Unyanyapaa kikwazo wanawake kutibiwa uraibu dawa za kulevya

Ofisa elimu kwa jamii kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Shaban Miraji, akizungumza kwenye kongamano la vijana lililohusisha pia wanafunzi zaidi ya 500 kutoka shule za sekondari kwa ajili ya kutoa elimu dhidi ya kupinga rushwa na dawa za kulevya

Muktasari:

  • Wanawake wengi wanashindwa kuhudhuria vituo vya kutolea huduma za tiba dhidi ya uraibu wa dawa za kulevya kutokana na unyanyapaa.

Arusha. Imebainika wanawake wengi wanashindwa kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za tiba dhidi ya uraibu wa dawa za kulevya kutokana na kukumbana na unyanyapaa.

Moja ya unyanyapaa huo ni jamii kuwanyooshea vidole na kuwatenga, kutokuwakubali na kuwahukumu baada ya kujitokeza hadharani kukiri na kuhitaji tiba dhidi ya uraibu wa dawa za kulevya.

Hayo yamebainishwa leo Jumapili, Machi 10, 2024 mkoani Arusha kwenye kongamano la vijana la kupinga rushwa na matumizi ya dawa za kulevya kanda ya kaskazini lililoandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kushirikina na Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).

Akizungumza kwenye kongamano hilo, Ofisa Elimu Jamii kutoka DCEA, Shaban Miraji amesema wanawake wengi walioathirika na dawa za kulevya hawataki kuhudhuria kwenye tiba kutokana na kuogopa kunyanyapaliwa.

“Jamii inaamini matumizi ya dawa za kulevya ni mambo ya wanaume, hivyo wakiona mwanamke ameathiriwa nayo wanawanyooshea vidole, wewe ni mama, wewe ni mlezi, kwanini unaingia huko, huoni aibu! Jambo ambalo ni kweli haipaswi kujiingiza huko, lakini kama ameshaathirika basi asaidiwe kuokoka mapema,” amesema Miraji.

Amesema kwa kanda ya kaskazini pekee, kuna zaidi ya waraibu 2,002 waliopo kwenye matibabu, kati yao wanaume ni 1,884 na wanawake ni 118 pekee.

“Hivi karibuni kuna ongezeko kubwa la matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake, lakini kama unavyoona wanaojitokeza ni wachache, hivyo tutoe wito kwa jamii kuwaibua na wasiwanyanyapae, bali wawaelekeze kwenye vituo kupata tiba mapema kabla hawajapata madhara zaidi,” amesema Miraji.

Amesema katika kurahisisha hilo, wamekuwa wakitoa elimu kwa jamii pamoja na kuandaa makongamano mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuachana na biashara na matumizi ya dawa za kulevya sambamba na kuwajulisha madhara yatokanayo, lakini pia adhabu za kisheria.

“Leo tumekutanisha wanafunzi zaidi ya 500 kutoka shule mbalimbali za sekondari za wilaya ya Arumeru na Arusha jiji ambao wanaishi kwenye jamii inayohusika na matendo haya” amesema Miraji.

Amesema lengo ni kuwaokoa wasijiingize kwenye biashara wala matumizi ya dawa za kulevya, lakini pia kuwajulisha madhara na umuhimu wa kutoa taarifa za matukio haya kwa mamlaka husika.

Kwa upande wake, Mkuu wa Takukuru mkoa wa Arusha, Zawadi Ngailo amesema wamebaini kuwepo kwa uhusiano mkubwa kati ya mapambano ya rushwa na dawa za kulevya, ndiyo maana wameamua kuungana ili kuleta mafanikio ya haraka.

Amesema sababu kubwa ya kuunganisha nguvu ni kuokoa jamii hasa vijana dhidi ya madhara ya biashara na matumizi ya dawa hizo yanayofanikishwa na vitendo vya rushwa baina ya watekelezaji na mamlaka yenye dhamana ya kudhibiti.

“Tumeona vita ya dawa za kulevya ina uhusiano mkubwa na rushwa, kwani biashara na usambazaji wake, kumekuwa na matumizi makubwa ya rushwa ili kufanikisha uhalifu huo, hivyo na sisi mamlaka tumeongeza nguvu kwa ajili ya kufanikisha vita kwa haraka,” amesema Ngailo.

Mmoja wa wadau wa kongamano hilo, kutoka kampuni ya Edlink Ltd inayohusika na uuzaji na usambazaji wa vifaa tiba, Edger Japhet amesema wamekuwa wakisaidia vifaa kwa ajili ya tiba na kinga dhidi ya uraibu wa dawa za kulevya kwa ajili ya kusaidia jamii kujua umuhimu wa afya zao.

“Tumekuwa tunasaidia vifaa kwa ajili ya kuwatibu waathirika wa dawa za kulevya ambao wakirudi kwenye jamii wanakuwa mashuhuda wazuri juu ya hali waliyopitia, lakini pia tuna vifaa vya kuwakinga dhidi ya matumizi ya dawa hizo haramu, lengo ni kuijenga jamii safi na salama dhidi ya vilevi hivyo,” amesema Edger.

Mmoja wa waraibu waliopata nafuu baada ya matumizi ya bangi, Shofina Ayubu amesema moja ya changamoto wanayokumbana nayo baada ya kupata nafuu, mbali na unyanyapaa ni mtaji wa kufanya shughuli za kuwaingizia kipato, hivyo kujikuta wakikumbwa na tatizo la msongo wa mawazo.

“Unaweza kupona na kurudi mtaani, lakini kama huna usaidizi au uangalizi wa mtu wa karibu au familia, unaweza kujikuta umeingia kwenye makundi na kupata uraibu mwingine kutokana na msongo wa mawazo wa kipato,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali na wadau kuwepo na mfuko wa kuwasaidia mtaji wowote wa kiuchumi ikiwemo elimu ya ujasiriamali na mtaji wa kufanya shughuli hiyo au biashara, ili kuwa huru na maisha mapya kwenye jamii wanayorudi na kuweza kuhimili misukosuko ya unyanyapaa.