Utafiti kubaini vivutio vya utalii kufanyika mikoa ya Kanda ya Ziwa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Watafiti wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) wanafanya utafiti kubaini na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Mikoa ya Kanda ya ziwa.

Mwanza. Watafiti wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM) wanafanya utafiti kubaini na kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika Mikoa ya Kanda ya ziwa.

Akizungumza katika warsha ya kupanua wigo wa utalii Kanda ya Ziwa iliyoandaliwa na chuo hicho, naibu makamu mkuu wa taaluma UDSM,  Profesa Bonaventure Rutinwa amesema ni  mradi wa utalii endelevu unaofadhiliwa na Serikali ya Sweden.

Amesema utafanyika  Mwanza, Geita na Kagera kwa siku 21 kuanzia leo Ijumaa  Machi 5, 2021 na baadaye Shinyanga, Simiyu na Mara.

“Kuanzia leo watafiti hawa watakuwa na jukumu la kuibua, kubainisha na baadaye kuandaa mpango mahiri wa utalii katika mikoa hii mitatu,” amesema Profesa Rutinwa

Amebainisha kuwa mpango huo utatoa taarifa muhimu zitakazosaidia sekta binafsi na sekta ya umma  kuendeleza, kutangaza na kuuza utalii jumuishi katika mikoa ya kanda hiyo.

Katika uzinduzi naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amesema utafiti huo utasaidia kuendeleza sekta ya utalii na kufanikisha lengo la Serikali kufikisha watalii 2.5 milioni kufikia mwaka 2024/25.

“Ongezeko hilo la watalii litaongeza mchango wa sekta ya utalii katika pato la Taifa kutoka asilimia 17 inayochangia sasa hadi 19.5,” amesisitiza.

Amesema ili kushindana na mataifa mengine duniani yenye vivutio vya kitalii ni lazima nguvu iwekezwe kwenye utafiti ili kuibua fursa mbalimbali pamoja na mikakati ya kusogeza mbele maendeleo ya Utalii nchini.

Mratibu wa mradi huo, Profesa Wineaster Anderson amesema mradi huo pia umefanikisha mitaala ya shahada za awali, umahiri na uzamivu katika eneo la menejimenti ya utalii na ukarimu kutoka UDSM.

Amesema kupanua wigo wa utalii kunahitaji hatua tatu ambazo ni kutambua vivutio na bidhaa za utalii zilizopo, kuendeleza vivutio vilivyotambuliwa, kutangaza na kuviuza vivutio hivyo.

Amesema vivutio vyote vitakavyotambuliwa vitawekwa kwenye ramani ili kuwafikia watu wengi zaidi.