Usilojua kuhusu vumbi la Kongwa
Eneo mojawapo la Kongwa
Muktasari:
- Kutana na historia ya kimbunga kilichokuwa kinasababisha vumbi kubwa kwa siku nne hadi saba maarufu ‘vumbi la Kongwa’ lililokuwa linaathiri wilaya za Kongwa, Chamwino, Dodoma Mjini, Bahi na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Singida.
Dodoma. Kati ya historia kubwa zilizopo mkoani Dodoma ni pamoja na kimbunga kilichokuwa kinasafirisha vumbi kwa umbali mrefu, maarufu kwa jina la ‘vumbi la Kongwa’.
Vumbi hilo lilikuwa linatokea kwa siku nne hadi saba, Oktoba ya kila mwaka ambapo ni kipindi cha kiangazi mkoani Dodoma.
Vumbi hilo lilikuwa linasababisha madhara mbalimbali, ikiwemo kuezua mapaa ya nyumba, kuangusha miti mikubwa, kuleta madhara ya kiafya kama vile magonjwa ya macho, kifua na mafua kwa wakazi wa maeneo linapopita vumbi hilo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Zubeir White anasema vumbi hilo lilitokana na kukatwa miti kwa ajili ya kilimo cha karanga kwenye wilaya hiyo, hivyo kusababisha jangwa kubwa, ambalo wanyama waliokuwa wanapita kwenye mashamba hayo walisababisha vumbi, hasa wakati wa kiangazi.
White anasema eneo ambalo kimbunga hicho huanzia hasa ni Kijiji cha Sagala, Kata ya Sagala kulikuwa na uharibifu mkubwa wa mazingira kutokana na kukatwa miti yote iliyopo kwenye eneo hilo.
Anasema wakati wa kiangazi, upepo mkali huvuma kuanzia kwenye kijiji hicho na kwa sababu hakuna miti ya kuuzuia, hupata nguvu kadiri unavyotembea na kuzoa vumbi jingi ambalo huwa linasafiri kwa siku nne hadi saba na kuleta tafrani kwa wananchi.
Anasema kijiji hicho kina upepo mkali ambao huwa unavuma mara kwa mara, hali ambayo kama ni mgeni utashindwa kuvumilia mazingira hayo.
“Eneo lingine ambalo huleta vumbi jingi ni la mbugani ambako kulikuwa na makambi ya wapigania uhuru. Sasa kumejengwa Shule ya Sekondari Kongwa, huko nako kuna upepo mkali ambao huwa unazoa vumbi na kulisafirisha umbali mrefu na vumbi lake ni jeupe,” anasema White.
Anasema kutokana na kuwepo kwa mbuga kwenye wilaya hiyo inayoanzia kwenye eneo la ranchi ya Narco Kongwa, inasababisha upepo mkali unaozoa kila kitu inachokutana nacho njiani na madhara huwa yanaonekana pia kwenye wilaya za Chamwino, Dodoma Mjini, Bahi na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Singida.
“Lakini kwetu sisi wenyeji wa Wilaya ya Kongwa vumbi hili huwa ni ishara kuwa kutakuwa na mvua kubwa mwaka huo, hivyo wakulima huwa wanaandaa mashamba yao mapema kwa imani kuwa mvua kubwa itanyesha na watapata mazao mengi,” anasema White na kuongeza:
“Hili vumbi lilikuwa ni vumbi kweli kwa sababu lilikuwa likipita ni lazima tuanze kuulizana nyumba ya nani imeezuliwa kwa sababu lilikuwa linasababisha uharibifu mkubwa kila linapopita.”
Hata hivyo, anasema kwa miaka ya hivi karibuni vimbunga hivyo vimepungua nguvu kutokana na jitihada za Serikali za kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali, ili kudhibiti uharibifu wa mazingira uliofanywa na wakoloni.
Kwa miaka takribani minne, anasema vumbi hilo limepungua nguvu kwa kiasi kikubwa kwa sababu likikutana na miti huwa linapunguza kasi, tofauti na zamani ambapo eneo kubwa lilikuwa jangwa kutokana kukatwa miti kwa ajili ya kilimo cha karanga.
Mwenyekiti huyo anasema vumbi hilo la Kongwa ni maarufu kwa Mkoa wa Dodoma, kwani linapoanzia huwa linachukua rangi nyeupe, linapofika jijini Dodoma huwa lina rangi nyekundu, hali inayosababisha purukushani mjini.
Oktoba mwaka 2019, kimbunga hicho kiliangusha gari la mizigo (semitrailer) kwenye mzunguko wa kituo cha mafuta cha Shabiby, jijini Dodoma na kuezua mapaa ya nyumba kadhaa pamoja na kuangusha miti mikubwa, ukiwamo mbuyu uliokuwepo eneo la Hoteli ya St Gasper.
Magreth Mahinyila (75), mkazi wa Jiji la Dodoma anasema wazee wa Mkoa wa Dodoma hawajapata majibu ya moja kwa moja kuhusu chanzo cha vumbi hilo ambalo hupita kila mwaka kati ya Oktoba 10 hadi 20.
Anasema vumbi hilo linatajwa kuwa lilianza kutokea baada ya Vita ya Pili ya Dunia na chanzo chake kinatajwa kuwa ni uharibifu wa mazingira.
Anasema wenyeji wa Dodoma bado wanaamini kuwa vumbi hilo linapopita huwa ni kiashiria kuwa msimu wa kiangazi unakwisha na wanaingia katika msimu wa masika.
Naye Chedego Masima (70), anasema historia ya vumbi hilo licha ya kutokuwa na ukweli wa kiashiria cha mvua, kwa asilimia fulani ina ukweli, kwani hutokea wakati ambao msimu wa mvua huwa umekaribia.
Masima, ambaye ni mkazi wa Kongwa, anasema chanzo cha vumbi hilo ni uharibifu wa mazingira uliofanywa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Anasema eneo la Kongwa lilianza kuonekana kuwa na umaarufu mkubwa kwa kilimo cha karanga.
“Kilimo cha karanga kinataka ardhi ambayo haina miti wala visiki, hivyo miti ilifyekwa kwa wingi na kung’olewa visiki vyote, ikafanya eneo hilo kuwa jangwa, lakini baada ya vita hali ilikuwa mbaya zaidi, hivyo upepo ukawa mwingi na kuanza kusafiri mwendo mrefu,” anasema Masima.
Anasema anavyofahamu vumbi hilo huanzia maeneo ya milima ya Lubeho ambako ni mpakani mwa wilaya za Gairo (Morogoro) na Kongwa (Dodoma) kupitia mbuga ya Laikala ambako ni maeneo wazi yasiyo na miti.
Masima anasema tangu alipoanza kupata akili ya utu uzima, vumbi hilo alikuwa akiliona kila mwaka mara moja na limekuwa likitokea Oktoba.
“Lakini siri yake moja ni kuwa eneo linakopita huwa ni hapohapo, yaani kama likisogea huwa haizidi kilomita moja, linapita wilaya za Kongwa, Chamwino, Dodoma mjini, Bahi na kisha linaishia vijiji vya wilaya ya Manyoni (Singida) ambako kuna miti mingi inayozuia,” anasimulia Masima.
Anasema kuwa haamini kama vumbi hilo linatokana na uharibifu wa mazingira, badala yake anaona ni mpango wa Mungu unaochangiwa na imani za makabila, hasa kwa Wagogo na Wakaguru.