Upelelezi kesi ya Kaimu Mkurugenzi Taasisi ya Elimu bado haujakamilika

Muktasari:
- Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Desemba 8, 2014 na Mei, 2017, ambapo katika utekelezaji wa majukumu, walienda kinyume na utaratibu na kuwateuwa watu wasio na sifa kufanya marekebisho ya vitabu vya bailojia kidato cha sita na tano, Kemia kidato cha sita, Kiingereza darasa la tatu na kitabu cha Kiingereza kidato cha kwanza hadi nne.
Dar es Salaam. Serikali imesema bado inaendelea na upelelezi katika kesi ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya Sh7 bilioni inayomkabili aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Elia Yohana na mwenzake.
Yohana na mwenzake, Yusuph Kilewa ambaye ni Mkurugenzi wa uandaaji wa Vifaa vya kielimu kutoka taasisi hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 9 likiwemo la kuisababishia Serikali hasara.
Wakili wa Serikali, Frank Michael ameieleza Mahakama hiyo, leo Novemba 8, 2023 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Michael amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalu, kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Swalu baada ya kusikiliza hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22, 2023 itakapotajwa na washtakiwa wapo rumande.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, October 24, 2023 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Desemba 8, 2014 na Mei, 2017 washitakiwa hao katika utekelezaji wa majukumu, walienda kinyume na utaratibu na kuwateuwa watu wasio na sifa kufanya marekebisho ya vitabu vya bailojia kidato cha sita na tano, kemia kidato cha sita, Kiingereza darasa la tatu na kitabu cha Kiingereza kidato cha kwanza hadi nne.
Masomo mengine ni Najifunza kuandika darasa la kwanza, kitabu cha mwanafunzi darasa la kwanza na sita, jiografia kidato cha kwanza, historia kidato cha kwanza hadi sita, kitabu cha Kiingereza kidato cha tano na sita na Literature and Stylistics kidato cha tano na sita.
Alidai kuwa watuhumiwa hao waliwateua kimakosa Arafati Sharifa, Opti Lucas, Qenance Mwasinga, Elius Magusha, Razia Yahaya, Chris Kasalalia, Demitria Hiyera, Wilbert Ijumba na Stomin Msaka, kitendo ambacho ni kinyume na taratibu za mwajiri.
Iliendelea kudaiwa kuwa vitabu vyote hivyo vilifanywa kinyume na waraka wa 4 wa mwaka 2014 uliotolewa na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia sambamba na muongozo wa tathmini ya vitabu wa mwaka 2015 wa taasisi ya elimu Tanzania.
Pia, inadaiwa kwa uzembe uliofanywa na Watuhumiwa hao, wameisababishia Serikali hasara ya Sh7, 065,414,562.