Umuhimu wa wanafunzi kujifunza elimu ya fedha
Dar es Salaam. Ili kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana wadau wameshauri elimu ya fedha na ujasiriamali itolewe kwa wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.
Kufanya hivyo kumeelezwa kutasaidia kuwajengea msingi wa kujitegemea tangu wanapokuwa wanafunzi.
Hayo yamebainishwa na wadau mbalimbali walioshiriki katika ‘Mshiko Bonanza’ hafla ya kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika kutekeleza mawazo yao ya kibiashara kupitia mradi wa ‘Msiko Club’ unaotekelezwa na taasisi ya kuwawezesha wasichana ya Her Initiative.
Mradi huo ambao ulianza mwaka 2019 unalenga kusaidia wasichana kubaki shule na kupata ujuzi wa elimu ya fedha na uwezeshaji kwa ujumla.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Her Intiative, Lydia Charles amesema ili kuendelea kupambana na changamoto ya ajira hasa kwa wahitimu waliona kuna haja ya kuwainua vijana, hususani wasichana, katika nyanja za elimu, kujiamini, na ujasiriamali.
Lydia amesema lengo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anapata uelewa na ujuzi wa maisha, kuanzia kusimamia fedha, kupanga matumizi, hadi kuanzisha na kuendesha biashara ndogondogo shuleni.
“Ujuzi huo anaoupata utamsaidia hata anapohitimu masomo yake na akakosa ajira bado anaweza kujipatia kipato kwa kujiajiri”anasema.
Anaongeza kuwa kupitia mradi huo wanafunzi wanafundishwa ujuzi wa ujasiriamali, elimu ya fedha na masoko ya bidhaa wanazozizalisha.
Amesema hadi sasa mpango huo umeanza kutekelezwa katika shule kadhaa za kata ikiwemo Shule ya Sekondari Saranga, wanafunzi wanatengeneza sabuni ya kufulia.
Pia shule ya Sekondari King’ongo ambao wamejikita katika kilimo cha mbogamboga huku Shule ya Sekondari Kiluvya, wameanzisha mradi wa kinyozi na Shule ya Sekondari ya Wasichana Dar es Salaam ikijikita kwenye biashara za lishe kwa kuzalisha bidhaa kama pilipili na ubuyu.
“Hadi sasa wanafunzi 591 wamenufaika na mradi huo na fedha zinazopatikana baada ya kuuzwa kwa bidhaa zao imesaidia kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa taulo za kike”amesema.
Kwa upande wake Afisa Tarafa, Agness Kyando akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando amepongeza jitihada hido zilizofanyika huku akisisitiza wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha miradi ya aina hiyo yenye tija kwa vijana inaendelezwa.
Kyando amesema ujuzi huo wanaoupata utawasaidia wanafunzio kujitambua, kutumia ubunifu wao na kutafuta fursa zilizopo katika jamii zao.
“Inawajenga katika msingi wa kujitegemea badala ya kutegemea ajira pekee pale wanapohitimu”amesema.
Hafla hiyo pia iliambatana na utoaji wa wazawadi kwa wanafunzi waliofanya vizuri katika kutekeleza miradi yao ya biashara.
Shule ya Sekondari Saranga iliibuka mshindi wa kwanza na kuzawadiwa tuzo pamoja na fedha zitakazowasaidia kuboresha zaidi biashara yao.