Uongozi wa Hospitali Mawenzi wataja sababu kukosea maiti iliyozikwa Chalinze

Mwili wa Steven Massawe ukiwa umebebwa ukipelekwa makaburini kwa ajili ya Kuzikwa, Kibosho Mkombole Wilaya ya Moshi.

Muktasari:

  • Juni 26 mwaka huu, ulichukuliwa mwili wa Steven Massawe wa Kibisho Mkombole, Wilaya ya Moshi na kwenda kuzikwa Chalinze mkoani Pwani, huku mwili wa Idd Semindu ambaye ni wa Chalinze ukiachwa Mochwari.

Moshi. Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi, umesema mkanganyiko uliotokea wa kuchanganya miili ya marehemu, ulitokana na marehemu Idd Semindu wa Chalinze, kutokuwa na ndugu Moshi, hivyo waliotumwa kuandaa na kuchukua mwili, kushindwa kufanya utambuzi sahihi.

Juni 26 mwaka huu, ulichukuliwa mwili wa Steven Massawe wa Kibisho Mkombole, Wilaya ya Moshi na kwenda kuzikwa Chalinze mkoani Pwani, huku mwili wa Idd Semindu ambaye ni wa Chalinze ukiachwa Mochwari.

Hatua hiyo ilisababisha usumbufu kwa ndugu wa Massawe walipofika kuandaa mwili na kuuchukua kwenda kuzika, jambo ambalo lililazimu uongozi wa hospitali kwa kushirikiana na ndugu, kwenda hadi Chalinze kuufukua mwili ambao ulishazikwa tangu Jumatatu na kuurudisha kuzikwa upya Kibosho.


Akizungumza leo Juni 30, 2023, msemaji wa Hospitali ya Mawenzi, Venna Karia amesema licha ya kwamba marehemu walikuwa wakitofautiana umri, lakini Idd ambaye alikuwa akiishi Kitongoji cha Shabaha Wilaya ya Moshi, hakuwa na ndugu hali iliyosababisha mkanganyiko wakati wa utambuzi.

"Kulitokea mkanganyiko wa kuchanganya miili ya marehemu Juni 26 mwaka huu, ambapo mwili wa Massawe ambao ulitakiwa kwenda kibosho ulikwenda Chalinze na wa Chalinze ukabaki hapa," amesema.

"Uongozi wa Hospitali kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu tulifanyia kazi na kubaini hilo, hivyo tulilazimika kwenda Chalize kuufuata mwili wa Steven Massawe ambao ulirudishwa na kuzikwa Kibosho na tulienda na mwili wa Idd ambao umezikwa Chalinze Mboga."

Akielezea sababu za mkanganyiko huo, Karia amesema ulitokana na marehemu Idd kutokuwa na ndugu na hivyo waliotumwa kuchukua mwili kuchanganya.

"Kuna shida kidogo, marehemu Idd huku Moshi alikokuwa akiishi Shabaha, hana ndugu, hivyo mauti ilipomkuta mwili uliletwa na majirani kuhifadhiwa na hata kuja kuchukua mwili uongozi wa kitongoji uliandika tuu barua ya kutuma watu kuandaa mwili na kuupeleka Chalinze," amesema.

Amesema ili kudhibiti tatizo kama hilo kutokea tena, tayari uongozi wa hospitali umeweka utaratibu kwa miili inayotoka nje ya hospitali, kuwa na ndugu watatu watakaouhifadhi ambao ndio watapaswa kufika siku ya kuuchukua.

"Kutaja jina kwa msimamizi wa mochwari haitoshi, pia kunahitajika kuutazama na kuutambua mwili. Hivyo ili kudhibiti tatizo hili lisijirudie tena. Uongozi wa hospitali tumechukua hatua zaidi za utambuzi hasa kwa maiti zinazotoka nje kwa maana ya miili inayokuja kuhifadhiwa. Unakuta hajafia hapa hospitali, ziwe na watu watatu watakaokuja kuhifadhi na hata wakati wa kuuchukua ili kuongeza umakini katika utambuzi," amesema.

Philipo Kwai, ambaye ni ndugu wa marehemu Massawe, amesema si tukio la kwanza la miili kuchanganywa hospitali na kutaka umakini kuongezwa ili kuepusha usumbufu kama huo.

"Hili si tulio la kwanza, hata hapa Kibosho hili ni la tatu ambapo uliwahi kuchukuliwa mwili wa Kibosho na kwenda kuzikwa Singida, baadaye ilipobainika ukafukuliwa na kurudishwa, tunaomba serikali iliangalie hili na umakini uongeze," amesema.