Rufani ya Sabaya yapokewa Mahakama Kuu

Muktasari:

  • Ikiwa zimepita siku 22 tangu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imepokea rufaa yao.


Arusha. Ikiwa zimepita siku 22 tangu aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya na wenzake wawili kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja, Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha imepokea rufaa yao.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, Wakili wa utetezi Mosses Mahuna amesema rufaa hiyo imepokelewa na kupewa namba 129 ya mwaka 2021.

Amesema rufaa hiyo iliyowasilishwa wiki hii na kupokelewa na kwamba wana hoja zaidi ya 10 za kukata rufaa hiyo. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzielezea kwa undani.

"Rufaa ambayo tumekata ni ya kesi namba 105 ya 2021 na imefunguliwa wiki hii na kupewa namba 129 na sasa tunaendelea kusubiri taratibu nyingine," amesema Mahuna.

Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwemo la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kesi hiyo ya jinai ya unyang'anyi wa kutumia silaha namba 105 ya 2021, ilisikizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Odira Amworo.

Oktoba 18,2021 mawakili waliokuwa wakiwatetea washitakiwa hao waliwasilisha notisi ya nia ya kukata rufaa.

Washitakiwa hao walikuwa wakitetewa na jopo na mawakili sita wakiongozwa na Duncan Oola, Mosses Mahuna, Edmund Ngemela, Sylvester Kahunduka, Fridolin Bwemelo na Jeston Jastin.

Katika shauri hilo upande wa Jamhuri ulikuwa ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka na Mawakili wa Serikali Waandamizi Abdallah Chavula, Felix Kwetukia na Wakili wa Serikali  Baraka Mgaya.

Katika shauri hilo upande wa Jamhuri uliwasilisha vielelezo nane na mashahidi 11.