Utata kielelezo waahirisha kesi ya Sabaya

Tuesday November 30 2021
utata pic
By Amina Ngahewa

Arusha. Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Lengai Ole Sabaya na wenzake sita.

Hakimu anayesikiliza kesi hiyo Dk Patricia Kisinda ameahirisha kesi hiyo leo Jumanne Novemba 30, 2021 baada ya malumbano ya kisheria kutokana na kielelezo ambacho kiliwasilishwa na shahidi wa Jamuhuri, Fransis Mrosso.

Kabla ya uamuzi huo, Mawakili wa upande wa utetezi waliomba kupokelewa kielelezo kilichotolewa na Mrosso ambacho kimetofautiana na maelezo aliyoyatoa polisi, huku upande wa Jamuhuri ukikataa kupokewa kielelezo hicho.

SOMA: Shahidi aeleza jinsi alivyojificha msikitini kumwogopa Sabaya (2)

Katika kielelezo hicho, maelezo yaliyotofautiana ni idadi ya vijana waliokuwa na Mrosso alipokwenda kutoa fedha benki ya CRDB tawi la Kwa Mrombo jijini Arusha, umri wa shahidi huyo na namba ya mlipakodi (TIN number)

Katika maelezo hayo, inaonyesha kuwa akiwa kituo cha polisi shahidi amesema ana miaka 47 na mahakamani alisema ana miaka 44, pia tofauti nyingine ni namba ya mlipakodi katika kielelezo cha polisi imepungua namba moja.

Advertisement

Hata hivyo hoja hiyo ya kupokelewa kielelezo hicho chenye mapungufu imepingwa vikali na mawakili wa Jamhuri wakiongozwa na Wakili Mwandamizi, Tarsila Gervas ambapo ameiomba mahakama kutopokea kielelezo hicho kwa kuwa kimekiuka matakwa ya uwasilishaji katika Sheria ya ushahidi.

Wakili Tarsila ameieleza mahakama kwamba kielelezo hicho kilipaswa kifuate utaratibu hata kama shahidi amekubali kitumike mahakamani hivyo hakiwezi kukiuka Sheria na kupokea kielelezo chenye makosa.

Wakili Tarsila aliieleza mahakama kuwa baada ya kupitia kielelezo hicho kilipaswa kisingizwe kwani shahidi alikitambua kielelezo hicho kwa Tin number (namba ya mlipakodi) saini pamoja na majina.

Baada ya malumbano hayo ya kisheria, Hakimu Dk Patricia Kisinda ameiahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano Desemba Mosi, 2021.

Advertisement