Shahidi aeleza jinsi alivyojificha msikitini kumwogopa Sabaya (2)

Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya

Muktasari:

  • Julai 19, 2020, siku ambayo kesi ya unyang’anyi iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ilipoanza kusikilizwa mfululizo, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Mohamed Saad, alitoa madai yaliyoshtua na kuwasikitisha wengi waliofika mahakamani.


Arusha. Julai 19, 2020, siku ambayo kesi ya unyang’anyi iliyokuwa inamkabili aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ilipoanza kusikilizwa mfululizo, shahidi wa kwanza wa Jamhuri, Mohamed Saad, alitoa madai yaliyoshtua na kuwasikitisha wengi waliofika mahakamani.

Saad ambaye ni mmiliki wa duka la vifaa vya nyumbani aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi, Arusha jinsi alivyokimbia na kujificha msikitini baada ya Sabaya na wenzake kuingia dukani kwake mbako hakuwepo muda huo, na kumpa dakika tano afike.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, shahidi huyo alidai aliamua kukimbilia Msikiti wa Kijenge kwa hofu baada ya kupigiwa simu na ndugu yake, ally Saad, kuwa Sabaya yupo dukani kwake na amekuwa akiwasumbua wafanyabiashara.

Aliendelea kueleza kuwa Februari 9, mwaka huu, Sabaya na wenzake walivamia dukani kwake na kuchukua Sh2.7 milioni baada ya kujitambulisha kuwa ni maofisa wa Serikali na kuanza kumsaka yeye.

Aliieleza mahakama kuwa wakati anazungumza na ndugu yake aliyekuwa dukani, Sabaya alichukua simu yake na kumtaka ndani ya dakika tano afike dukani.

Alisema alilazimika kukimbia na kujificha kwenye Msikiti wa Kijenge kuanzia saa 12 jioni hadi saa mbili usiku na baadaye alikwenda kulala kwa rafiki yake eneo la Esso Makaburini.

Shahidi huyo aliieleza mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo, kuwa baada ya kufanya upekuzi dukani kwake na kuchukua mashine ya EFD, Sabaya na kundi lake walikwenda nyumbani kwake na kufanya upekuzi mwingine.

“Nilipigiwa simu na mke wangu kuwa Sabaya na wenzake walivunja nyumba wakiwa na bastola na kuingia ndani wakinitafuta na wamesema hawatalala hadi wanipate,” alidai shahidi huyo.

Kutokana na kujawa hofu, Saad alidai aliamua kukimbilia Wilaya ya Simanjiro kujificha na baadaye alirudi Arusha Februari 17, mwaka huu na kuichukua familia yake na kuipeleka Nairobi, Kenya ambako alikuwa akiishi hadi siku alipokuwa akitoa ushahidi.

Baada ya kutoa ushahidi wake, ilifuata zamu ya mawakili utetezi kumhoji. Moja ya mambo aliyoeleza wakati akihojiwa ni kuwa aliogopa kutoa taarifa ya tukio hilo kituo chochote cha polisi kwa sababu ya hofu.

Aangalia chini muda wote

Wakati akitoa ushahidi huo, Saad alionekana kuangalia chini muda wote. Alipohojiwa kwa nini alifanya hivyo, shahidi huyo alisema kwa mujibu wa dini yao hapaswi kuangalia mtu usoni.

Baada ya Saad kutoa ushahidi, ilifuata zamu ya shahidi wa pili wa Jamhuri, Numan Jasin (17), ambaye ni msaidizi wa Saad (mjomba wake) kutoa ushahidi.

Kijana huyo aliieleza mahakama kwa kirefu jinsi Sabaya alivyoongoza kundi la watu tisa kuvamia duka lao.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka, Jasin alidai kuwa kabla ya makundi mawili ya watu kuingia dukani humo alitangulia mwanamke ambaye alinunua kapeti dogo la mlangoni la Sh10,000 na baada ya muda mfupi kundi la watu sita waliojitambulisha kuwa ni wateja wa jumla wa mapazia wakaingia.

Alisema watu hao walimwamuru mara kadhaa ampigie simu mmiliki wa duka hilo kwa kuwa wao ni wateja wa jumla wa mapazia na alipodai mmiliki yuko mbali, waliendelea kumwamuru ampigie simu aje dukani.

“Baada ya muda mfupi kundi la pili la watu wanne wakiwemo wanaume watatu na mwanamke tuliyemuuzia kapeti muda mfupi uliopita, wakaingia. Wakarudishia mageti ya duka, mmoja akaniamuru nimpigie mwenye duka nimwambie maofisa wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wapo dukani kwake,” alidai.

Alidai siku moja kabla ya tukio hilo, mwanamke aliyekuja na kundi hilo alifika tena Februari 9, dukani hapo na kundi hilo la watu na kuchagua zulia la Sh200,000. Alidai ulipofika wakati wa malipo alitaka kulipa kwa Dola za Marekani 100 lakini alimkatalia.

Shahidi huyo aliendelea kuieleza mahakama kuwa mmoja wa ‘mabaunsa’ wa Sabaya aliyekuwepo mahakamani alivua mkanda wa suruali kisha kumtuhumu mwanamke huyo kuwa kuna dola za Marekani 70,000 zimeibwa Moshi na kuwa mwanamke huyo ameshirikiana na mwenye duka kuiba fedha hizo.

Kesi yashindwa kuendelea

Julai 20, mwaka huu Shauri hilo lilipangwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi lakini mahakama ililazimika kuahirisha baada ya kuelezwa na Wakili Kweka kuwa shahidi huyo alikuwa kwenye sala ya Eid al hajj.

Atumia kiarabu

Julai 22, Shahidi aeleza mahakama namna Sabaya aliongoza mabaunsa kuvamia na kuiba

Baada ya kesi hiyo kuahirishwa Julai 20, Jasin aliendelea kutoa ushahidi wake tarehe 22 Julai. Siku hiyo aliieleza mahakama jinsi Sabaya alivyoongoza ‘mabaunsa’ kuvamia na kuiba nyaraka dukani kwao ikiwemo mashine ya kielektroniki (EFD) na Sh2.7 milioni za mauzo.

Aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa hao walitumia muda wa saa tatu kuwapekua na kuwapiga kabla ya kuwapeleka Kituo cha Polisi, Arusha.

Jasin aliieleza mahakama kuwa alilazimika kutumia lugha ya Kiarabu kuongea na mama yake na kumwambia asifungue mlango wa nyumbani kwao baada ya kutakiwa kufanya hivyo na mmoja wa ‘mabaunsa’ waliotaka kuingia nyumbani kwao wakiwa na Sabaya.

Shahidi alidai kuwa alipokuja Diwani wa Kata ya Sombetini, Bakari Msangi, Sabaya aliamuru apigwe. “Alipigwa kipigo kizito hadi akaishiwa nguvu huku akilia na kuomba msamaha kwa Sabaya,” alidai shahidi huyo na kuongeza kuwa alimwona Sabaya akitoa silaha na kumtisha Msangi.

Shahidi alidai baada ya Msangi kuishiwa nguvu na kulala chini, kiongozi (Sabaya) aliamuru akalishwe na kutoa silaha aina ya bastola akamnyooshea Msangi na kumwambia ana kiherehere na amekuwa akifuatilia mambo yake.

Jasin aliieleza mahakama kuwa Msangi alifungwa pingu baada ya kuwekwa chini ya ulinzi kwa amri ya Sabaya. Alidai baada ya muda aliamriwa kumpigia muuzaji wa duka hilo aliyemtaja kwa jina moja la Abuumansoor ambaye kwa siku hiyo hakuwepo kazini baada ya kudai hajisikii vizuri.

Alieleza muuzaji huyo alipofika dukani alianza kuhojiwa iwapo anamfahamu dada huyo aliyemhudumia jana yake. “Akajibu kuwa alienda kumsaidia kubadili dola zake kwenye duka la kubadili fedha za kigeni,” alisema.

Alidai kiongozi huyo aliyekuwa akiitwa General (Sabaya) aliamuru Mansoor awekwe chini ya ulinzi na kupekuliwa na kupigwa na mabaunsa wa Sabaya baada ya kuamrishwa kufanya hivyo, baadaye baadhi ya watu waliokuwa dukani waliachiwa huru.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa kabla hawajaambiwa wafunge duka lilipekuliwa eneo la kaunta na kuchukuliwa fedha hizo Sh2.76 milioni, kisha kuanza safari kuelekea nyumbani kwao Mtaa wa Soko Kuu hadi Bondeni.

Jasin alieleza kuwa baada ya kuonyesha geti la nyumbani kwao alipewa simu yake na kutakiwa kumpigia mama yake ili afungue mlango. “Niliongea na mama yangu kwa lugha ya Kiarabu kuwa asifungue mlango huo,” alisema na kudai kuwa baada ya hapo waliondoka na kuelekea kituo cha polisi.

Alisema walipofika kituo cha polisi wakaambiwa washuke na kiongozi huyo akawa anaongea na askari kwa muda kidogo. Alidai waliingizwa kwenye ofisi na kuhojiwa kisha wakaachiwa kwa dhamana na kukabidhiwa simu zao ambapo askari huyo aliwapa lifti hadi nyumbani kwao.