Utingo, majeruhi waeleza kilichotokea ajali iliyoua 25
Muktasari:
- Serikali yatoa mkono wa pole Sh1 milioni kwa kila mwili, kugharimia matibabu kwa majeruhi.
Arusha. Utingo wa lori la mizigo lililohusika katika ajali ya magari manne iliyosababisha vifo vya watu 25 jijini hapa, ameeleza alivyojaribu kupiga kelele na kuonyesha ishara kwamba gari lao haliko salama.
Jastus Juma, utingo wa lori lililosababisha ajali likitokea Kenya kuelekea Dar es Salaam, ambaye ni mmoja wa majeruhi ameeleza hayo leo Februari 25, 2024 akiendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Ajali hiyo ilitokea jana Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), mkoani Arusha katika Barabara Kuu ya Arusha-Namanga.
Imesababisha vifo vya watu 25 wakiwamo raia saba wa kigeni na kujeruhi wengine 21. Lori hilo linaelezwa kufeli mfumo wa breki, hivyo kupoteza mwelekeo na kugonga magari mengine madogo matatu.
Juma, raia wa Kenya amesema lori hilo likiwa limebeba buldoza awali halikuwa na changamoto yoyote.
Amesema lori hilo lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba ZF 6778 ni mali ya Kampuni ya KAY Construction ya Nairobi nchini Kenya.
Amesema, “Tulipofika kwenye mteremko, dereva nikawa namuuliza shida iko wapi akawa ananiambia breki haishiki, nikawa najaribu kupiga kelele watu watoke barabarani tusiwakanyage.”
“Tulipokutana na magari mengi kwenye kona hawakuweza kutoka na hapo ndipo ajali ilipotokea. Awali gari halikuwa na tatizo kabisa zaidi ilipata changamoto ya gurudumu tukabadilisha na baadaye tukapita mahali sijui panaitwaje breki ndipo ilianza kufeli na kupoteza mwelekeo,” amesema.
Ameeleza, “Baada ya ajali kutokea ikawa mimi nina nafasi ya kutoka, nikawa najisaidia nitoke kwenye gari. Nilipoanguka nje palepale watu wakatusaidia wakatubeba, wakatuweka kwenye daladala wakatuleta hapa. Nauliza sijui dereva yuko wapi, anaitwa Joseph Kiru.”
Majeruhi mwingine, Jovin Daud amesema alikuwa akizungumza na dereva wa daladala akiwa nje ya gari ndipo alipogongwa na kuanguka mtaroni. Amepata majeraha kwenye mguu na kichwani.
“Mimi nilikuwa eneo la tukio nazungumza na dereva wa daladala, mara nikashangaa naona Coaster imeanguka, imegongwa na gari kubwa, ikaja ikapiga daladala na mimi nilikuwa jirani ikanigonga, nikarushwa mtaroni. Nikaona watu wengine gari lao linazidi kupondwa. Nimeumia mguu na kichwa kidogo japo sijaumia sana,” amesema.
Kiundu Roika, mkazi wa Nanja amesema: “Nilikuwa naeleka Oldonyosambu kumfuata mke wa kaka yangu na nikapanda daladala na baba yangu, nilikuwa nimekaa siti ya mbele na dereva na mtu mwingine. Baba alikaa nyuma ya dereva, gari lilisimama pale kuchukua abiria ndipo ghafla tukagongwa. Baba alifariki papo hapo.”
Apelo Apeto, raia wa Togo ni mmoja wa majeruhi anayeendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa huduma nzuri za afya wanazoendelea kupatiwa.
Mkono wa pole
Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa pole na kuahidi Serikali kugharimia matibabu kwa majeruhi na mkono wa pole wa Sh1 milioni kwa kila aliyepoteza maisha.
Taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella imesema Serikali itatoa majeneza kwa familia ambazo zitahitaji.
"Rais amefikisha pole zake kwa familia zote na maelekezo yake ni kwamba, Serikali tuhusike kikamilifu kwenye jambo hili, baada ya maelekezo hayo Serikali ya mkoa tumesema wale ambao wako tayari kuchukua miili na kiimani na maelekezo ya familia kwenda kuihifadhi tutafanya hivyo,” amesema.
Taarifa imesema, “Kama Serikali tutatoa Sh1 milioni kwa kila mwili ili kwa haraka kusaidia familia. Mchango huu wa Serikali kwa maelekezo ya Rais, wala si kwamba unaziba pengo la ndugu zetu tuliowapoteza maisha ila Serikali imesema kwa sababu ni wananchi wake ili turahisishe kuwahifadhi na kwa wale ambao watahitaji jeneza Serikali tutatoa.”
Raia wa kigeni
Awali, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini alisema raia saba wa kigeni waliofariki katika ajali hiyo wametoka mataifa ya Marekani, Togo, Afrika Kusini, Uingereza na Nigeria. Mataifa mengine mawili hayakuweza kupatikana.
“Ajali hii imehusisha raia wa kigeni kutoka mataifa saba na wengi (majeruhi) nimeongea nao wameridhika na huduma wanazopatiwa kuanzia walipopata ajali,” amesema.
Amesema walikuwa nchini kwa shughuli za kujitolea katika Shule ya New Vision na walikuwa wanatarajia kuondoka nchini Ijumaa wiki hii.
“Taarifa walizotupatia walikuwa wamekuja kujitolea New Vision, wamekuwa na utaratibu wa kutembelea shule na mataifa mbalimbali kwa ajili ya kujifunza. Walikuwa hapa kwa ziara ya mafunzo na tumeambiwa Ijumaa hii walikuwa wamalize ziara yao na kuondoa kurejea kwao,” amesema.
Ameagiza Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi wa magari na ukaguzi badala ya kusubiri wiki ya nenda kwa usalama barabarani.
“Tumetembelea lile gari tumeona hali yake ni kweli ajali zipo ila gari linaonekana lina hali ya kuchoka. Tuweke mifumo ya kukagua magari yanayotoka nje yanapoingia nchini. Upo utaratibu wa ukaguzi wa magari wa kawaida, gari limetokea Kenya limekuja kuleta madhara hapa na linaonekana limechoka lingekaguliwa mpakani na kugundulika lina tatizo lingezuiwa, mpaka lirekebishwe,” amesema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru, Dk Alex Ernest amesema jana Februari 24, 2024 walipokea majeruhi 11 na miili 21.
Mingine minne ilipokewa katika hospitali nyingine ila kwa sasa yote imehifadhiwa hapo.
Amesema kati ya majeruhi wote 11, wanawake ni wawili na wanaume tisa, na raia wa kigeni ni saba.