Shahidi aomba kupumzika kwa dakika tano kesi kina Sabaya

Muktasari:

  • Jopo la mawakili sita wanaomwakilisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita katika kesi ya uhujumu uchumi, wamemhoji shahidi wa saba katika kesi hiyo, Geofrey Nnko, hadi akaomba kupumzika kwa muda wa dakika tano.

Arusha. Jopo la mawakili sita wanaomwakilisha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na wenzake sita katika kesi ya uhujumu uchumi, wamemhoji shahidi wa saba katika kesi hiyo, Geofrey Nnko, hadi akaomba kupumzika kwa muda wa dakika tano.

Nnko, ambaye ni Ofisa wa Tehama wa Benki ya CRDB Kanda ya Kaskazini, jana aliomba kuketi wakati akihojiwa na mawakili hao na kuomba kupumzika kwa dakika tano kabla ya kuendelea kuhojiwa baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake wa msingi.

Mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, shahidi huyo alikuwa akiendelea kutoa ushahidi wake baada ya mahakama hiyo kupokea ruhusa ya maandishi kutoka kwa Sabaya kutaka mawakili wake waendelea na shauri hilo bila yeye kuwepo kwa kuwa anaumwa.

Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Sylvester Kahunduka kuhusiana na video za CCTV alizotoa na kumpatia shahidi wa nane katika kesi hiyo, aliieleza Mahakama kuwa hakuwa anapeleleza shauri lolote wakati anazitoa.

Pia, alidai alidai mahakamani hapo kuwa hakuwa na maombi yoyote kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ya kuelekezwa kuhusu channel inayohitajika.

Bali alitoa channel namba 1, 12 na 13 baada ya ofisa uchunguzi kutoka maabara ya kiuchunguzi Takukuru, Johnson Kisaka kuchagua clip hizo.

Shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa binafsi hakupokea barua bali alipokea maelekezo kutoka kwa kiongozi wakje wa kazi afike kwenye tawi hilo na hakuwa ameweka alama ya kipekee kwenye flash hiyo.

Sehemu ya mahojiano hayo ilikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Hebu iambie mahakama 31/5/2021 hii flash uliyoitambua kuna alama ya pekee uliyoweka ili uweze kuitambua?

Shahidi: Hapana sina zaidi ya maelezo.

Wakili: Si unafahamu flash zinakuwa na serial namba.

Shahidi:Ndiyo

Wakili: Wewe kama mtaalamu wa IT uliweza kuzinakili hizo serial namba?

Shahidi: Sina zaidi ya nilichoeleza hapa mahakamani.

Mheshimiwa naomba kukaa (alikuwa amesimama), naomba dakika tano.

Shahidi aliruhusiwa kukaa na baada ya muda kidogo Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga, aliieleza mahakama kuwa shahidi anaomba kwenda chooni kabla hajaendelea na aliporejea aliieleza mahakama kuwa yuko sawa kuendelea kuhojiwa.

Awali, akihojiwa na Wakili wa utetezi Mosses Mahuna, shahidi huyo aliieleza mahakama kuwa hawezi kuzungumzia ripoti iliyopo ndani ya flash kwa sababu anazitambua clip sita alizozitoa na kuhusu ripoti anaifahamu Kisaka na ndiye anaweza kuielezea.


Sabaya akata rufaa

Wakati huohuo, akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama, Wakili Mahuna alisema Mahakama Kuu imepokea rufaa yao yenye hoja 10 ya kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha ya Sabaya na wenzake.

Sabaya na wenzake wawili Sylvester Nyegu na Daniel Mbura walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, Oktoba 15, mwaka huu kwa kutiwa hatiani kwa makosa matatu likiwamo la unyang’anyi wa kutumia silaha.