KESI YA POLISI WANAODAIWA KUMUUA MUUZA MADINI: Shahidi adai mtuhumiwa alitoa sharti kuonyeshwa mwili ulikotupwa

Washitakiwa wa mauaji ya Mfanyabiashara wa madini ambao ni Maofisa wa Polisi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara. Picha na Maktaba.

Mtwara. Shahidi wa tatu katika kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa  polisi mkoani Mtwara, ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara kuwa mmoja wa watuhumiwa  alivyokwenda kuonyesha walikoutupa mwili alitoa sharti moja.

Shahidi huyo, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Yustino Mgonja amebainisha sharti alilolitoa  mtuhumiwa huyo, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Grayson Mahembe kuwa alichagua timu ya wapelelezi ambao alieleza yuko tayari kwenda kuwaonyesha huku akimkataa yeye na timu yake.

Pia, Mgonja ameeleza timu ya wapelelezi hao aliowakubali walipofika mahali hapo ilikuta mbavu nne tu, lakini baadaye yeye alipokwenda na timu yake na wataalamu baada ya kukagua zaidi walipata mbavu nane na mifupa miwili ya mguu wa kulia.

Mgonja wakati wa mauaji hayo shahidi huyo alikuwa Mkuu Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mtwara (RCO), kwa sasa ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, jijini Dar es Salaam.

Ametoa maelezo hayo leo Novemba 17, 2023 katika mwendelezo wa ushahidi wake wenye simulizi ya jinsi mfanyabiashara huyo alivyouawa, akibainisha matukio ya kabla, wakati na baada ya mauaji hayo, kwa maelezo aliyoyapata kwa mashuhuda na watuhumiwa katika upelelezi na timu yake.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya namba 15/ 2023 ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara (OC- CID), Mrakibu wa Polisi (SP), Gilbert Sostenes Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, (OCS), Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Maurice Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Stanslaus Kisinza, A/Insp Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi (Insp) John Yesse Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, A/Insp Shirazi Ally Mkupa na Koplo Salim Juma Mbalu.

Maofisa hao wa polisi wanakabiliwa na shtaka la mauaji wakidaiwa kumuua Mussa kwa kumchoma sindano ya usingizi na kisha kumziba mdomo na pua kwa tambala katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Kesi ya maofisa hao saba wa polisi mkoani Mtwara inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika mwendelezo wa ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu, shahidi huyo alidai kuwa Mussa aliuawa na SP Kalanje kwa kumziba kwa tambala mdomoni na puani.

Kwa mujibu wa ACP Mgonja, SP Kalanje alichukua hatua hiyo muda mfupi baada ya Dk. Msuya (mshtakiwa wa tano) kumdunga sindano ya usingizi mfanyabiashara huyo.

Sindano hiyo alidai  aliipendekeza Dk Msuya  ambayo alidai ingemfanya aeleze matukio yote ya uhalifu aliyokuwa ameshayafanya baada ya kuzinduka, badala ya kumdunga sindano ya sumu aliyokuwa ameipendekeza SP Kalanje kwa madai wanataka wampoteze kabisa.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada ya kuwahoji baadhi ya askari waliokuwa zamu katika kituo cha Polisi Mitengo, Dk Msuya mwenyewe na A/Insp Grayson (marehemu) ambao walisimulia tukio hilo.

Wakati wa tukio hilo, ACP Mgonja alikuwa RCO Mkoa wa Mtwara na kiongozi wa timu ya wapelelezi watano wa polis na timu ya askari wa kikosi maalumu ya kukabiliana na ugaidi kilichoongozwa na SP Simba aliyoiomba iungane nao kuanzia wakati wa kumhoji mtuhumiwa Grayson.

Kwa mujibu wa ACP Mgonja walikubaliana kuwa kabla ya kumhoji Grayson, walimleta Dk Msuya  asimulie mbele yake Grayson nini kiliendelea pale Mitengo kama alivyokuwa amemsimulia yeye.

Dk Msuya alisimulia hivyo na walipomuuliza Grayson akakubali kuwa alivyosimulia Dk Msuya ndivyo walivyofanya.

Hivyo, alimtaka Grayson awaoneshe huyo waliomuua yuko wapi, ndipo akatoa sharti kwamba yuko tayari kuwaonyesha  wale askari wa kikosi kazi chini ya SP Simba na si wapelelezi wa timu ya awali aliyoiongoza yeye ACP Mgonja, sharti ambalo walikubaliana nalo.

Hata hivyo, ACP Mgonja alimwelekeza SP Simba kwamba endapo wataonyesha na kuthibitisha, basi awajulishe nao waende kushuhudia na kuthibitisha na wakaondoka kwenda eneo la tukio siku hiyohiyo Januari 21, 2022 yapata muda wa saa tano usiku.

Akiwa katika kituo cha Polisi Mtwara na timu yake baada ya dakika kama 50, ACP Mgonja alipokea simu kutoka kwa SP Simba akimjulisha kuwa wamefika eneo la tukio ni jirani na kiwanda cha Sementi cha Dangote kuna mtu mkubwa mahali panaitwa Majengo Kata ya Hiari.

ACP Mgonja alitaka kujua wameona nini na SP Simba akajibu kuwa kwanza wamekutana harufu kali sana kama ya uozo  na kwamba baada ya kumulika na tochi eneo hilo waliona mabaki kama ya mbavu nne.

Hivyo, ACP Mgonja na timu yake nao walikwenda eneo la tukio kwa mwongozo wa SP Simba, ambako  pia alisikia harufu ya uozo lakini baada ya kuhesabu zile mbavu alipata tano.

Alielekeza eneo lile tuzungushie utepe na pia akaelekeza askari wawili wenye bunduki Ditektivu Koplo (DC) Denis na Ditektivu Sajenti (DS) Diamond wakilinda mpaka asubuhi watakapokwenda na wataalamu kuchunguza mabaki hayo.

Pia alielekeza Insp Abubakar aandike maelezo ya nyongeza ya Grayson  kwenye maelezo yake ya awali katika jalada la uchunguzi.

Pia ACP Mgonja alimuelekeza DC Denis kwamba baada ya Grayson kumaliza kuandika maelezo yake amuweke mahabusu naye akafanya hivyo pale Mitengo chumba cha pekee yake na akawajulisha tena RPC na DCI

Januari 22, 2022, ACP Mgonja aliamka na jukumu la kutafuta timu ya wataalamu kwa ajili ya kwenda eneo la tukio walikoona zile mbavu na kufanya uchunguzi kuzibaini kama ni za binadamu na kuthibitisha walichokuwa wanakitafuta yaani mwili wa Mussa.

Hivyo  alimtafuta daktari wa Hospitali ya Mkoa, Mkemia, kutoka ofisi ya Mkemia Mkoa wa Mtwara, mwakilishi wa Ofisi ya Mwendesha mashtaka Mkoa wa Mtwara, Mwenyekiti wa Kijiji cha Majengo na Mtendaji wa kata ya Hiari.

Pia aliandaa askari wa  kitengo cha wanne wa kikosi cha uchunguzi wa sayansi jinai wakiongozwa na Inspekta Apobokile.

Taarifa za kujinyonga Grayson

Wakati akiendelea kukusanya timu ya wataalamu hao, muda wa  saa nne asubuhi alipokea simu ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mtwara (OCD), Mrakibu wa Polisi Mwandamizi (SSP) Nguvila akimjulisha kuwa kwenye kituo cha Mitengo A/Insp. Grayson amejinyonga akiwa mahabusu.

Yeye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara (RPC) na timu yake ya wapelelezi na ya Forensic na walipofika kituoni Mitengo walishuhudia kweli Grayson amejinyonga akiwa  amening'inia kwenye kamba aliyokuwa ameifunga kwenye dirisha.

RPC alielekeza lifunguliwe jalada la kifo cha mashaka cha Grayson na likafunguliwa, kisha akamuelekeza naendelee kukusanya timu ya wataalamu kwenda eneo tukio walikoonyshwa kuwa ndiko ulikotupwa mwili wa Mussa.

Baada ya kuwapata wataalamu wote walielekea eneo la tukio hilo ambako walifika saa 5:30 wakawakuta mwenyekiti wa Koji cha Majengo na Mtendaji wa kata ya Hiari wakiwa wameshafika pamoja na askari waliowaacha kulilinda eneo hilo ambalo pia lilikuwa kama walivyoliacha.

Baada ya kuwapatia maelezo ya kile walichokuwa wamekiona usiku, wataamu hao daktari, Mkemia na watu wa kitengo cha uchunguzi wa sayansi jinai waliingia kwenye lile eneo wakusanye vitu walivyokuwa wanavipata. 

Wao waliona mbavu nyingine tatu pamoja na zile tano za awali zikawa tano. Pia sehamu nyingine waliona mifupa miwili ya miguu na sehemu nyingine pia kulikuwa na kama uozo na kulikuwa na funza wakaweka alama na kupiga picha.

Daktari alieleza kwa  ufupi palepale kwamba kwa utaalamu wake zile mbavu ni mbavu za binadamu.

Baada ya kupiga picha na kuchora ramani, mkemia na Apobokile walikusanya vile vielelezo. Pale walichukua mbavu nane na mifupa miwili ambayo daktaria alisema ni ya mguu wa kulia, suruali na funza.

ACP na timu yake walifanya kazi yao ya kikachero kwa maana ya kuandika maelezo ya mashuhuda na wote waliokuwepo pale.

Mabaki hayo yalichukukiwa na Mkemia na Apobokile wakavipeleka  ofisini kwa ACP Mgonja, ili aandike barua kuvikabidhi kwa mkemia kwa mujibu wa utaratibu, baada ya kuviwekea lakiri.

"Kwa unyeti wake kwamba ni viungo vya binadamu ambavyo vikitoa majibu vitaunganisha kesi yetu, niliona bora vikae ofisini kwangu, hivyo nilikuwa navitunza mimi kwenye kasiki", alieleza ACP Mgonja na kuongeza:

"Vitu hivyo vilikaa ofisini kwangu toka Jumamosi ya Januari 22 mpaka Jumanne Januari 24, 2022. Siku hiyohiyo (Januari 22) mwili wa Grayson ulisafirishwa kwenda kwao (Tabata- Segerea, Dar es Salaam kwa mazishi)

Januari 23 ACP Mgonja alimpigia  mjomba wa marehemu,  Salum Ng'ombo amtafute mama wa marehemu, Hawa Bakari ili aende  azungumze naye akikubali aende kuchukuliwa sampuli (mpanguso wa mate) akafanyiwe vipimo vya vinasaba (DNA).

Pia aliwajulisha RPC na DCI kuwa kwa ushahidi ambao wameukusanya, unawahusisha askari wao, hivyo akaomba kibali cha kuwakamata na kuwahusisha mauaji hayo.

Januari 24 idhini ikatoka kufungua jalada la mauaji  ambapo walifungua jalada la mauaji kumbukumbu namba MTR/IR/154/2022 na akaelekezwa watuhumiwa wote wahojjwe kuhusiana na mauaji ya mfanyabiashara huyo.

Kesi hiyo itaendelea Jumatatu, Novemba 20, 2023.