Wataka sheria kudhibiti uharibifu mazingira

Muktasari:
Wananchi Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameomba sheria zitungwe kudhibiti uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji miti, uharibifu vyanzo vya maji na uchomaji misitu hasa kipindi cha kiangazi.
Buhigwe. Wananchi Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma wameomba sheria zitungwe kudhibiti uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na ukataji miti, uharibifu vyanzo vya maji na uchomaji misitu hasa kipindi cha kiangazi.
Wakizungumza Novemba 22, 2023 katika kijiji cha Biharu wakati wa uzinduzi wa upandaji miti zaidi ya 2,000,000 itakayopandwa maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe ikiwa ni mpango wa Tuungane kwa msimu wa mwaka 2023/24, wamesema utungwaji wa sheria hizo utasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira katika maeneo yao.
Mkazi wa kijiji cha Biharu, Shedrack Meshack amesema Serikali na wadau wa mazingira wamekuwa wakijitoa na kujitahidi kupanda miti katika maeneo mbalimbali lakini wananchi wamekuwa sababu ya kuharibu mazingira kwa kuikata na kufanya shughuli za kibinadamu hivyo utungwaji wa sheria utasaidia kukomesha jambo hilo.
“Baadhi ya wananchi wanachoma misimu nyakati za kiangazi jambo ambalo ni hatarishi kwa mazingira yetu, wanalima kandokando ya vyanzo vya maji na kulisha mifugo yao jambo ambalo si sawa ila kama sheria itakuwepo ikiambatana na adhabu jambo hili litafika mwisho,”amesema Meshack
Naye Mariam Ramadhani amesema wananchi hawana uelewa wa kutosha kuhusiana na utunzaji wa mazingira hivyo Serikali na wadau wasichoke kutoa elimu hiyo mara kwa mara juu ya umuhimu wa utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti, kutokutana miti na kutunza vyanzo vya maji.
Mkurugenzi wa Mpango wa Tuungane, Lukindo Hiza amesema mpango huo ni kwaajili ya kurudisha uoto wa asili uliopotea kwa shughuli za kibinadamu na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha uharibifu wa mazingira.
“Uharibifu wa mazingira kwenye ukanda wetu wa Magharibi unakuwa kwa kasi sana na ni eneo kubwa ambalo ndio kuna uoto wa asili uliobaki, sisi kama watu wa Tuungane tumejikita kwenye jambo hili pia kwaajili ya kuendeleza utunzaji wa mto maragalasi ambao unapeleka maji katika Ziwa Tanganyika,”amesema Hiza
Mkuu wa kitengo cha Maliasili na Mazingira Halmashauri ya wilaya ya Buhigwe, Asha Luhuly amesema uhifadhi katika halmashauri hiyo unakabiliwa na changamoto ya kilimo cha bustani na kupanda miti ambayo si rafiki wa maji karibu na vyanzo vya maji na kusababisha uharibifu na uchafuzi wa vyanzo vya hivyo.
Amesema hali hiyo inasababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko na uhaba wa rasilimali maji pamoja na mwamko mdogo wa jamii kushiriki katika shughuli mbalimbali za uhifadhi ikiwemo ya upandaji miti na kulinda uoto wa asili.
Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina amewaonya wananchi wanaochoma moto misitu kipindi cha kiangazi akidai wanaua mbolea ya asili iliyopo ardhini pamoja na viumbe wanaosaidia kukua kwa mazao wakati wa kilimo.