Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Utakatifu hufungua mlango wa rehema na maisha mapya katika Kristo

Mchungaji Baricimpande Celestin anapatikana Kanisa la Be Holy, Bujumbura – Burundi.

Muktasari:

  • Neno la Mungu linatufundisha kwamba tunapaswa kuishi maisha yasiyo na lawama mbele zake. Lakini tukimkataa Kristo na kuendelea kuishi katika dhambi, tunajiweka katika hukumu.

Ninawasalimu katika jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.  Ninaitwa Mchungaji Baricimpande Celestin. Ninamshukuru Mungu kwa kutujalia nafasi nyingine ya kukutana kupitia ujumbe huu ulioandaliwa na Kanisa la Be Holy (Uwe Mtakatifu). Popote ulipo, ninakukaribisha tusikie pamoja neno la Mungu litakalotutia moyo, kutushauri na kutuongoza katika maisha ya kila siku. Ninaamini Mungu atafungua mioyo yetu ili tulipokee neno lake na kulifanyia kazi. Amina.

Neno la Mungu linalotuongoza leo linapatikana katika 1 Petro 1:15-16, linalosema: "Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote. Kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni Mtakatifu."

Mungu anatuita kuishi maisha ya utakatifu. Maisha ya utakaso siyo jambo la hiari kwa Mkristo, bali ni mwito ambao kila anayemwamini Yesu Kristo anapaswa kuufuata kila siku. Kuwa mtakatifu kunamaanisha kujitenga na dhambi na kujitoa kwa moyo wote kuishi maisha yanayompendeza Mungu. Ndiyo maana kila mfuasi wa Kristo anatakiwa kuachana na dhambi, kushika amri za Bwana na kufanya mapenzi yake katika kila eneo la maisha.

Tunapoisoma Biblia tunaona kwamba hapo mwanzo Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake. Alifanya hivyo kwa upendo wake mkuu na kwa neema yake. Alituumba ili tumwabudu, tumsifu na kumpendeza katika kila jambo. Mungu alipokusudia maisha ya mwanadamu, alitaka aishi katika ushirika wa karibu naye na afurahie uwepo wake.

Lakini mpango huo ulivurugwa wakati Ibilisi alipowadanganya wazazi wetu wa kwanza wakaasi dhidi ya Mungu. Kwa sababu ya uasi huo dhambi iliingia duniani, na matokeo yake yakawa maumivu, mateso na hatimaye mauti. Tangu wakati huo mwanadamu alijikuta ametengwa na Mungu na akahitaji Mwokozi.

Habari njema ni kwamba Mungu hakumwacha mwanadamu aangamie. Kwa upendo wake alimtoa Yesu Kristo aje kuutafuta ulimwengu uliopotea. Yesu mwenyewe alisema katika Luka 19:10 kwamba, "Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea." Huo ndio msingi wa wokovu wetu. Kristo alikuja ili aturudishe kwa Mungu na kutuwezesha kuishi maisha ya utakaso.

Biblia inasema katika Yohana 1:12 kwamba, "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake." Hii ina maana kwamba kila anayempokea Yesu Kristo kwa imani anasamehewa dhambi zake na anapewa nafasi ya kuanza maisha mapya. Damu ya Yesu hutusafisha na kutufanya kuwa watu wapya mbele za Mungu.

Neno la Mungu linatufundisha kwamba tunapaswa kuishi maisha yasiyo na lawama mbele zake. Lakini tukimkataa Kristo na kuendelea kuishi katika dhambi, tunajiweka katika hukumu. Ndiyo maana Yohana 3:18 inatukumbusha kwamba asiyeamini amekwisha kuhukumiwa.

Pengine unajiuliza, mtu akitenda dhambi afanye nini? Jibu la Biblia ni rahisi na la wazi. Kwanza anatakiwa kukubali kwamba ametenda dhambi. Pili anatakiwa kutubu na kuziungama dhambi zake mbele za Mungu. Tatu anatakiwa kuziacha kabisa na kuanza kutembea katika njia ya utakaso.

Mtume Yohana anatufundisha katika 1 Yohana 1:8-10 kwamba tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe, lakini tukiziungama dhambi zetu Mungu ni mwaminifu na wa haki kutusamehe na kutusafisha na udhalimu wote. Vivyo hivyo, Methali 28:13 inasema, "Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema."

Huo ndio uzuri wa neema ya Mungu. Hata pale tunapokosea, Mungu bado anatupa nafasi ya kurejea kwake. Hatuitwi kubaki katika hukumu, bali tunaalikwa kupokea rehema zake. Tunapotubu kwa moyo wa kweli, Mungu hutusamehe na kuturudishia ushirika naye.

Utakatifu haupaswi kuonekana kanisani pekee, bali katika maisha yetu yote. Unapaswa kuonekana nyumbani, kazini, shuleni, katika biashara zetu na popote tunapokuwa. Maisha yetu ndiyo ushuhuda unaoonyesha kwamba kweli tumempokea Kristo.

Kwa sababu hiyo kila Mkristo anapaswa kujichunguza mara kwa mara. Mtume Paulo anasema katika 2 Wakorintho 13:5, "Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe." Kujichunguza hutusaidia kuona kama bado tunatembea katika njia ya Mungu au tumepotoka.

Ndugu yangu, ikiwa leo unatambua kwamba umemkosea Mungu, usikate tamaa. Njoo kwake kwa moyo wa toba. Mwambie, "Bwana, nisamehe. Nimefanya yaliyo mabaya mbele zako. Nisaidie kuishi katika utakaso. Damu ya Yesu inisafishe na unirudishe katika ushirika wako."

Kumbuka kwamba Mungu bado anakuita leo. Anakuita uache maisha ya dhambi na uingie katika maisha ya utakatifu. Kristo alikufa na kufufuka ili upate msamaha, amani na uzima wa milele. Ukitembea naye kwa uaminifu, utaishi chini ya neema yake na utakuwa ushuhuda wa upendo wake kwa ulimwengu. Mungu akubariki. Amina.