Vazi la taifa bado kitendawili aisee!

Muktasari:
Julai 3 mwaka huu, akiwa anazindua tamasha la kwanza la utamaduni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza mchakato wa vazi la Taifa kuendelea ulipoishia.
Julai 3 mwaka huu, akiwa anazindua tamasha la kwanza la utamaduni, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliagiza mchakato wa vazi la Taifa kuendelea ulipoishia.
Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita miaka kumi sasa tangu mchakato huo uliposimama. Akizungumza katika tamasha hilo la utamaduni, pamoja na mambo mengine, Waziri Mkuu alisema inasikitisha kuona hatuna vazi letu la Taifa hadi sasa na kutaka mchakato huo uendelee kama ambavyo wizara iliwahi kuahidi.
Waziri Majaliwa alisema katika mataifa mbalimbali duniani wanaposafiri wanakutana na watu wamejitambulisha kwa mavazi yao.
“Mfano Wachina wanajitambulisha kwa mashati yao yasiyokuwa na kola, Afrika Magharibi nao pia wana mavazi yao, je, Watanzania tunajitambulisha na nini?” alihoji Majaliwa.
Aliongeza: “Wizara ilishaahidi hili lakini mpaka sasa hakuna kilichofanyika. Naagiza wizara ikae pamoja na wadau, tafuteni alama ya Mtanzania ambayo tutakuwa tunavaa inatutambulisha”.
Moja kwa moja maagizo ya Waziri Mkuu Majaliwa yanakwenda kwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammedi Mchengerwa. Swali ni je, atauweza mfupa uliowashinda watangulizi wake?
Kwani mchakato wa kutafuta vazi la Taifa ulianza mwaka 2004, ambapo kuliundwa kamati maalumu na aliyekuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wakati huo, Dk Emmanuel Nchimbi.
Hata hivyo baada ya kutokea mabadiliko katika baraza la Mawaziri mwaka 2011 ambapo Dk Fenella Mukangara alikabidhiwa kusimamia wizara hiyo, kamati maalumu iliyoteuliwa kusimamia upatikanaji wa vazi hilo ilikabidhi michoro sita kutoka katika 200 iliyowasilishwa na wasanii mbalimbali katika wizara hiyo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo alikuwa Joseph Kusaga na Katibu ni Angela Ngowi, huku wajumbe wa kamati hiyo wakiwa ni Habib Gunze, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali, Makwaia Kuhenga, Ndesambuka Merinyo na Absalom Kibanda, ambaye baadaye alitangaza kujiweka kando.
Waziri Mukangara alionyesha shauku ya kuona vazi hilo linapatikana haraka na kwamba lingevaliwa katika maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanganyika yaliyofanyika Desemba 9, mwaka 2012. Lakini wapi, jambo hilo halikufanikiwa.
Hata wizara hiyo ilipokuwa chini ya Innocent Bashungwa, haikufanikisha hili na alipoulizwa kuhusu mchakato wa vazi la Taifa alisema apewe muda kwanza.
Mchakato wa vazi la Taifa ulivyoanza na kupotea...
Desemba 22, 2011, kamati maalumu ya kutafuta vazi la Taifa ilizinduliwa rasmi na Dk Nchimbi, aliyekuwa waziri mwenye dhamana wakati huo, tayari kuanza mchakato ambao ulipaswa kukamilika ndani ya siku 75.
Wakati wa shughuli za uzinduzi huo, Waziri huyo mwenye dhamana na kusimamia utamaduni, aliahidi kuwa mara baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi hiyo, ikiwamo kuainisha mapendekezo mbalimbali ya vitambaa vinavyoweza kufaa, Watanzania watakuwa wamepata vazi lao.
Aliainisha kuwa kamati hiyo haitaanza mchakato upya, bali wataendeleza walipoishia waliouanza mwaka 2004.
Septemba 10, mwaka 2012 baada ya mabadiliko ya baraza la mawaziri, kamati hiyo ilikabidhi ripoti kwa Waziri Mukangara aliyekuwa na Naibu wake, Amos Makalla.
Uwasilishaji wa ripoti hiyo ulifanywa na Katibu wa Kamati ya Vazi la Taifa, Angela Ngowi, akiwa na wajumbe wa kamati hiyo, Joyce Mhaville, Mustafa Hassanali na Ndesambuka Merinyo.