Sintofahamu vifo, majeruhi ajali ya treni mkoani Tabora

Muktasari:

  • Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likisema watu wanne wamefariki na wengine 132 kujeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea leo eneo la Malolo mkoani Tabora, mkuu wa Mkoa huo amesema waliofariki ni watatu na majeruhi ni 205.


Dar es Salaam. Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likisema watu wanne wamefariki na wengine 132 kujeruhiwa katika ajali ya treni iliyotokea leo eneo la Malolo mkoani Tabora, mkuu wa Mkoa huo amesema waliofariki ni watatu na majeruhi ni 205.

Ajali hii imetokea leo Jumatano Juni 21,2022 ikihusisha treni iliyokuwa ikifanya safari kati ya Kigoma na Dar es Salaam na chanzo chake kikielezwa kuwa ni hujuma iliyofanywa katika miundombinu ya reli.

Baada ya treni hiyo kupata ajali kumekuwa na mkanganyiko wa takwimu za majeruhi na waliofariki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TRC kupitia mkuu wa kitengo cha habari na uhusiano TRC, Jamila Mbarouk,  inaeleza kuwa watu wanne wamefariki na majeruhi 132 walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa ya Kitete- Tabora kwa ajili ya matibabu.

 “Kati ya waliofariki wapo watoto wawili, mmoja wa kike ana umri wa miaka mitano na wa kiume ana  miezi minne na watu wazima wawili, mwanaume na mwanamke,” imeeleza taarifa hiyo.

Muda mchache baadaye mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amesema waliofariki ni watatu na 205 wakijeruhiwa katika ajali hiyo.

Wakati wawili hao wakieleza hayo, Dk Honoratha Rutatinisibwa amesema bado wanaendelea kuhesabu waliofariki na majeruhi wa ajali hiyo huku akigoma kujibu idadi ya waliofariki kama ni wanne au watatu.

Mmoja wa watumishi wa hospitali ya Kitete ambaye hakutana jina lake kutajwa anesema waliofariki ni zaidi ya wanane.

Treni iliyopata ajali iliondoka stesheni ya Kigoma  saa mbili usiku Jumanne Juni 21,  2022 kuelekea Dar es Salaam ikiwa na behewa nane zilizobeba abiria 930.

“Ilipofika eneo la malolo kilomita  10 kutoka stesheni ya Tabora, behewa tano za abiria daraja la tatu, behewa moja la vifurushi, behewa moja la huduma ya chakula na vinywaji na behewa la breki yalianguka na kusababisha ajali,” kwa mujibu wa taarifa ya TRC.

TRC imesema inaendelea  kuwasafirisha manusura wa ajali kutoka Tabora ili kuendelea na safari ya Dar es Salaam.

“Pia TRC inaendelea kufuatilia kwa karibu ili kufahamu m chanzo cha ajali na kuchukua hatua. TRC inatoa pole kwa familia za marehemu na linawaombea majeruhi wmwapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu ya ujenzi wa Taifa," inaeleza taarifa hiyo.

kwa upande wake Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa amesema kuna kipande cha reli kiliondolewa katika eneo hilo na kisha kurudishwa kwa kuegeshwa.

“Mwendo wa treni ulikuwa mdogo ungekuwa ni mkubwa vifo na majeruhi idadi ingekuwa kubwa. Eneo la ajali ni la makazi ya watu na mara zote treni za abiria na mizigo hupita kwa mwendo wa polepole,” amesema Kadogosa.