Ugonjwa ‘fungashada’ wawatesa wakulima migomba, waomba hatua za dharura zifanyike

Afisa Kilimo mkuu wa mamlaka ya afya ya mimea na viuatilifu Tanzania (TPHPA), Hamad Lyimo akionesha mgomba ulioshambuliwa na virusi vya BBTV kwenye moja ya mashamba ya migomba yaliyopo kata ya Kauzeni Manispaa ya Morogoro. Picha Hamida Shariff
Muktasari:
- Umeibuka ugonjwa unaoshambulia zao la migomba kwenye maeneo mbalimbali hapana chini uliopewa jina la 'fungashada' unaosababishwa na kirusi cha kinachojulikana kitaalamu (Banana Bunchy Top Virus( BBTV) kwa kuwa kirusi hicho kimekuwa ni hatari kwa uzalishaji wa ndizi na kuchangia kushuka kwa kipato cha wakulima.
Morogoro. Wakulima wa zao la migomba wameiomba Serikali na wadau wengine kuchukua hatua madhubuti kudhibiti ugonjwa unaoshambulia migomba, unaosababishwa na kirusi kinachojulikana kitaalamu kama Banana Bunchy Top Virus (BBTV).
Wamesema kirusi hicho ni hatari kwa uzalishaji wa ndizi na kimechangia kushuka kwa kipato cha wakulima.
Ofisa Kilimo Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Hamad Lyimo amesema ugonjwa huo unafahamika kwa jina lililozoeleka kwa wakulima kama ‘fungashada.’
Amesema jina hilo linatokana na jinsi majani ya mgomba yanavyojikunja na kufanana na shada la maua, baada ya kushambuliwa.
Lyimo ameyasema hayo leo Ijumaa Julai 4, 2025 alipokuwa akiwasilisha matokeo ya utafiti uliodhaminiwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa wakulima wa migomba, maofisa ugani na waandishi wa habari.
Ameelekeza namna ya kukabiliana na ugonjwa huo ambao tayari umeingia mkoani Morogoro na kuathiri mashamba mengi, hususan katika Kata ya Kauzeni.
Lyimo amesema ugonjwa huo hauna tiba wala chanjo na umesababisha madhara makubwa ya kiuchumi kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa ndizi kwa asilimia 90 hadi 100 katika mashamba yaliyoathirika.
Amesema ugonjwa huo pia husababisha migomba kudumaa na kirusi husambaa kwa kasi kwenye mashamba ya jirani.
“Ndizi ni chakula kikuu na cha asili kwa sehemu kubwa ya wananchi, hasa mikoa ya Kagera, Kilimanjaro na Mbeya. Pia mikoa mingine huzalisha kwa wastani kwa ajili ya kuuza. Kama ugonjwa huu hautadhibitiwa, uzalishaji katika mikoa hii utashuka, tutapoteza chakula na uchumi utadorora,” amesema Lyimo.
Amebainisha kuwa katika mwaka wa 2022/2023, uzalishaji wa ndizi nchini ulikuwa tani 3,577,000, na wakulima wadogo walizalisha tani 2,037,371 na wakubwa tani 1,539,629.
Lyimo amesema ugonjwa huo ulibainika kwa mara ya kwanza Desemba, 2020, katika Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma na ufuatiliaji wa kiuchunguzi Aprili 2021 ulithibitisha dalili zake.
“Dalili zake ni majani kunyauka kutoka pembeni kuja ndani, mistari ya kijani iliyokolea chini ya majani, na udumavu mkali unaosababisha majani kuwa mafupi, membamba na kushikana kiasi cha kuufanya mgomba ufanane na shada la maua,” amesema.
Lyimo amesema virusi hivi husambazwa kwa kupitia miche ya migomba yenye maambukizi inapopelekwa kutoka shamba moja kwenda jingine.
Amesema pia husambazwa kwa njia ya wadudu aina ya vidukari wanaosambaza kirusi hicho kutoka shina moja hadi jingine ndani ya shamba au kati ya mashamba.
Akitaja mikoa iliyoathirika mpaka sasa ni pamoja na Kilimanjaro, Morogoro, Dar es Salaam, Songwe, Mbeya, Dodoma, Katavi, Geita, Kigoma, Mwanza na Pwani.
“Ukiacha mikoa ya Kagera na Mara, mikoa mingine inayozalisha zaidi ndizi imeathirika. Lakini nawahakikishia wananchi kwamba ugonjwa huu hausambazwi na maji ya umwagiliaji, udongo, vifaa vya shambani au tunda lenyewe la ndizi. Ndizi kutoka mgomba ulioathirika haina madhara yoyote kwa mlaji,” ameongeza Lyimo.
Meneja wa Menejimenti ya Maarifa wa COSTECH, Dk Philbert Luhunga amesema jukumu la Tume hiyo ni kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika katika kutunga sera na mipango mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Dk Luhanga amesema COSTECH inao wajibu wa kuishauri serikali kuhusu masuala ya sayansi na teknolojia na kuhakikisha matokeo ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanawafikia walengwa kama watunga sera, wafanya uamuzi, wananchi na wadau wengine.
Amesema wakulima wamefundishwa mbinu za kulinda mashamba yao dhidi ya kirusi hicho na kuhakikisha wanapanda miche safi na salama ili kuzuia maambukizi mapya.
Mtafiti Kiongozi wa zao la migomba kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Mpoki Shimwela amesema matokeo ya utafiti yanaonyesha umuhimu wa wakulima kuhakikisha wanapata mbegu kutoka kwenye vyanzo salama na vilivyothibitishwa.
“Ugonjwa huu ukishambulia shamba, athari zake ni kubwa kwa mkulima binafsi na Taifa kwa ujumla, kwa sababu unapunguza uzalishaji na kuathiri uchumi,” amesema Dk Mpoki.
Amesema kutokana na matokeo hayo, COSTECH imeitisha kongamano kwa ajili ya kutangaza matokeo na kueleza kwa kina athari zake na hatua zinazopaswa kuchukuliwa na wakulima ili kudhibiti maambukizi yasienee zaidi.
Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa ni kudhibiti matumizi ya mbegu zisizo salama, kuepuka kusafirisha miche kutoka eneo moja kwenda lingine, kuhakikisha mbegu zote zinakuwa na uthibitisho wa ubora, kuwa na mkakati wa kung’oa na kuteketeza migomba iliyoathirika kwa kutumia dawa za kuua magugu ili kuivunja na kisha kupanda mipya na salama.
Awali, mkulima wa ndizi kutoka Kata ya Kauzeni, Manispaa ya Morogoro, Godfrey Yamba alisema kabla ya kuingia kwa ugonjwa huo, alikuwa anavuna kati ya mikungu 150 hadi 300 kwa mwaka katika shamba lake la hekari moja.
“Mwaka jana (2024) ugonjwa huu uliingia na umeniathiri sana kiuchumi. Nilikuwa napata wastani wa Sh1 milioni kwa mwaka kutokana na kuuza ndizi, lakini sasa napata takribani Shi200,000 baada ya kuvuna mikungu isiyozidi kumi,” amesema Yamba.
Amesema anaamini chanzo cha maambukizi kilikuwa miche aliyoichukua kutoka kwa wakulima wenzake ambao mashamba yao pia yameathirika.
Ameshauri Serikali, kupitia maofisa kilimo wa kata, kutoa elimu zaidi kwa wakulima kuhusu ugonjwa huo, huku akiwataka wakulima wenzake kutumia mbegu bora na salama zinazozalishwa na taasisi zinazotambulika, zikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua).