UWT yapendekeza waharibifu wa maadili ‘wahasiwe’

Muktasari:

  • Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), umeandaa sherehe za kumpongeza Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufikisha miaka miwili madarakani.

Dar es Salaam. Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) umependekeza Serikali ifanye marekebisho ya sheria na kuleta sheria kali kudhibiti vitendo vya mapenzi ya jinsia moja vinaovyoonekana kushika kasi kwa sasa.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda ametoa ombi hilo leo Jumapili, Machi 19, 2023 wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka miwili ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, zilizofanyika Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Samia aliyekuwa Makamu wa Rais, aliapishwa Machi 19, 2021 kuwa Rais wa Tanzania baada ya aliyekuwa Rais John Magufuli kufariki dunia Machi 17, 2021 jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Chatanda amesema kama Serikali itaona vyema ziwepo sheria zinaowabana wanaofanya vitendo hivyo na wanapobainika wahasiwe.

“Hawa wakibainika wahasiwe maana tukiwaacha wataendelea kuliharibu taifa letu,” amesema Mary, kauli iliyopokelewa kwa shangwe na wanawake waliokuwa kwenye sherehe hizo.

Mary pia ametoa ahadi kwa niaba ya wanawake wote walio katika nafasi kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa ili kumuunga mkono Rais Samia katika ujenzi wa taifa na kuleta ustawi wa nchi