UWAZIIII ZIIII!

What you need to know:

  • Sijui kama majirani wamefikia mwisho wa mchakato wao au kama bado muvi inaendelea, lakini mimi kwanza sina budi kuwalaumu sana kwa kuvuruga usingizi wangu na njozi ya ajabu kabisa. Niliota hivi.

Sijui kama majirani wamefikia mwisho wa mchakato wao au kama bado muvi inaendelea, lakini mimi kwanza sina budi kuwalaumu sana kwa kuvuruga usingizi wangu na njozi ya ajabu kabisa. Niliota hivi.

Nilikuwa nimekaa mahali nikitafakari juu ya wizi na uwazi katika uchaguzi. Wezi waweza kuvuruga uwazi au uwazi ndio kiboko cha wizi?

Wakati ninatafakari hivi, nikakuta niko nimekaa meza moja na jamaa mmoja niliyemtambua kama ni mnene fulani wa nchi yetu, ingawa nilishindwa kujua kama ni mnene wa mpira au wa siasa (si yote ni michezo!). Lakini kila nilipojaribu kuongea naye au hata kumsalimia anitambue na mimi akaashiria yuko bize na simu yake. Kwa hiyo, bila kupenda, ilibidi nimsikilize.

“Unasemaje jamani? Yaani bora tuwasiliane kwa mtandao? Kwani mtandao bado unafanya kazi? Usiniambie hahaha! Watu wa VPN watakoma. Lakini iweje watu waweze kufuatilia mubashara? Kwa nini wamefanya upumbavu wa aina hiyo? Nani alikuwa mzembe? Lazima afukuzwe kazi aisee.

Eti nini? Hakuna uzembe. Wameacha watu waongee wakati wa uchaguzi? Sasa watawezaje kupanga matokeo? Unasemaje? Hawataki kupanga matokeo? Mungu wangu! Wana akili kweli?

Enhee! Enhee! Hivi umevuta bangi wewe? Kila gazeti linahesabu matokeo? Kila kituo kinaonesha wazi matokeo? Haiwezekani. Na kuna kituo huru kinachofanya mahesabu yote tofauti na tume ya uchaguzi. Ai ai ai ai ai! Mbona hawakujifunza kutoka kwetu. Sisi tulifunga kituo kile huru na kuchukua kompyuta zote ndiyo maana tulimaliza vijiherehere vya wapinzani uchawara! Ha ha ha.

Unasemaje? Hawataki kumaliza vijiherehere vya watu? Eti uchaguzi wa kweli ni uchaguzi wa wazi? Sasa naamini kweli umevuta bangi. Utafanyaje wizi ndani ya huu uwazi?”

Ama kweli hawa majirani zetu wametuaibisha sana. Naona wamekuwa vibaraka wa mabeberu kabisa. Hawajui utamaduni wetu wa Afrika Mashariki? Bosi ni bosi. Bosi hajambi, anatamba. Sasa wanataka kutuvua nguo sisi ambao tunajua kwamba ili pasiwe na uchafuzi wa ushuuzi katika uchaguzi, ni lazima kutumia ubaguzi. Unachagua kabla ya uchaguzi, wengine wasilete kuconfyuzi. Dah! Ndiyo mila zetu. Kwani mtemi alichaguliwa? Kweli tumeondoa mila ya urithi kifamilia lakini bado tunajua umuhimu wa kurithisha. Unawaridhisha wananchi kwa kuwapa nafasi ya kuchagua huku unapanga kurithisha. Basi Bwana inatosha. Ngoja nipumzishe akili maana habari hizi zimenitibua kabisa. Sijui tutafanyaje mbele ya safari.”

Akaweka simu chini, nikataka kumsalimia na kujipendekeza kidogo, lakini akapigiwa simu nyingine.

“Hello. Nani? Rais mstaafishwa wa Marekani anataka kuongea nami? Sawasawa.”

Jamaa akajipanga vizuri kwenye kiti, akavutavuta suti yake aonekane vizuri kama vile yuko kwenye runinga. Nikabaki nashangaa huyu mstaafishwa amejua wapi Kiswahili.”

“Habari gani mheshimiwa? Nashukuru sana kwa heshima hii. Nikusaidie nini? Uchaguzi wa Kenya? Tunabaki tunashangaa.

Oh kumbe na wewe uliwapigia? Ulitaka kumfundisha mzee mwenzio jinsi ya kushinda? Eti kwa nini hakutaka kuwashinikiza wanaohesabu kura kutafuta kura za ziada kama ulivyofanya wewe? Na alikataa? Jamani jamani. Kumbe hata wewe unaona majirani zetu wametuaibisha sana katika mipango yetu ya demokrasia dhibitishi? Unajua sisi tulituma watu wetu wengine kama waangalizi ili watoe angalizo kwa wenzetu. Kwa nini hawakutaka kujifunza kutoka kwetu? Inasikitisha sana Mheshimiwa Rais Mstaafishwa lakini ujue tu tuko pamoja. Upande wetu tumejifunza mengi kutoka kwako. Na bila shaka umejifunza kutoka kwetu pia. Bila kudhibiti hii demokrasia, usalama wetu utatoka wapi? Haya mheshimiwa, tunakutakia ushindi katika mchezo wako pendwa golf. Nasikia kule ni mtaalam wa kubadilisha matokeo hata katika mchezo ha ha ha.

Ah hapana mheshimiwa, hapana, ni utani tu. Tuko pamoja mheshimiwa. Karibu kwetu.”

Hatimaye nilifikiri nitapata nafasi ya kumwaga sifa za sifuri, lakini alikuwa ameshapiga simu kwa yule mtu wa kwanza.

“Haya Bwana, nimeshaongea na Rais mstaafishwa wa nchi, kiongozi wa kinachoitwa dunia huru. Na yeye pia anajua uhuru maana yake ni watu kuwa na uhuru wa kuchagua ili sisi tuwe na uhuru wa kuamua. Bila hivyo huwezi kujua mambo yatakuwaje?”

“Eti nini? Bila uhuru ule asingechaguliwa Rais? Kwa hiyo? Bado alikuwa Rais na bado anajua kwamba ukishapata, shika, vinginevyo utapatikana. Hitler naye alijua lakini yule alishindwa kushika vizuri na sasa amepatikana.

Sasa hebu niambie. Hakuna dalili yoyote ya fujo pale? Bora pawe na fujo ionekane wazi kwamba uwazi ni adui wa uchaguzi. Nasikia hawaelewani, basi bora wapigane tuweze kuonesha kwamba demokrasia dhibitishi ndiyo njia bora. Usalama kwanza!

We Bwana acha kuvuta bangi huko. Tulikupeleka kuwa mwangalizi wa uchaguzi, ili kuhalalisha uchaguzi, sasa unasema umeenda kujifunza njia bora za kuendesha uchaguzi. Kwamba majirani walikuwa wamechoka na vificho vilivyoleta vifo vya watu ndiyo maana wameng’ang’ania uwazi katika mchakato mzima wa uchaguzi. Na kwamba fujo ikitokea sasa ni kwa sababu wengine walifanya mambo mengine kwa kificho? Ghafla umekuwa nabii wa uwazi?

Sikiliza Bwana, bora urudi hapa na kuniambia kwamba ulikuwa umelewa. Vinginevyo huna nafasi tena na wewe. Kufuru!”

Mnene yule akazima simu kwa nguvu. Kisha akaamka na kuanza kupaza sauti kwa nguvu.

UWAZI ZIII. UWAZI ZIII. UWAZI ZIII !!!

Hadi niliposhtuka na kelele zake na kukuta niko kitandani. Ndoto ya ajabu sana. Bora niachane na kufuata uchaguzi wa watu. Sijui wa kwetu utakuwaje?