18 wafariki ajalini Nzega baada ya basi kugongana na lori

Muktasari:

  • Watu wapatao 18 wamefariki baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori mjini Nzega.
  • Basi lilikuwa likitokea Shinyanga kwenda Dar es Salaam, DC wa Nzega, Naitapwaki Tukai, athibitisha.

Tabora. Watu 18 wafariki baada ya basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori la mafuta eneo la Uchama, kilomita zisizozidi 10 kutoka Nzega mjini.

Akitoa taarifa ya ajali hiyo leo Jumamosi Oktoba 21, 2023, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao amesema ajali hiyo imehusisha basi la Alpha linalofanya safari zake kati Mwanza na Dar es Salaam na kwamba wakati wa ajali, lilikuwa likitokea Mwanza.

"Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Richard Abwao amesema katika 18 waliofariki, 13 ni wanaume na wanne ni wanawake ambapo pia kuna mtoto mmoja wa kiume.

Kuhusu majeruhi, RPC huyo amesema kuwa ni ngumu kusema kwa sasa kwani wanaendelea kuwahessabu kwani kuna ambao wapo Hospitali ya Wilaya Nzega, na kuna wengine wamepelekwa Hospitali ya Nkinga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Naitapwaki Tukai amesema amepata taarifa ya ajali hiyo akiwa wilayani Sikonge katika maadhimisho ya miaka 100 ya Hospitali ya Misheni inayomilikiwa na Kanisa la Moravian, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian.

Kwa mujibu wa DC huyo, basi hilo la Alfa lilikuwa likitokea Mwanza kwenda Dar es salaam, na kwamba taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha ajali ni “uzembe wa dereva wa lori la mafuta,”

Hii ni ajali kubwa kuua idadi kubwa ya watu katika Mkoa wa Tabora kwa mwaka huu.

Endelea kufuatilia tovuti ya Mwananchi na mitandao yake ya kijamii kwa taarifa zaidi.