Makandarasi miradi ya umwagiliaji watahadharishwa
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Mweli (Kulia) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa.
Muktasari:
- Tume ya Umwagiliaji inachukua asilimia 30 ya bajeti yote ndani ya Wizara ya Kilimo.
Dodoma. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli ameagiza makandarasi kutekeleza kikamilifu miradi waliyokabidhiwa ili iwe na thamani inayotakiwa vinginevyo hakutakuwa na kusameheana.
Mweli ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 18,2026 wakati akizungumza na makandarasi na washauri elekezi wa miradi kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), ambapo ameagiza mahusiano kwa pande hizo mbili yasipitilize kiasi cha kusababisha miradi ikwame.
Makandarasi na wasimamizi wa miradi kwenye Tume ya Umwagiliaji wapo jijini Dodoma kwa siku ya nne wakijadiliana na kuwekeana mikakati ya jinsi watakavyotekeleza kwa haraka na ubora miradi iliyotolewa na tume hiyo.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa, thamani ya fedha katika miradi hiyo lazima ionekane na miradi itekelezwe kwa wakati kwa kila mtu atakayekabidhiwa na kutaka wasimamizi wasiruhusu mambo yaharibikie mikononi mwao.
“Tunataka ukamilishwaji wa miradi kwa wakati na kwa ubora, ninyi ambao mnakwenda kuwa wasimamizi msikubali kujenga mazoea ya kupitiliza na hawa wanaojenga miradi, kumbukeni Serikali imewekeza fedha nyingi kwa ambazo zinapaswa kuonekana ili Watanzania wanufaike,” amesisitiza Mweli.
Ameeleza kuwa Tume ya Umwagiliaji inachukua asilimia 30 ya bajeti yote ndani ya Wizara ya Kilimo kwa hiyo ni fedha nyingi, lakini akaonya baadhi makandarasi hawamalizi miradi kwa wakati na wakati mwingine inakosa ubora unaotakiwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa amesema jumla ya miradi 146 inakwenda kutekelezwa katika kipindi hiki ambapo kipaumbele pia kimeangalia kwa makandarasi wazawa.
Mndolwa amesema muda wote waliokaa jijini Dodoma, makandarasi na washauri elekezi wamefanya mapitio na kuwekeana mikakati ya namna wanavyokwenda kutekeleza miradi hiyo ili iishe kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Lakini, kingine hapa tunapoondoka tumekubaliana kuwekeana mikakati na mikataba ili mtu akifeli tunaagana ama kwa sherehe au kimyakimya na tunaomba tuwe wazalendo kwa nchi yetu ili tuweze kuthamini miradi tuliyokabidhiwa,” amesema Mndolwa.
Amesema katika miradi hiyo, wametenga asilimia kadhaa kwa ajili ya makandarasi wazawa na mingine watapewa wageni ambapo amewataka wahandisi wa mikoa kutoa ushirikiano na kwa kuweka usimamizi usiotiliwa shaka.
Katika taarifa yake amesema miradi mikubwa 28 wameikamilisha na mingine 18 imefikia asilimia 75, 52 ipo kati ya asilimia 0 hadi 50, 48 itaingizwa katika bajeti ijayo wakati miradi 26 iko kwenye kundi la kimkakati.
Mmoja wa washauri elekezi katika miradi hiyo Kepha Masige amesema mikakati waliyopewa ni kuhakikisha miradi kwa wakati kulingana na mikataba.
“Tumeambiwa bila kufanya hivyo kipo kipengele ambacho kinatulazimu kujieleza jambo ambalo hatupo tayari kuona likitokea.”