Utata Polisi wakidaiwa kuua muuza mkaa Kibaha

Mke wa marehemu, anayetaka Serikali imsaidie matunzo ya watoto, baada ya mumewe, Franky Kessy kufariki akidaiwa kupigwa risasi na polisi.

Muktasari:

  • Kifo cha muuza mkaa aliyetajwa kwa jina la Franky Kessy, kimegubikwa utata baada ya ndugu kudai kuwa ndugu yao aliuawa kwa risasi baada ya kutokea mapambano kati ya Polisi na wauza mkaa wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Kibaha. Wakati kifo cha mfanyabiashara wa mkaa, Franky Kessy kikizua utata, ndugu wa marehemu na mkewe wameiangukia Serikali juu ya matunzo ya watoto.

Kessi aliyekuwa mkazi wa Mailimoja Kibaha mkoani Pwani alifariki Machi 9, 2024 ikidaiwa kuwa alipigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa askari polisi waliokuwa doria eneo la Kibaha.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amesema mwili wa marehemu Kessy uliokotwa na wananchi jirani na eneo la tukio wilayani Kibaha.

"Kijana mmoja aliyetambulika kwa jina la Franky Bonifacy Kessy (33 alikutwa na wananchi akiwa amefariki dunia katika eneo hilo la tukio uchunguzi wa kifo hicho unaendelea kwa kushirikisha wataalamu mbalimbali," amesema Kamanda Lutumo katika taarifa yake kwa vyombo vya habari aliyoitoa jana Machi 10, 2024.

Hata hivyo, Kamanda Lutumo amesema kulikuwa na mapambano kati ya askari wa jeshi hilo na watu wanaodaiwa kuwa wavunaji haramu wa mazao ya misitu.

Amesema askari hao walikutana na kundi la wabeba mkaa waliokuwa na pikipiki na waliwasimamisha na kwamba walikaidi na kuanza kuwashambulia askari kwa mapanga na visu.

"Askari walijibu kwa kufyatua mabomu hewani na risasi hewani lakini wafanyabaiashara hao walikaidi na kuendelea kupambana na askari hali iliyosababisha  askari mmoja kujeruhiwa,” amesema.

Ndugu waeleza

Akizungumza na Mwananchi jana Machi 10, 2024 kaka wa marehemu, Isaya Shoki amesema kuwa kuna kila dalili kuwa ndugu yao aliuawa  kwavkuwa waliukuta mwili wake ukiwa na majeraha yenye alama ya risasi na umelazwa kwenye magunia ya mkaa na pembezoni ukiwa umewekewa panga.

"Nilifika siku hiyo na kukuta mwili wa ndugu yetu ukiwa umelazwa kwenye magunia ya mkaa,  lakini kuna alama zinazoashiria kutobolewa na risasi, tukauchukua tukaupeleka Hospitali ya Mlandizi na baadaye Tumbi,” amesema.

Amesema kuwa kitendo hicho kimewapa wakati mgumu ikizingatiwa marehemu ameacha mjane na watoto kadhaa,  ambao bado wanahitaji kusoma pamoja na mahitaji mengine muhimu.

"Tunaiomba Serikali iangalie familia watoto wasome kwa sasa hawana tegemeo baba yao ameshafariki katika mazingira hayo," amesema.

Mjane wa marehemu,  Ester Endrew amesema kuwa mara ya mwisho  mumewe aliondoka Machi 9, 2024 akimuaga kuwa anakwenda kwenye majukumu yake ya biashara ya mkaa na alishitushwa kusikia taarifa ya kifo chake.

Amesema kuwa mumewe amekuwa akifanya biashara hiyo kwa miaka mingi, huku akifuata taratibu za Serikali kama zinavyoagiza hivyo alishangaa kusikia kufikwa na mauti kwenye tukio hilo.

"Naiomba Serikali iniangalie hasa kwa watoto wangu ikiwezekana iwasomeshe ili kuandaa maisha yao ya baadaye, maana msaada mkubwa ulikuwa baba yao na baba yao amefariki mimi peke yangu sitaweza," amesema.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kilimahewa, Benedict Nyasi amesema kuwa marehemu enzi za uhai wake,  alikuwa ni mmoja wa vijana waliokuwa wakitumia muda wao vizuri wa utafutaji mali hivyo amepoteza moja ya nguvu kazi.

Amesema kuwa ni vema mamlaka zinazohusika zikaweka utaratibu rafiki kati ya wafanyabaiashara wa mkaa na wasimamizi wa sheria,  ili kuondoa hali ya sintofahamu inayosababisha matukio kama hayo ya kupoteza nguvu kazi.

Mmoja wa wafanyaabaishara wa mkaa amesema kuwa hivi sasa wanafanya kazi hiyo katika mazingira magumu na hii inatokana na mamlaka zinazohusika kubadili utaratibu mara kwa mara tena kwa kushitukiza.