Urasimu watawala taarifa ya ajali iliyoua 18 Nzega

Tabora. Upatikanaji wa taarifa za ajali ya basi kugongana na lori na kusababisha vifo vya watu 18 umetawaliwa na urasimu baada ya wahusika kurushiana mpira.

Hii ni baada ya jitihada za Mwananchi kupata taarifa za utambuzi wa miili na hali za majeruhi kushindikana kutwa nzima ya leo Jumatatu, Oktoba 23, 2023 ambapo awali Mganga Mkuu wa Wilaya (DMO) wa Nzega, Dk Anna Chaduo aliahidi kutoa taarifa baada ya kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nzega.

"Kutoa taarifa hizo ni lazima nipate idhini kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri,’’ alisema Dk Chiduo

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Mji Nzega, Shomari Mndolwa kwa ajili ya kupata kibali cha kupata taarifa hizo alisema:”tumekubaliana kuwa mtoa taarifa kuhusu ajali hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai.’’

Alipotafutwa, Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai alisema kwa wakati huo alikuwa kwenye kikao na kuelekeza atafutwe Saa 9:30 alasiri na alipotafutwa kwa mujibu wa maelekezo yake, simu ya kiganjani ya kiongozi huyo haikuwa hewani.


Tukio la ajali

Ajali hiyo iliyohusisha basi na lori la mafuta kugongana uso kwa uso ilitokea Oktoba 20, mwaka huu katika eneo la Undomo Wilaya ya Nzega na kusababisha vifo vya watu 18 huku wengine zaidi ya 40 wakijeruhiwa.

Hadi jana Jumapili, Oktoba 22, 2023, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Dk John Magere aliiambia Mwananchi kuwa miili ya marehemu ambao baadhi walishatambuliwa na ndugu bado ilikuwa imehifadhiwa hospitalini hapo kusubiri taratibu za kisheria na kifamilia.

Alisema majeruhi 26, kati yao wakiwemo wanaume 16 walikuwa bado wamelazwa hospitalini hapo kwa matibabu wakati majeruhi wakiwa wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando huku wengine 14 wakihamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Tabora, Nkinga.