Utiririshaji majitaka nyumba za wageni wawaponza viongozi Mtaa wa Midizini

New Content Item (1)

Mwenyekiti Mtaa wa Midizini (mwenye kanzu), akiwa ameshika bendera ya balozi wa uchafu baada ya kukabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba (mwenye shati la bluu aliyeshika kipaza sauti). Picha na Nasra Abdallah

Muktasari:

  • Katika kampeni hiyo, Serikali ya Mtaa wa Manzese iliibuka mshindi na kupata zawadi ya Sh600,000 huku Mtaa wa Madizini ukiambulia bendera hiyo ya balozi wa uchafu ambayo viongozi wa mtaa huo wanatakiwa kukaa nayo.

Dar es Salaam. Utiririshaji wa maji machafu katika nyumba mbalimbali za wageni, umewaponza viongozi wa Serikali ya Mtaa wa Midizini uliopo katika kata ya Manzese mkoani hapa baada ya kupata bendera ya kuwa kinara wa uchafu katika wilaya ya Ubungo.

Mkuu wa wilaya hiyo, Hashim Komba amewakabidhi bendera hiyo leo Februaru 17, 2024 alipokwenda kukabidhi bendera hiyo iliyoandikwa “Balozi wa uchafu Ubungo” ikiwa ni kampeni ya Kataa Uchafu, Safisha, Pendezesha Ubungo (Kausapeu) iliyoanza miezi mitatu iliyopita kwa lengo la kuweka wilaya hiyo katika hali ya usafi wakati wote.

Katika kampeni hiyo, Serikali ya Mtaa wa Manzese iliibuka mshindi na kupata zawadi ya Sh600,000 huku Mtaa wa Madizini ukiambulia bendera hiyo ya balozi wa uchafu ambayo viongozi wa mtaa huo wanatakiwa kukaa nayo.

“Pamoja na mambo mengine, jambo kubwa lililouponza mtaa huo ni kuwepo kwa utiririshaji hovyo wa maji taka katika mitaro na hivyo kuufanya kuonekana mchafu wakati wote.

“Niwaombe wananchi wa mtaa huu, mshirikiane kuwabana na kuwachukulia hatua mtakaowabaini wanatiririsha maji hayo, kwani mbali na kuwapa sifa mbaya ya uchafu lakini pia wanahatarisha afya zenu.

“Pia, kila mwananchi anapaswa kuona fahari ya kusafisha mazingira yake kila wakati jambo litakalowafanya kuepuka magonjwa ya mlipuko,” amesema Komba.

Hata hivyo, wakati bendera hiyo ya uchafu ikitakiwa kupeperushwa katika ofisi za Serikali ya Mtaa na kukaa hapo miezi mitatu mfululizo, Komba amebadili msimamo huo na badala yake amewaambia itakaa kwenye droo la meza ya mwenyekiti wao ikiwa kama onyo la kuwataka wabadilike.

Hatua hiyo imefuata baada ya wananchi wa eneo hilo akiwemo Abdul Karim, kuomba wapewe onyo kwa kuwa ndio mara yao ya kwanza na kuahidi miezi mitatu ijayo watasimamia kwa karibu suala la usafi.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa mtaa huo, Abbas Abeid ameshukuru uamuzi huo na kuahidi safari inayokuja Midizini itakuwa tofauti kwa kuwa kama kiongozi imemfedhehesha.

Hata hivyo, Abeid amesema moja ya changamoto wanazokumbana nazo ni wananchi kutokuwa tayari kulipa tozo ya uzoaji takataka na kuahidi kuwa watazidi kutoa elimu ili kila mmoja aje kujua ni wajibu wake kufanya hivyo.