Umwagiliaji yachanja mbuga vijijini, visima vyamwaga maji
Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa.
Dodoma. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeanza utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji vijijini, ambapo tayari imechimba visima 390 katika mikoa 25 nchini.
Kati ya visima hivyo, Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kunufaika na visima 93, ukifuatiwa na mikoa ya Manyara na Tabora ambayo kila mmoja umepata 44 katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumza leo Jumanne, Julai 21, 2026, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa kuchimba jumla ya visima 1,064 nchini.
Mndolwa amesema katika mwaka wa fedha 2026/27, tume hiyo inatarajia kuchimba visima vingine 696 katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza upatikanaji wa maji kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji na kuimarisha uzalishaji wa kilimo.
Ameitaja mikoa mingine ni Geita walikopata visima 42, Singida 32, Njombe 30, Tanga 22, Iringa 20, Morogoro 17, Mara 17, Pwani 10, Arusha 10, Mtwara vinane, Mbeya saba, na mkoa wa Ruvuma wenye visima vitano.
“Tunachimba visima kwenye maeneo ya mashamba ya watu mahali ambapo wanaweza kuungana wakulima angalau 16 na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji hapo tunawapa huduma,” amesema Mndolwa.
Hata hivyo, amesema kwa kuwa uchimbaji wa visima hivyo unalenga kwenye maeneo ya watu, Serikali inakaa nao na kujadiliana ambapo wanalazimika kuandika kwa maandishi kwa kuruhusu maeneo yao kuwa sehemu ya kutolea huduma.
Amefafanua kuwa wameshanunua jumla ya pampu 2,000 kwa ajili ya kuzigawa kwa wakulima ambapo 1,000 zimeshapokelewa katika mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Kigoma, Simiyu na Katavi.
“Pampu hizi zinagawiwa kwa vikundi 769 vya wakulima na kuwanufaisha wakulima 15,022 na jumla ya ekari 13,518.75 zitamwagiliwa kwa kutumia pampu hizi.
Mndolwa amesema, mpango walionao kwa sasa ni kuhakikisha wakulima wanasajiliwa ili wawe kutambulika na kupewa mahitaji kila inapobidi jambo linaloweza kusaidia kwenye makusanyo ya mapato.