Usafiri wa treni SGR Dar hadi Moro wanukia

Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza baada ya  Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutembelea na kukagua thamani za fedha zilivyotumika katika Mradi wa SGR kutoka Stesheni ya Morogoro hadi Dar es Salaam ambapo walisafiri kwa kutumia usafiri wa treni maalum ya wakandarasi. Picha na Lilian Lucas

Muktasari:

  • Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likifikisha asilimia 97.93 ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro na kubakiza maeneo machache yatakayokamilika Aprili.

Morogoro. Wakati Shirika la Reli Tanzania (TRC) likifikisha asilimia 97.93 ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Dar es salaam hadi Morogoro, safari za treni hizo sasa zinanukia.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya TRC kutumia zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya kununua vichwa vya treni, mabehewa ya abiria na mizigo pamoja na vifaa vitakavyotumiwa katika reli hiyo.

Akizungumza leo Machi 21 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) iliyotembelea na kukagua thamani za fedha zilivyotumika katika Mradi wa SGR kutoka stesheni ya Morogoro hadi Dar es Salaam kwa kutumia usafiri wa treni maalum ya wakandarasi, Mkurugenzi mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa amesema wameshaagiza mabehewa 30 ya abiria na vichwa viwili vya treni.

Kadogosa amesema shirika hilo linasimamia ujenzi wa vipande sita vya reli hiyo na kwa kipande cha Morogoro hadi Dar es Salaam ujenzi wake umefikia asilimia 97. 93 na kwa ujumla ujenzi stesheni umekamilika wote ndiyo maana treni inaweza kutoka Morogoro hadi Dar es Salaam.

Kadogosa amesema sehemu chache zilizobakia ni maeneo yenye vivuko vya juu vya kupita magari na watembea kwa miguu kwa kuwa mwendo wa treni hiyo wa kilometa 160 kwa saa hairuhusu mtu wala gari kukatisha.

Ameyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Barabara ya Nyerere, Viguguti na Banana ambayo yote ni katika jiji la Dar es Salaam na ujenzi wake unaweza kukamilika mwishoni mwa Aprili mwaka huu.

Pia ametaja maeneo ya ushoroba wa wanyama tembo eneo la Ngerengere mkoani Morogo.

Eneo lingine amelitaja kuwa reli inayoingia bandarini na kwamba stesheni zote ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 100.

Kadogosa amesema licha ya kununua mabehewa 14 mapya ambayo tayari yameshaletwa, mengine 45 yameagizwa na yanatarajiwa kuwasili nchini Mei Mwaka huu 2023.

"Hivi karibuni mtaona mabehewa yanapita na abiria tunaanza kuwachukua na serikali inatarajia kununua vichwa vipya 17 na malipo yameshatolewa kwa ajili ya utegenezaji na vitaanza kuletwa nchini,” amesema.

Akizungumza baaba ya kukagua reli hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC, Japhet Hasunga ameipongeza Serikali kwa uwekezaji uliofanywa katika Mradi wa ujenzi wa SGR na kwamba mradi huo ni wenye tija na unaochangia kuleta maendeleo katika nchi.

Hasunga alisema Kamati hiyo imejionea mabehewa mapya 14 yaliyonunuliwa ya daraja la kawaida yatakayotumiwa na abiria pale yatakapoanza kazi kuwa ni mapya tofauti na jinsi ambavyo yameonekana kwenye mitandao ya kijamii kwamba ni mabehewa ya zamani.

"Tuliyoyaona mabahewa haya ni mapya kabisa japo rangi ya nje ni rangi ya Shirika letu la Reli ya zamani, ndiyo maana watu wakafikiri pengine ni used (yaliyotumika) haya ni mapya kabisa tumeridhishwa," amesema Hasunga.