Usaili ajira serikalini kufanyika kidijitali

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene

Muktasari:

  • Sekretarieti ya Ajira imezindua mfumo wa usaili kidigitali (AOTS) kupunguza gharama za usafiri.

Dodoma. Sekretarieti ya Ajira imezindua mfumo wa usaili kidigitali (AOTS) utakaomwezesha mwombaji kusailiwa eneo alipo badala ya kusafiri umbali mrefu, ili kupunguza gharama kwa Serikali na kwa wanaosailiwa.

Hayo yamebainishwa jana Machi 23, 2024 jijini Dodoma, kwenye kikao kazi cha kuutambulisha mfumo huo kwa wakuu wa Tehama wa Serikali, sekta binafsi na vyuo vikuu kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Mfumo huo utaanza kutumika rasmi Aprili 6, mwaka huu.

Akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Ajira kuwa waadilifu na waaminifu kwenye mchakato wa kutoa ajira kwa kuwa suala hilo ni nyeti na linagusa usalama wa Taifa.

Simbachawene amesema suala la ajira ni maisha ya watu, hivyo mchakato wake utawaliwe na uwazi na uadilifu ili kuondoa manung'uniko kwa wale ambao wanatafuta ajira serikalini.

Amesema mfumo huo utasaidia kupunguza gharama za wasailiwa ambao walikuwa wanalalamika kusafiri umbali mrefu kwenda kwenye kituo cha usaili kwa kutumia muda mwingi na gharama kubwa, halafu mwisho wa siku wanakosa ajira.

"Unakuta mtu anasafiri kutoka Lindi kuja Dodoma kwa ajili ya usaili, wakati mwingine anafika hata hajui atafikia wapi, nauli yenyewe amekopa halafu anafika anatakiwa akae siku tatu za usaili. Unakuta hata saikolojia yake haiko vizuri, lakini kwa mfumo huu utasaidia kupunguza gharama ambazo mwanzo zilisababisha wengi kushindwa kwenda kwenye vituo vya usaili," amesema Simbachawene.

Waziri amesema pamoja na mlolongo huo, lakini mwisho wa siku mtu anakosa ajira wakati ametumia gharama kubwa kwa ajili ya usaili, hali iliyokuwa inasababisha manung'uniko miongoni mwa wasailiwa.

Amewataka watumishi wa Sekretarieti ya Ajira kutenda haki kwa wote wanaotafuta ajira nchini ili wasiharibu usalama wa Taifa.

Ametoa mfano wa usaili wa nafasi za kazi za Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) na Mamlaka ya Mapato (TRA) ambao ulizua taharuki kubwa nchini kwa kukusanya vijana wengi kwa wakati mmoja na wakati idadi iliyokuwa inatakiwa ilikuwa ndogo.

"Ule usaili ulizua taharuki kubwa kwa sababu TPA ilikuwa inahitaji watu 1,500 lakini waliojitokeza walikuwa ni 14,000 na TRA ilikuwa inahitaji watu 2,100 lakini waliojitokeza walikuwa 36,000. Hii ni hatari kubwa, watu 36,000 kuingia kwa wakati mmoja kwenye mkoa mmoja na wengine walikuwa wanalala stesheni na wengine stendi wakati wanasubiri matokeo ya usaili wao," amesema.

Amesema mfumo huo ukifanya kazi vizuri utaingizwa pia kwenye sekta za elimu na afya ili wanapoajiri watumie mfumo huo wa usaili.

Kaimu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Ajira, Innocent Bomani amesema mfumo huo utawawezesha waombaji kufanya usaili kwenye vituo vilivyotengwa katika mikoa yao badala ya kusafiri kwenda mingine.

Amesema hiyo itapunguza gharama za umbali na nauli ambazo wasailiwa walikuwa wanatumia.

Katibu Msaidizi wa Miundombinu ya Tehama kutoka Sekretarieti ya Ajira, Mtage Ugullum amesema kati ya vituo 154 vilivyotengwa kwa ajili ya usaili nchi nzima, 119 ndiyo vilivyokuwa na sifa vyenye kompyuta 8,375 zilizokuwa na mtandao wa intaneti.

Amesema usaili wa kwanza kutumia mfumo huo utafanyika Aprili 6, 2024 ambao utakuwa kwa ajili ya kuwapata maofisa Tehama.