Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utafiti wa viashiria vya Ukimwi waleta matumaini

Muktasari:

  • Utafiti umeonyesha kwa kipindi cha miaka mitano, kiwango cha kufubaza virusi vya Ukimwi kimekua kwa wastani wa asilimia 78 mwaka 2022/2023 kutoka asilimia 52 mwaka 2016/2017 hali inayoleta matumaini mapya ya kutokomeza Virusi Vya Ukimwi (VVU).

Dar/Morogoro. Matumaini yanazidi kuongezeka baada ya utafiti wa viashiria vya ukimwi kubaini kiwango cha kufubaza Virusi Vya Ukimwi (VVU), kinaendelea kukua kwa wastani wa asilimia 78 kutoka asilimia 52 mwaka 2016/2017.

Matokeo hayo yanamaanisha kuwa kiwango cha wanaofubaza VVU kinapokua, ndipo uwezekano wa waliofubaza kuambukiza wengine ukipungua.

Akisoma matokeo ya utafiti huo leo Ijumaa, Desemba Mosi, 2023; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya Sekondari ya Morogoro, mjini Morogoro amesema maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye umri zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua.

“Maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/2017 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/2023. Hii ni sawa upungufu wa asilimia 0.18 ambapo asilimia 0.24 ni wanawake na asilimia 0.11 ni wanaume,” amesema.

Amesema Serikali iliamua kufanya utafiti kwa lengo la kujua hali ya sasa ya VVU na Ukimwi ilivyo nchini na matokeo yameonesha kuwa Tanzania imepata mafanikio makubwa katika mapambano hayo.

Waziri Mkuu amesema taarifa za awali zinaonyesha kuwa watu wanaoishi na VVU wenye umri zaidi ya miaka 15 ni asilimia 4.4, kati ya hao asilimia 4.5 ni wa upande wa Tanzania bara na asilimia 0.4 ni wa upande wa Zanzibar.

Amesema kwa kigezo cha jinsia wanawake ni asilimia 5.6 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 3.0 na kwa kuzingatia kigezo cha makazi, maeneo ya mijini ni asilimia 5 na vijijini ni asilimia 4 huku kijinsia wanawake ni asilimia 5.6 wanaume ni 3.0.

“Kiwango cha kufubaza VVU kimeendelea kukua ambapo kwa sasa ni wastani wa asilimia 78 ambapo kwa upande wa wanawake kiwango kimekua kwa asilimia 80.9 na wanaume asilimia 72.2 ikilinganishwa na asilimia 52 iliyokuwepo kulingana na utafiti wa mwaka 2016/2017,” amesema.

Majaliwa amesema kiashiria hicho ni muhimu kwa sababu mtu anapokuwa amefubaza VVU anakuwa na afya njema na hatasumbuliwa Ukimwi wala magonjwa nyemelezi.

Ameongeza kuwa anapofikia kiwango ambacho virusi havionekani maabarai hataweza kuambukiza kwa wengine.

Akizungumzia takwimu hizo amesema kiwango cha ushamiri wa VVU kwa umri kuanzia miaka 15 na zaidi kwa mikoa ya Tanzania Bara kinaanzia asilimia 1.7 kwa Mkoa wa Kigoma hadi kufikia asilimia 12.7 kwa mikoa ya Njombe, Mbeya na Iringa na kwamba Njombe ina viwango vya ushamiri zaidi ya asilimia 9 sawa na mara mbili ya kiwango cha Taifa.

Majaliwa ametaja vidokezo muhimu vya utafiti huo kuwa ni uwepo wa tofauti ya msingi kwenye ushamiri wa VVU kwa kuzingatia umri, jinsi na mikoa na matokeo kuonyesha ushamiri mkubwa miongoni mwa wanawake.

“Matokeo ya jumla yanaonyesha wanaume wamefubaza kidogo kuliko wanawake na wakati huo huo vijana wamefubaza kwa asilimia kidogo ikilinganishwa na watu wazima,” amesema.

Pia amesema ili kufikia azimio la UNAIDS la kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030, ni vema kuendelea kujikita kwenye upimaji ili kuwabaini wenye maambukizi sambamba na kutoa huduma ya matibabu haraka kwa atakayegundulika.

Katika hatua nyingine amehamasisha uchangiaji wa Mfuko wa Udhamini wa Udhibiti Ukimwi (AIDS Trust Fund – ATF) akisema mpaka sasa umefanikiwa kukusanya Sh4.2 bilioni kiasi alichokitaja kuwa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji halisi.

Pia ametoa maelekezo mengine 10 ikiwemo kuwasihi vijana wajitambue na kuthamini maisha yao kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, akiwataka wadau kuweka kipaumbele katika kundi hilo muhimu ili kulinusuru na athari za Ukimwi.

Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema ili kuimarisha afua za mapambano ya vvu, Wizara inatarajia kuzindua mpango mkakati jumuishi wa kuratibu wahudumu wa afya ngazi ya jamii Januari 2024 watakaoshughulikia magonjwa ya kuambukiwa kwa maana ya kifua kikuu, ukimwi na malaria.

Amesema wanatarajia kutoa mafunzo kwa wahudumu 137,000 watakaopita nyumba kwa nyumba kushughulikia maeneo sita ya vipaumbele ikiwemo ukimwi.

Amesema katika hatua nyingine pia wamebadilisha mpango wa kudhibiti ukimwi: “Tumeanzisha Mpango wa wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP) lengo tushughulikie magonjwa ya ngono na homa ya ini magonjwa yanayokuja kwa kasi hivi sasa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenister Mhagama amesema ipo haja ya kuendelea kuweka nguvu kwa vijana ambao wanaonekana kupata maambukizi kwa wingi.

Mhagama amezitaka familia kuwa na mipango endelevu ya udhibiti ukimwi na hiyo ifanyike pia ngazi ya jamii, mitaa, vitongoji na vijiji huku akitaka maeneo hatarishi kutambuliwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Afya na Ukimwi Stanslaus Nyongo, amepongeza Serikali kwa jitihada kubwa ilizoziwekeza na kufanikisha kupungua kwa maambukizi.

“Tacaids wanafanya kazi kubwa ingawa wana upungufu wa bajeti, lakini tunashukuru wafadhili wamekuwa wakileta fedha nyingi pia kamati tunaipongeza Serikali imekuwa ikitenga fedha nyingi kwa ajili ya mapambano ya ugonjwa wa Ukimwi,” amesema.

Mratibu wa Pepfar nchini Tanzania, Jessica Greene ameiomba Serikali ya Tanzania kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuwasaidia watu wanaoishi na vvu kuendelea kupata huduma bora.

“Tangu mwaka 2003 mambo mengi yamebadilika, kulikuwa na vituo vichache vinavyotoa huduma za VVU lakini kwa sasa vimeongezeka maradufu, wakati Pepfar ikija na hili wazo ilikuwa namna gani ya kufikisha ARV leo tunaona kuna mfumo mzuri wa ugavi na magari ya kutosha kufikisha dawa popote vituo vya afya,” amesema Jessica.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, amesema Morogoro itaendelea kuwa mfano katika mapambano dhidi ya Ukimwi kwa kujikita katika kutoa elimu ili kupunguza maambukizi kwani mkoa huo una mwingiliano mkubwa.

Mwenyekiti wa Baraza la watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Leticia Mourice amesema jamii ina mchango mkubwa wa kuhakikisha Ukimwi unatokomezwa na kwamba bado jamii ipo kwenye hatari kubwa kupata maambukizi kama haitaendelea kuelimishwa.

Mourice amesema kwa sasa suala la unyanyapaa limepungua ikilinganishwa na hapo awali: “Sasa hivi watu wanaoana na kuzaa kwani unapokuwa na maambukizi na ukatumia dawa ipasavyo unafubaza virusi, bado elimu inahitajika.”