Usiyoyajua kuhusu maziko ya wazee wa zamani Rombo
Muktasari:
- Mkoani Kilimanjaro, utamaduni wa Warombo enzi za ukoloni ulikuwa wa kipekee, mtu alipofariki dunia hakuzikwa badala yake alikalishwa kwenye majani ya sale katikati ya miti
Rombo. Licha ya historia za kusisimua kuhusu maisha ya jamii mbalimbali enzi za ukoloni, utamaduni wa wakazi wa Rombo mkoani Kilimanjaro ilikuwa kubwa kuliko.
Wakati unastaajabu utaratibu wa Wahindi kutozika wafu, utamaduni wa Warombo enzi za ukoloni utakushangaza.
Kwa mujibu wa wazee mbalimbali wenye asili hiyo, enzi za ukoloni hakukuwa na utaratibu wa kuzika iwapo ungetokea msiba, kila mfu aliegeshwa kwenye mti kama alivyo.
Wazee hao, wanasema ilifanyika hivyo ili kutoa nafasi kwa wanyama wakali kuula mwili huo na kila walipouacha hawakuwahi kukuta hata mfupa.
Hata hivyo, wanasema waliokuwa wanakufa wakati huo ni wazee waliokuwa na umri wa miaka 100 huku vijana na watoto wakifa kwa uchache.
Katika mazungumzo yao na Mwananchi, wazee hao wanasema ilikuwa vigumu kuzika wakati huo kwa sababu watu hawakuwa na elimu.
Akizungumzia namna miili ya watu ilivyokuwa ikitelekezwa kwenye misitu na majani ya 'sale', mmoja wa wazee wa Kijiji cha Lessoroma, Athanas Kikari anasema utaratibu huo ulidumu kwa muda mrefu hadi pale dini zilivyoanza kuingia kipindi cha wamisionari.
"Zamani wakati wa ukoloni watu walikuwa hawazikwi huku kwetu, mtu akifa alikuwa anawekwa kwenye majani ya 'sale' au anapelekwa kwenye miti mingi na anakalishwa yaani ukimkuta utafikiri amekaa, usiku kwasababu kuna fisi wengi wanapita maeneo hayo na hawasahau mizoga hivyo wanakula nyama yote na mkiamka asubuhi hamkuti hata mfupa," anasema Kikari.
Anasema baada ya kuenea kwa dini kwenye maeneo yao, walibadilisha utaratibu kwa kuzika na kuondokana na dhana ya kikoloni.
Kikari anasema watu walianza kuzikwa kwa kuchimbiwa kaburi na wakati huo walizika bila jeneza.
Anasema badala ya kutumia jeneza kuhifadhi mwili na kuuzika walikuwa wakitumia ngozi ya ng'ombe waliyokuwa wakiiviringishia kwenye mwili wa aliyefariki dunia na kisha kumzika nayo.
Kikari anasema baada ya miaka mitano mtu akishafariki dunia hufukua mabaki ya mwili na kwenda kuyahifadhi kwenye eneo maalumu kwa ajili ya mitambiko na mpaka sasa maeneo hayo ya historia yapo.
Anasema baadaye muda ulivyozidi kwenda watu walibadilika na mtu wa familia akifa walitengeneza jeneza lao wenyewe kwa kutumia mbao kisha kuzika mwili.
"Zamani kulikuwa hakuna utaratibu wa kuaga mwili, ilikuwa mtu akifa anachukuliwa hivyo hivyo, anakwenda kukalishwa na njia ilikuwa haipitiki mtu akifa, watu walikuwa waoga kupita eneo hilo lakini zamani waliokuwa wanakufa ni wazee tu," anasema Kikari.
Dementria Joseph, mkazi wa Ubetu anasema jamii ilikuwa inafanya hivyo, kabla dini na hakukuwa na aliyefikiria kuwa mtu akifa anazikwaje.
"Huu utaratibu wa watu kutozikwa na mwili kuachwa kwenye miti na majani ya 'sale' ulidumu kwa muda mrefu lakini kipindi hicho watu walikuwa wanawaza kuzika ni gharama na kurahisisha mambo, lakini dini zilipoingia miaka ya 1890 watu walibadisha utaratibu na kuachana na aina hiyo ya kuzika," anasema Joseph.
Anasema ilifika mahali baada ya dini kuenea maeneo mbalimbali wilayani humo, walibadilisha utaratibu na kuanza kutengeneza majeneza ya miti na kuzika.
Joseph anasema baada ya miaka mitatu walikuwa wakifukua mabaki na kwenda kufanyia mitambiko.
John Mkira (90), mkazi wa Ubetu, wilayani humo anasema miaka ya 1890 kabla ya ujio wa dini wilayani humo, watu walikuwa wakifukua miili ya watu waliokufa na kisha kuiweka kwenye majani ya 'sale' kwa ajili ya matambiko.
"Zamani ilikuwa mtu akifa, baada ya miaka mitatu mabaki yake yanafukuliwa na kuwekwa kwenye majani ya 'sale' na walikuwa wakifanya hivyo kwa sababu kulikuwa hakuna dini na watu walikuwa hawajabatizwa," anasema Mkira.
Anasema baadaye dini ilienea maeneo mbalimbali wilayani humo, watu wakabatizwa na kumjua Mungu na baadhi ya familia ziliachana na zile mila za kikoloni za kufukua mabaki ya miili na kuweka kwenye 'sale' kwa ajili ya mitambiko.