu lakini baadaye walianza kuzoea na hata kuwakataza kumpa salamu ya shikamoo, huku akiwaeleza maana halisi ya neno hilo.
“Mwanzo ilikuwa ngumu kwa watoto kunielewa, lakini baadaye walianza kuzoea na nilipokuwa nakutana na changamoto, nilikuwa namuita binti yangu wa kwanza naongea naye anishauri kitu chochote anachoona kinafaa, lakini hakuelewa nini cha kufanya na hapo ndipo urafiki na mabinti zangu ulikuwa wa moto.
“Kutokana na hilo na wao wakaanza kuniambia changamoto zao na hata binti yangu wa kwanza alipovunja ungo mtu wa kwanza kuniambia ilikuwa ni mimi kwa sababu nilikuwa rafiki yake na niliweza kumsaidia kupitia msimamizi wa shule aliyokuwa nasoma kipindi hicho,” anasema John.
Anasema hiyo ilimpa nguvu zaidi kwa wanawe na amepata mkombozi wa kutatua migogoro inayomtatiza hata alipopata mwanaume, aliweza kumshirikisha baba yake nini cha kufanya ili kuepukana na changamoto ya mahusiano.
Kwa upande wake Edward Mbaga, baba wa watoto wawili wa kike anasema amekuwa rafiki wa watoto wake kutokana na hali ya mabadiliko ya malezi kwenye familia, hivyo anawapa uhuru watoto wake kumueleza kila wanachojisikia.
Anasema kuna wakati watoto wake wamekuwa na maswali mengi, hususan binti yake mkubwa kwa kutaka kufahamu mambo mengi kuhusu mabadiliko ya mwili.
Kutokana na maswali hayo, Mbaga anasema hukaa na binti yake kirafiki na kuanza kumuelezea mabadiliko ya kimwili na pindi atakapokutana nayo asione ni kitu cha ajabu na hii itasaidia kunusurika na vitendo vya kikatili kutoka kwa baadhi ya watu.
"Nilishatengeneza urafiki na watoto wangu muda mrefu na nimewapa uhuru wa kunielezea kitu chochote na mimi ninawapa majibu, maana hii inasaidia kumfanya mtoto kujiamini katika kila jambo lake analofanya," anasema Mbaga.
Naye Simon Mwabungu anasema watoto wake wa kike ni marafiki zake tangu utotoni na kwa kuwa muda mrefu mke wake alikuwa nje ya nchi, alibeba jukumu la malezi ya watoto.
"Nilitoa nafasi kwa mabinti zangu kunieleza kile wanachoona kinafaa tangu walipokuwa wadogo, kwa sasa ni watu wazima na familia zao, inapotokea wamekwazana na waume zao wananipigia simu kunielezea changamoto wanazokutana nazo," anasema Mwabungu.