Polisi walioshtakiwa kwa mauaji wakataa kesi kwa mtandao

Washitakiwa wa mauaji ya Mfanyabiashara wa madini ambao ni Maofisa wa Polisi wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara. Picha na Maktaba.

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu mkazi Mtwara, imeahirisha kesi ya mauaji inayowakabili maafisa saba wa polisi hadi Agosti 24, 2022 itakapoitwa tena kwa ajili ya kutajwa.

Mtwara. Wakati mshtakiwa namba moja wa kesi ya mauaji, Mrakibu wa Polisi Gilbert Kalanje akishindwa kuhudhuria mahakama kwa njia ya mtandao (VTC) kwa sababu ya kuugua, washitakiwa wenzake wameiomba Mahakama hiyo kuwaruhusu wawe wanakuja mahakamani moja kwa moja.

Kalanje aliyekuwa Mkuu wa upelelezi wilaya ya Mtwara pamoja na wenzake sita wanashitakiwa kwa mauaji ya mfanyabiashara wa madini na mkazi wa Kijiji cha Ruponda, Wilayani Nachingwea mkoa wa Lindi, Musa Hamis (25) siku ya Januari 5, 2022.

Kesi hiyo ambayo kwa mara ya kwanza ilifikishwa mahakamani hapo Januari 5, 2022 ilianza kusikilizwa kwa njia ya mtandao Juni 6, 2022 kwa kile kilichoelezwa na Hakimu huyo kuwa ni maagizo kutoka juu.

Akijibu maombi ya washitakiwa hao leo Jumatano Agosti 10, 2022, Hakimu Kasebele amesema mahakama nayo ni sehemu ya maendeleo ya teknolojia.

"Tumesikia hoja yao na haya ni maagizo kutoka juu kwamba kesi ambazo upelelezi bado unaendelea tuzitaje kwa njia ya mtandao, mahakama nayo ni sehemu ya maendeleo ya teknolojia hatuwezi kujitenga," amesema Hakimu Kasebele.

Kalanje na washitakiwa wengine sita wapo katika gereza la Lilungu lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Hata hivyo, Hakimu Kasebele amesema hafahamu Kalanje anasumbuliwa na maradhi gani lakini ameelezwa na askari magereza kuwa mshtakiwa huyo anaumwa.

"Kwa kweli sijui anaumwa nini lakini nimeelezwa kuwa anaumwa kwa hiyo hakuweza kuhudhuria kesi ambayo tumeiendesha kwa njia ya mtandao,” amesema.

Akielezea mwenendo wa kesi, Wakili wa serikali Mwandamizi, Wilbroad Nduguru amesema kuwa upelelezi bado haujakamilika hivyo kuomba tarehe kwa ajili ya kutajwa tena.

Hakimu Kasebele ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 24, 2022.

Washtakiwa wengine wa kesi hiyo ni pamoja na Mrakibu wa polisi aliyekua Mkuu wa kituo cha polisi Mtwara, Charles Onyango, Mrakibu wa polisi aliyekua Mkuu wa Intelijensia mkoa, Nicholaus Kisinza, Mkaguzi wa polisi, John Msuya, Mkaguzi msaidizi wa polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa polisi, Shirazi Ally Mkupa na Askari namba G5158 Koplo Salum Juma Mbalu.