Una tatizo la figo? Usile vyakula hivi

Muktasari:

  • Watu walio hatua za mwanzo za ugonjwa wa figo wamezuiliwa kula baadhi ya vyakula tofauti na wale ambao tayari wana tatizo hilo.

Watu walio hatua za mwanzo za ugonjwa wa figo wamezuiliwa kula baadhi ya vyakula tofauti na wale ambao tayari wana tatizo hilo.

Wataalamu wanasema vyakula vinavyozuiwa kwa mgonjwa wa figo hutofautiana kulingana na kiwango cha uharibifu wa kiungo hicho.

Akizungumza na Jarida la Afya, Ofisa Lishe Mtafiti kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) Fatma Mwasora anasema endapo mtu atagundulika kuwa na ugonjwa wa figo, mtaalamu wa afya au lishe ndiye atamshauri aina ya vyakula kwa ajili ya kukabiliana na mgonjwa.

Kwa watu wenye ugonjwa wa figo wa hali ya juu, anasema ni muhimu kufuata ushauri wa lishe unaofaa kwani husaidia uchujaji wa uchafu na utokaji wa maji mwilini, lengo ni kupunguza sumu kwenye damu.

“Lishe mara nyingi huwa maalumu kwa wagonjwa wa figo, ili kuongeza utendaji wa figo na kuzuia uharibifu zaidi,” anaeleza.


Mambo ya kuepuka

Mtaalamu huyo wa lishe anasema mgonjwa wa figo anashauriwa kuepukana na matumizi ya vyakula vyenye madini ya sodium ambayo kwa kiwango kikubwa hupatikana kwenye chumvi ya mezani.

Anasema utafiti unaonyesha figo zenye afya nzuri husaidia kudhibiti kiwango cha sodiam mwilini.

Kwa mwenye matatizo ya figo, Fatma anasema sodiam husababisha kuvimba kwa vifundo vya mguu, shinikizo la damu, shida ya kupumua, mkusanyiko wa maji kuzunguka moyo na mapafu, hivyo inashauriwa kutumia chumvi kwa kiasi kidogo kwenye chakula.

Anasema figo zilizoharibika haziwezi kuchuja ziada ya sodiam, hivyo huongeza uwezekano wa kuwepo kwa kiasi kikubwa kwenye damu.

“Epuka chumvi ya kuongeza mezani, matumizi ya vyakula vilivyochanganywa na chumvi nyingi, tumia viungo ulivyoshauriwa na mtaalamu badala ya chumvi,” anaeleza.

Pia Fatma anasema, wagonjwa wa figo wanahitaji kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya vyakula vyenye potasiam, akitolea mfano ndizi, parachichi, tikiti maji, asali, zabibu, mboga za majani, maziwa, viazi vitamu, mbaazi, matango, maboga na uyoga, ili kuepuka kiwango kikubwa cha madini hayo kwenye damu.

Kuhusu madini ya protini mwilini, Fatma anasema watu wenye ugonjwa wa figo wanapaswa kuepuka kwa kiasi kikubwa kwani figo zilizoharibiwa haziwezi kuondoa mabaki ya protini iliyopo kwenye damu.

“Inabidi apunguze kula vyakula vyenye protini nyingi hasa za wanyama ambazo ni nyama, dagaa na bidhaa za maziwa,” anasema.

Baadhi ya tafiti zinaonyesha wagonjwa wa figo waliofikia hatua ya mwisho, figo hushindwa kufanya kazi, hivyo kulazimika kuanza kupatiwa matibabu ya kuchuja na kusafishwa damu.

“Kwenye hatua hii mgonjwa anahitaji mtaalamu wa afya au lishe ili kupata ushauri sahihi wa lishe,”anaeleza.

Fatma anasema ni muhimu kwa mgonjwa kupunguza kiasi cha nishati lishe na protini, kwani kinapozidi mwilini huzipatia figo kazi ya ziada ya kutoa mabaki wakati zenyewe zimeshaathirika.

Kwenye matumizi ya vinywaji na vimiminika Fatma anasema, ni muhimu kupunguzwa matumizi yake, ili kuuepusha maji kujaa mwilini.

“Maji yakizidi mwilini husababisha kushindwa kupumua, shinikizo kubwa la damu, kuvimba mwili na kusababisha ugonjwa wa moyo.

“Hivyo, mgonjwa anashauriwa kunywa maji kulingana na mapendekezo ya daktari. Pia ni muhimu kudhibiti ongezeko la uzito wa mwili ili kugundua mapema kama maji yanazidi mwilini,’’ anasema.


Ukubwa wa tatizo

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kwa kila watu 10, mtu mmoja mfumo wa utendaji kazi wa figo zake hauko vizuri. Hii ni sawa na makadirio ya asilimia 10 kwa wananchi wote kusumbuliwa na tatizo hilo, huku asilimia 2.4 wakipoteza maisha na asilimia 2.7 wakigundulika kwenye hatua za mwisho.

Machi mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya figo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Alfelo Sichwale alisema Watanzania 5,800 hadi 8,500 wanahitaji huduma ya kusafisha damu au kupandikizwa figo.

Alisema Januari 31 mwaka huu, wagonjwa 2,750 sawa na asilimia 32 walipata huduma ya kusafishwa damu, 325 wakipandikizwa kiungo hicho.

Alisema kati ya wagonjwa 93 waliopandikizwa figo hapa nchini, Hospitali ya Taifa Muhimbili ilipandikiza wagonjwa 67 na Benjamin Mkapa ya Dodoma wagonjwa 26.


Chanzo cha ugonjwa


Miongoni mwa mambo yanayotajwa kuchangia tatizo hilo ni unene kupitiliza.

Takwimu za Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (TDHS –MIS) unabainisha, uzito uliokithiri na unene kwa wanawake umeongezeka mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka 25 iliyopita, kutoka asilimia 11 mwaka 1991-1992 hadi asilimia 28 mwaka 2015-2016.Kulingana na takwimu za utafiti huo, mwanamke mwenye miaka 15-49 mmoja kati ya 10 wa Tanzania ni wembamba lakini asilimia 28 wana uzito uliokithiri au uliopitiliza.

Kwa wanawake wa mijini Tanzania, asilimia 42 ni wazito au wanene mara mbili zaidi ya wale wa vijijini.


Wataalamu watoa tahadhari


Daktari wa magonjwa ya ndani na dharura kutoka Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Iringa, Mathew Cosmas anatahadharisha unene uliopitiliza unamuweka mtu kwenye hatari ya kupata sukari, magonjwa ya mfumo wa hewa, shinikizo la juu la damu, hali ambayo ni rahisi kutumbukia kwenye maradhi ya figo.

Mbali na hayo, Dk Cosmas anatahadharisha juu ya matumizi holela ya dawa za kupunguza maumivu, akisema badala ya kupunguza maumivu, huambulia magonjwa ya figo.

“Kuna aina za dawa zimeonekana zinaathiri figo moja kwa moja endapo ikitumika isiyo, baadhi ya hizi dawa ufanyaji kazi wake zinatolewa kupitia figo, hivyo zikiwa nyingi zinasababisha kiungo hicho kushindwa kufanya kazi,” anasema.

Kwa wagonjwa wanaoishi na virusi vya Ukimwi anasema, ili kutumia dawa za kufubaza makali ya ugonjwa huo, lazima kwanza wataalamu wampime utimamu wa figo zake, kwani kuanza dawa hizo bila uchunguzi kama figo haziko sawa uwezekano wa kushindwa kufanya kazi ni mkubwa.

Anasema asilimia 25 ya damu huchujwa kwenye figo na dawa nyingi hutumika kupitia damu, hivyo chochote kinachopita kwenye damu kama ni sumu huenda kuathiri kiungo hicho.


Shinikizo la damu, tezi dume na tiba asili zatajwa


Daktari bingwa wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Rufani kanda ya Mbeya, Octavian Kasanga anasema wagonjwa wengi anaokutana nao wenye matatizo ya figo ni wale wenye shinikizo la damu, matatizo ya tezi dume na wanaotumia tiba mbadala.

Akielezea matumizi ya tiba mbadala, Dk Kasanga anasema kumekuwa na wimbi la watu kukimbilia dawa za asili kutoka China, hivyo kujikuta wakiingia kwenye hatari ya kubeba magonjwa badala ya kuyatibu.

Kwa wagonjwa wa kisukari, Dk Kasanga anasema wapo kwenye hatari ya kupata matatizo ya figo, hivyo anashauri wawe wanafanya uchunguzi wa afya walau mara moja kwa mwaka.

Kuhusu kutokunywa maji, daktari huyo anatahadharisha hatari ya kushambuliwa figo kwani matumizi ya maji ni muhimu.

“Watu wenye magonjwa kama mawe kwenye figo wana hatari hiyo, magonjwa mengine yanayochangia mtu kupata shida kwenye figo ni kuwa na saratani ya kibofu, saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume na magonjwa mengine mengi yanachangia tatizo hilo,” anasema.