Upinzani waibua upya sakata uuzaji nyumba za Serikali

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika akimpongeza Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Suzan Kimwanga alipomaliza kuwasilisha hotuba ya kambi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka wa fedha 2019/2020. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeibua upya sakata la uuzaji wa nyumba za Serikali na kutaka waliouziwa kinyume cha mikataba wanyang'anywe.

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini  imeitaka Serikali kurejesha nyumba za umma ilizouza kinyume cha mikataba na malengo ya mauzo.

Kauli hiyo imetolewa leo, Alhamisi, Mei 9, 2019 na msemaji wa kambi hiyo kuhusu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Susan Kiwanga wakati akisoma maoni yao kwa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2019/2020.

Amesema Serikali imeshindwa kutekeleza azimio la Bunge la kurejeshwa kwa nyumba hizo na pia wabunge wameshaanza hisia  zao kuhusiana na kurejeshwa kwa nyumba hizo.

"Kambi Rasmi ya Upinzani inarudisha tena ombi kutaka Serikali ya Awamu ya Tano kuzirejesha nyumba za Serikali ambao hawakustahili na zoezi zima lililogubikwa na rushwa na upendeleo mkubwa wa kiundugu na uchafu mwingine wa aina hiyo," amesema.

Amesema kwa kuwa awamu ya tano ni Serikali ya kunyoosha nchi, itakuwa ni vyema ikanyoosha pale ambapo hapakuchukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria.

"Kambi ya Upinzani inaumiza ni lini Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) itachukua nafasi yake katika hili," amehoji Kiwanga.