Vee money... na pamba kwa wajanja siyo ganja...
Muktasari:
Soko la Mwafrika liko Afrika. Mengine hayo ni ziada tu. Ngozi ya Vanessa Mdee haiwezi kuushawishi ubongo wa kijana aliyezoea kuiona ngozi ya Nick Minaj.
Umeshamuona Vanessa Mdee kwenye show zake? Ni kama yuko faragha na Jux wake. Achana na yule kiumbe. Muziki wake mzuri sana. Mavazi yake mabaya sana. Huyu utakutana naye mwisho wa makala hii.
Sasa leo na mimi nimeamua kidogo niwaweke sawa masela kuhusu mavazi. Hii siyo kwa wanamuziki wetu na wacheza sinema tu. Ni kwetu sote vijana nikiwemo mimi mwenyewe.
Iko hivi. Epuka kuvaa marangirangi wakati una mechi’ mavazi yako. Punguza idadi ya rangi. Usichanganye marangi mengi kama mimea na viumbe vilivyopo baharini.
Vaa kulingana na mazingira. Mjanja anajua kubadilika, sio kuvaa jezi la Man United lenye jina la Lukaku mgongoni kwenye sherehe.
Utakera watu tu na unaweza kupigwa kwa tatizo dogo mno. Yaani unaweza kumgusa bahati mbaya shabiki wa kule alikotoka Sanchez akakutandika makofi.
Kwa wale wavaaji wa masharti ya kuchomekea. Marufuku kuvaa shati linalopwaya kama umevaa tambara la mashineni. Pia usivae mlegezo.
Hakikisha ‘singlet’ haionekani. Au makubazi wenyewe mnaita ‘sendozi’. Kama umevaa pensi/kaptula. Vaa soksi fupi zisizoonekana.
Piga raba au makubazi/sandals bila soksi.
Haipendezi kuchomekea kindezindezi. Miguu iwe misafi pia acha upoyoyo.
Usivae shati jeupe kama la mwanafunzi wa Shule ya Msingi Makurumla. Shati nyeupe wakati unanunua hakikisha kuwe na aina flani ya urembo au nakshi yoyote ile kimtindo.
Suruali nyeusi kwa mwanaume yeyote yule wa kijanja anajua umuhimu wake. Inaweza kukaa kwenye mashati ya rangi nyingi. Suruali nyeusi siyo vazi tu bali ni hazina. Achana na kuficha uchafu.
Kama umevaa jeans/kadeti unaruhusiwa kuvaa saa ya aina yoyote. Kama umevaa suti/suruali ya kitambaa epuka kuvaa saa ya mkanda wa plastiki. Utaonekana kituko tu.
Kwenye suala la miwani pagumu kidogo. Cha msingi zingatia muundo wa kichwa chako pamoja na aina ya macho uliyonayo na aina ya pamba ulizovaa pia. Na uso wako ulivyo.
Siyo umepiga jeans kali, kichwa kama nembo ya WCB. Macho kama bundi uso wako kama barabara ya mwendokasi kisha unapiga miwani ndogo ya njano. Ni kituko.
Vaa kofia za kijanja. Kofia pia huongeza mvuto, chagua kofia kulingana na aina ya kichwa na mavazi uliyovaa.
Haipendezi kuvaa suti na kapelo. Kwa mfano kanzu ivaliwe na barakashia ndo utaeleweka la sivyo ni sawa na kuvaa dera tu.
Mjomba usinitie aibu. Usivae mkanda mrefu kama vile umefunga nyoka kiunoni.
Mikanda ya vitambaa au madoido mengi inafaa kuvaliwa na jeans/kadeti au kaptula.
Jitahidi rangi ya mkanda na viatu kama umevaa nguo za kuchomekea ziendane.
Pia upana wa mkanda na rux za suruali yako ziwiane. Siyo rux kubwa mkanda kama mnyoo.
Tupia cheni za ukweli. Mikufu ya kiume pia huongeza mvuto.
Kama umevaa nguo za kuchomekea au suti itapendeza ukivaa cheni ndogo ambayo haitokezi nje ya shati.
Kama umepiga pamba za kishua mfano tishirt na jeans hapa tupia cheni kubwa lakini hata cheni ndogo zinakubali.
Suala la tai inatakiwa uvae kulingana na urefu wako. Kama wewe mwembamba inapendeza kuvaa tai nyembamba.
Jitahidi kuzingatia tai na rangi ya shirt/suruali. Hakikisha tai yako imefungwa vizuri shingoni.
Wanaume wajanja wa mjini hupenda kupiga tshirt na jeans na chini kutupia raba kali. Vazi hili lina mvuto wa aina yake hasa likivaliwa kitaani na sehemu za mitoko kama vile kwenye klabu za starehe.
Usivae suruali ya kuchomekea na makubazi. Ukipiga jeans unaweza “kumechi’ tisheti/shati na rangi ya viatu.
Ukivaa suti lazima upige kiatu kikali. Hapa ukichemka itakuwa sawa na Toyota IST yenye matairi ya Fuso. Zingatia sana haya makitu ili next time uweze kuopoa hata mtoto wa kishua.
Unakuta mtu kavaa rangi kama bendera. Shati bluu.
Suruali njano. Sox kijani.
Mkanda mweusi. Tai zambarau. Viatu rangi ya maziwa. Lazima uchekwe.
Na sheria za suti, usitembee kwa miguu safari ndefu. Usiombe lifti kilofalofa fanya kama umeharibikiwa gari.
Usibebe pesa za vichelechele mfukoni. Na ukinunua kitu usiombe chenji. Utadhalilisha suti.
Na usitafune mahindi njiani kama ng’ombe. Dondoo za mavazi ni nzuri kwani zinatupa uelewa wa namna ya kuvaa.
Kuna watu walikosa wake wanaowapenda ka dhati kwa sababu ya mavazi.
Kwa wanaume, ili kuondoa mlolongo mrefu na kuumiza kichwa. Vaa suruali ya kadeti na tisilheti form six au shati la jeans au shati la kawaida.
Ni vizuri kama ni shati uchomekee. Hii unaingia popote, ofisini, biashara, kitaa, sherehe, baa na unaonekana ni mtu na heshima yako.
Sasa turudi kwa dada yetu Vanessa Mdee ‘Vee Money’. Msichana pekee anaye wakilisha kisahihi muziki wetu kwenye majukwaa ya kimataifa.
Pamoja na muziki wake mzuri. Bado suala la mavazi kwake limekuwa tatizo sugu. Na pengine ubora wa muziki wake unaficha ubovu wa mavazi yake. Kiasi kwamba watu hawalioni hilo.
Vee Money anavaa mavazi ya ajabu sana. Mavazi ambayo siyo ya kufumbiwa macho na wale wazee wa pale Ilala Basata.
Achana na video zake. Show zake tu ukimshuhudia namna anavyovaa lazima upigwe bumbuwazi. Mtoto flani hivi amazing. Sura. Umbo na uchangamfu wake.
Yote hayo na ubora wa muziki wake tunajikuta hatuoni kabisa. Tunakuwa bubu na vipofu wa mavazi yake. Vee Money anavaa mavazi ya tatanishi sana.
Najua kuna mapoyoyo utasikia amelenga soko la kimataifa. Mataifa gani? Mataifa ya dunia hii ya kina Miriam Makeba?
Dunia hii ya mwanamke kama Angélique Kpasseloko Hinto Hounsinou Kandjo Manta Zogbin Kidjo, maarufu kama Angélique Kidjo?
Hapana bana. Hao waliiteka dunia bila kuiga mavazi ya Madona. Miriam Makeba hakutaka kuvaa kama Tina Tunner ili aushawishi ulimwengu umtambua.
Soko la Mwafrika liko Afrika. Mengine hayo ni ziada tu. Ngozi ya Vanessa Mdee haiwezi kuushawishi ubongo wa kijana aliyezoea kuiona ngozi ya Nick Minaj.
Yaani kifupi ni kwamba kuikamata Afrika huhitaji kukaa utupu. Na kuikamata dunia huhitaji kuvaa kama Rihanna.
Kama Rihanna anabamba duniani wa sababu ya kuvaa mavazi tatanishi. Basi wasichana wetu hawa waanze kuanza zoezi la kuboresha ngozi zao kabla ya kuanza kuvaa mavazi tatanishi.
Unaweza kuvaa vazi tatanishi kama Beyonce lakini mpaka unakufa huwezi kufikia ubora wa ngozi ya Beyonce. Acheni kuiga tamaduni za wenzetu sana.
Kuvaa vibaya ni kuvaa vibaya tu. Usipojua kuvaa utadharaulika.