UTAFITI MPYA: Uwekezaji kuzalisha nyama ya funza Tanzania

Friday May 14 2021
tafitipic
By Elias Msuya

Kwa takwimu zilizopo, Tanzania ina mifugo mingi kuliko watu wake lakini ukifuatilia ulaji nyama, utashangaa kwamba wengi hawatumii kitoweo hicho kama inavyoshauriwa.

Tanzania ina ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, kondoo milioni 5.65, kuku zaidi ya milioni 80, nguruwe milioni 1.9 na punda 595,160. Kwa idadi hii, Tanzania inakuwa nchi ya pili Afrika kwa kuwa na ng’ombe wengi ikiwa nyuma ya Ethiopia.

Pamoja na utajiri huo wa rasilimali, Watanzania sio walaji wazuri wa nyama, licha ya uwezo wa Taifa lao kuzalisha tani 701,679 kila mwaka, hivyo kujikuta wakikabiliwa na maradhi yanayotokana na ukosefu wa virutubishi muhimu.

Hii inatokana na ukweli kwamba Watanzania wanakula wastani wa kilo 15 tu za nyama kwa mwaka ilhali Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) linapendekeza kilo 50 kwa kila mtu.

Ulaji mdogo wa kitoweo hicho unaelezwa na wadau kwamba unatokana na bei kubwa ya nyama isiyoendana na kipato cha wengi. “Kilo moja ya nyama ambayo inatosha kwa familia yangu inauzwa zaidi ya Sh6,000.

Nikisema ninunue kila siku nitahitaji Sh180,000 kwa mwezi, hicho ni kiasi kikubwa sana kwangu ndio maana haiwezekani kula mara kwa mara kitoweo hicho, ingawa nafahamu umuhimu wake mwilini,” anasema Shaaban Hamis, mkazi wa Kibaha.

Advertisement

Hamis anasema kutokana na ukweli huo, nyama sio kipaumbele cha watu wengi ndio maana huwa inaliwa zaidi kipindi cha sikukuu.

“Wengi wanakuwa wamejichanga kipindi hicho ndio maana inakuwa rahisi kumudu nyama, vinginevyo watu wanakula kwenye sherehe au msibani,” anasema.

Nyama ni chanzo muhimu cha protini hivyo inahitajika kwenye kila mlo. Ukosefu wa mlo kamili ikiwamo protini husababisha udu mavu na maradhi mengine.

Asilimia 34 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini wamedumaa, licha ya Tanzania kujitosheleza kwa chakula.

Inaelezwa huenda hali ikawa mbaya zaidi miaka ijayo, kwani idadi ya watu inazidi kuongezeka hivyo kuwa na mahitaji ya vyakula tofauti, ikiwamo nyama.

Nyama bandia

Ingawa wengi wamesikia matumizi ya funza kulisha mifugo na samaki, wachache watakuwa wanafahamu kuwa wadudu hao ni chanzo kizuri cha protini kwa binadamu.

Hivi karibuni Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) ulitangaza matokeo ya utafiti wa lishe uliohusisha ubunifu wa kuzalisha nyama kutokana na funza inayoelezwa kuwa na protini nyingi zaidi kuliko inayopatikana kwenye nyama ya kawaida.

Katika utafiti huo, imebainika funza watokanao na nzi wana uwezo wa kuzalisha kitoweo cha kutosha kwa bei nafuu.

Mtafiti wa nyama hiyo, Diana Orembe anasema wamekusudia kutoa nyama ya gharama nafuu kwa wananchi ili kuimarisha lishe katika jamii.

“Tanzania ina upungufu wa tani 500,000 za nyama ambao utaongezeka mara tatu mwaka 2030 endapo hatua madhubuti hazitachukuliwa, hivyo tunatengeneza nyama hii kuziba pengo la upatikanaji. Tunataka tutengeneze nyama ya bei nafuu sokoni,” anasema.

Nyama hiyo itokanayo na funza anasema ina ladha kama ya nyama ya ng’ombe ila faida yake ya ziada ni wingi wa protini.

Yenyewe, anasema ina asilimia 50 zaidi ya iliyopo kwenye nyama ya ng’ombe. “Kwa sasa tumekamilisha utafiti na kinachofuata ni kuingiza bidhaa sokoni, tunaamini mpaka mwisho wa mwaka huu tutaanza uzalishaji,” anasema.

Utafiti wao anasema umegundua kitoweo kinachofanana na nyama iliyosagwa kinachofaa kwa mapishi tofauti.

Hiki kitoweo hakina mfupa ila unaweza kukikaanga au ukapika kwa mchuzi. Kwa sasa, anasema wameshafanya utafiti wa masoko na asilimia 80 ya watu walioonja nyama hiyo wameahidi kufanya nao biashara.

Soko wanaliolikusudia anasema ni Dar es Salaam kwa sababu asilimia 10 ya Watanzania wanaishi katika jiji hili hivyo mahitaji yake ya nyama ni makubwa, kwani takwimu zinaonyesha mtoto mmoja kati ya watano ana utapiamlo.

Akieleza jinsi nyama hiyo inavyotengenezwa, Diana anasema huwatumia nzi ambao hutaga mayai katika eneo maalumu ambako huyakusanya kwa hatua zinazofuata. Mayai hayo huchanganywa na virutubisho vingine vinavyohitajika ili kuyarutubisha. Kufanikisha urutubishaji, anasema wanatumia azola, maharage na magugumaji.

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano WFP, Fizza Moloo anasema utafiti huo ni miongoni mwa mradi inayotekelezwa jijini Dar es Salaam, mji unaokua kwa kasi kubwa duniani.

 “Idadi ya watu jijini Dar es Salaam inatarajiwa kufika milioni 10 ndani ya muongo mmoja ujao. Ukuaji huu unaweza kuleta changamoto ya usalama wa chakula na lishe, jambo linalohitaji ufumbuzi wa ubunifu,” anasema Moloo.

Ubunifu huo, Diana anasema unapaswa kuzingatia usalama yanayoathiriwa pia na idadi kubwa ya mifugo. “Tukisema tuongeze idadi ya mifugo kupata protini kuna changamoto ya mazingira. Kinyesi cha wanyama kinazalisha hewa ya ukaa ambayo ni hatari kwa mazingira, ndiyo maana tunakuja na nyama mbadala ili kuyalinda,” anasema.

Bodi ya Nyama yafunguka

Kwa muda mrefu, jamii tofauti zimekuwa zikila wadudu wa aina tofauti, mfano senene, kumbikumbi na majongoo hivyo utafiti huu, baadhi ya wananchi wanasema utaongeza orodha ya wanaoliwa. “Tatizo ni uzalishaji.

Kuna ugumu kufanya uzalishaji mkubwa, lakini leo hii ukiwa na kumbikumbi kwa mfano, utawauza kwa uhakika. Si unaona tunavyofungashiwa senene kutoka Bukoba,” anasema Agatha Nchimbi.

Bernard Richard, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam anasema wafanyabiashara wa vyakula watatakiwa kuwa wawazi zaidi kwa wateja wao nyama hiyo itakapoingia sokoni.

 “Kwa kuwa ni ya kusagwa, basi watengeneza sambusa, soseji na bidhaa nyingine watatakiwa kueleza hilo ili mteja anunue akijua anakula nyama ya funza, kuku au ng’ombe,” anakumbusha Richard.

Hata hivyo, msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB), Dk Daniel Mushi anasema nyama yoyote inayouzwa nchini inapaswa kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) na kuratibiwa na bodi hiyo.

Kuhusu ulaji mdogo wa nyama nchini, Dk Mushi anasema unasababishwa na mambo mengi ukiwamo utamaduni wa jamii moja mpaka nyingine.

Advertisement