Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

RPC asimulia mipango ya mauaji ya muuza madini

Washitakiwa wa mauaji ya Mfanyabiashara wa madini ambao ni Maofisa wa Polisi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara. Picha na Maktaba.

Mtwara. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Yustino John Mgonja ameieleza Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara namna mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis Hamis, alivyouawa.

Pia, amewataja washtakiwa waliokuwepo eneo la tukio na yule anayedaiwa kutekeleza mauaji hayo ya mfanyabiashara huyo aliyekuwa mkazi wa Nachingwea mkoani Lindi.

ACP Mgonja alitoa maelezo hayo jana wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya mauaji inayowakabili maofisa saba wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara. Yeye ni shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka kati ya mashahidi 72 wanaotarajiwa kuitwa na upande wa mashtaka katika kesi hiyo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 15 ya mwaka 2023 ni pamoja na aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Mtwara, Gilbert Sostenes Kalanje na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango.

Wengine ni aliyekuwa Ofisa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Nicholaus Kisinza, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, John Msuya, aliyekuwa mganga mkuu wa Zahanati ya Polisi Mtwara, Shirazi Mkupa na Koplo Salim Mbalu.

Maofisa hao wa Polisi wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji wakidaiwa kumuua kwa makusudi Mussa waliyemchoma sindano ya sumu katika kituo cha Polisi Mitengo Wilaya ya Mtwara, Mkoa wa Mtwara, Januari 5, 2022.

Hata hivyo, wakati polisi hao wakiwa mahabusu kabla ya kupandishwa kizimbani, mtuhumiwa mwenzao, Grayson Mahembe alidaiwa kujinyonga hadi kufa Januari 22, 2022 akiwa mahabusu.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji Edwin Kakolaki kutoka Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Pascal Marungu aliieleza mahakama kuwa Mussa aliuawa na SP Kalanje Kwa kumziba kwa tambala mdomoni na puani, muda mfupi baada ya Dk Msuya (mshtakiwa wa Tano) kumdunga sindano ya usingizi.

Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa alipata taarifa za tukio hilo baada ya kuwahoji baadhi ya askari waliokuwa zamu katika kituo cha Polisi Mitengo, pamoja na Dk Msuya mwenyewe na ofisa wa polisi, Grayson (marehemu kwa sasa) ambao walisimulia tukio hilo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, siku ya  tukio Januari 5, 2022, mshtakiwa wa kwanza, SP Kalanje alimpigia simu Dk Msuya akamtaka waonane na Dk Msuya ambaye al8ikaribisha ofisini kwake katika zahanati ya Polisi na wakazungumza.

Alidai kuwa SP Kalanje alimueleza Dk Msuya kuwa wana mtuhumiwa wao wa wizi wa pikipiki ambaye amekuwa akifanya matukio ya wizi huo maeneo mbali katika mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam na amekuwa akiwasumbua hivyo wanataka wammalize.

Hivyo alidai kuwa SP Kalanje alimuuliza Dk Msuya kama anaweza kufanya namna ya kupata sindao ya sumu ili wamdunge, lakini Dk Msuya alimjibu kuwa tangu aajiriwe na kuapa kuwa daktari hajawahi kumdunga mtu sindano ya sumu.

Shahidi huyo amedai kuwa badala yake. Dk Msuya alimshauri SP Kalanje wamdunge sindano ya usingi , akizinduka ataanza kueleza matukio yote ya wizi aliyoyafanya, ushauri ambao Kalanje alikubaliana nao.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, licha ya SP Kalanje kutaka waende kutekeleza mpango huo wakati huohuo, lakini Dk Msuya alimueleza kuwa wakati huo bado alikuwa na wagonjwa wengine akiwahudumua na akashauri wafanye baadaye.

Saa 8:30 mchana, Kalanje alifika ofisini kwa Dk Msuya kwa ajili ya kutekeleza mpango huo kama walivyokuwa wamekubaliana, hivyo alimuuliza kama alikuwa tayari akamjibu kuwa alikuwa tayari.

Lakini Dk Msuya alimuuliza SP Kalanje mahali alikokuwa huyo mtuhumiwa wao, akamjibu kuwa alikuwa katika kituo cha Polisi Mitengo.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, Dk Msuya alisema yeye anaelewa kituo cha Mitengo kina wahalifu sugu hivyo akajua na huyo amehifadhiwa kwa wahalifu sugu, akakubali akaingia kwenye gari na akakaa kiti cha mbele huku gari likiendeshwa na SP Kalanje.

Wakati gari inaondoka pale zahanati, Dk Msuya alihisi kama viti vya nyuma vina watu.

Hivyo aligeuka kutazama akawatambua watu wawili, ambao ni ASP Onyango na A/Insp Grayson waliokuwa wamekaa viti vya pembeni kulia na kushoto na katikati kulikuwa na mtu mwingine ambaye hakuweza kumtambua.

Waliendelea na safari hadi kituo cha Polisi Mitengo na SP Kalanje alishuka akaenda kuzungumza na mkuu wa kituo hicho, Paulo Kiula.

Dk Msuya na askari wale wawili pamoja na yule mtu ambaye hakumtambua nao walishuka wakamfuata SP Kalanje na mkuu wa kituo walipokuwa wanaelekea ndani ya jengo la kituo hicho.

Dk Msuya alimuomba OCS Kiula amuonyeshe Kalanje ofisi moja ambayo aliingia Kalanje, Onyango, Grayson na yule kijana na yeye akabaki nje.

Lakini baada ya dakika tatu hivi, naye alingia ndani ya hiyo ofisi na alimkuta yule kijana amevuliwa shati yuko kifua wazi na mikono yake ikiwa imefungwa kwa kamba kwa nyuma akiwa amelala kwenye sakafu huku akilia.

SP Kalanje alimwambia Dk Msuya amdunge sindano ya usingizi mkono wa kulia yule kijana.

Na baadaye kidogo, Dk Msuya anasema alimsikia Kalanje akisema huyo anawachelewesha, akachukua tambala akamziba yule kijana pua na mdomo.

Anasema baada ya Dk Msuya kuona vile aliamua kutoka nje akawaacha Karanje na wale wenzake na yule kijana akiwa amelala chini.

Lakini baada ya muda mfupi, Kalanje alimuita Dk Msuya akamuuliza, "tayari?" huku akimuonyesha yule kijana pale chini.

Dk Msuya alimuangalia kama hapumui lakini hakumpima ila alielewa lile swali la SP Kalanje kwamba lilikuwa linamaanisha kama amekufa na yeye alijibu kuwa tayari.

Hivyo wote walitoka mle chumbani na kumuacha yule kijana akiwa amelala pale chini.

SP Kalanje alikwenda kwa OCS akachukua kufuli likiwa na funguo akafunga mlango kisha wakaondoka wote akiwa na huo ufunguo, wakapanda gari na kuondoka.

Kamanda huyo wa polisi ambaye ni shahidi, aliieleza Mahakama kuwa baada ya maelezo hayo ya mdomo kutoka kwa Dk Msuya, alielekeza yaandikwe maelezo kama alivyosimulia na maelezo yake yawekwe kwenye jalada la uchunguzi.

“Wakati huo tulimchukulia Dk Msuya kama mtoa taarifa,” alidai Kamanda Mgonja.

Alidai wakati yote hayo yakifanyika, alijiuliza hayo mauaji ni ya huyo kijana Mussa ambaye ndugu zake walikuwa wanamtafuta au kuna mwingine?

"Hivyo nikaagiza atafutwe mjomba wa Mussa Hamis anayeitwa Salum Mombo aje ofini kwangu, alikuja nikamtaka anitafutie picha za Mussa kusudi ili niangalie yule mtu ambaye askari wanasema walimuona akiingia pale Mitengo ndiyo huyu kijana Mussa Hamis au ni mwingine,” alieleza.

Shahidi huyo alieleza kuwa mjomba huyo akiwa ofini kwake alipiga simu Nachingwea kwa baba wa kufikia wa Mussa akamtaka atafute picha zake azitume kwenye gari.

"Kesho yake Januari 22, 2022 zililetwa picha nikazitazama nikamkabidhi ASP Esau ili waendelee na utaratibu wa upelelezi,” alieleza ACP Mgonja.

Alidai kulikuwa na mauaji Januari 21,2022 niliagiza apatikane Grayson ambaye alikuwa mahabusu Tandahimba, kwanza kati ya watu wote waliotajwa yeye alikuwa ametajwa maeneo mengi.

Alieleza kuwa baada ya Grayson kuletwa aliongeza timu ya wapelelezi akiwajumuisha askari watano wa timu ya Task Force waliokuwa wanashughulikia magaidi wakingozwa na SP Simba, hivyo ikawa timu ya wapelelezi 10 akiwemo yeye mwenyewe.

"Tulifikiri kwa pamoja tukakubaliana tumlete Dk Msuya ili asimulie mbele ya Grayson nini kiliendelea pale Mitengo kama alivyonisimulia mimi.”

"Kwa kuwa Msuya alishuhudia kila kitu kilichofanyika pale Mitengo na Grayson akiwepo, kwa hiyo sisi kama makachero tuliona Grayson akisikia, basi mahojiano yetu naye yatakuwa rahisi."

Shahidi huyo alihitimisha Kwa kueleza kuwa katika mahojiano ya mdomo waliyoyafanya na Dk Msuya mbele ya Grayson, alisimulia kama alivyokuwa amemsimulia yeye na walipomuuliza Grayson, alikubali kuwa alivyosimulia Dk Msuya ndivyo walivyofanya.

“Hivyo mimi kama RCO picha iliyoniijia kichwani ni kwamba, haya sasa ni mauaji na kama ni mauaji hakuna mauaji ambayo hayana mwili au mtu aliyeuawa, hivyo nikamtaka Grayson atuonyeshe huyo ambaye wamemuua yuko wapi."

Hata hivyo wakati shahidi huyo anataka kueleza kile Grayson alichosema, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Majura Magafu aliweka pingamizi akisema kwa kuwa Grayson si mshtakiwa wala shahidi, hawezi kutoa maelezo yake kwa sababu hawatapata fursa ya kumhoji kuhusu ukweli wake.

Pingamizi hilo liliibua mvutano wa hoja na upande wa mashtaka na Jaji Kakolaki baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha kesi hiyo Kwa ajili ya kuandika uamuzi wake.